MANISPAA YAPORA ARDHI WANYONGE, YAUZA KWA VIGOGO

Eneo la Kilimahewa-Mitengo ambalo limetwaliwa na manispaa

MANISPAA ya Mtwara Mikindani imeingia kwenye kashfa ya kupora ardhi ya wanyonge na kuigawa kwa vigogo wa serikalini, wanasiasa  na wafanyabishara kinyume cha sheria.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya katika Mtaa wa Kilimahewa, Mitengo A na B, Mnazimmoja  kata ya Mitengo, Manispaa hiyo umebaini kuwa mbinu iliyotumika kupora ardhi hiyo ni kuitwaa kwa kuwalipa fidia ya sh. 100 kwa mita moja ya mraba wamiliki wa asili  na kisha kuwataka wailipie sh. 1200 kwa mita hiyohiyo ili wapate viwanja vya makazi.

Hali hiyo imesababisha wamiliki wa asili wa maeneo hayo ambao wengi wao wanakabiliwa na kipato duni kushindwa kulipia viwanja hivyo na kujikuta wakiambulia patupu, huku viongozi wa serikali, wanasiasa na wafanyabishara wakitumia mwanya huo kujilimbikizia viwanja hivyo.

Eneo la Kilahewa-Mitengo

Mbinu nyingine ni ile ya kuwataka kulipia viwanja hivyo miezi sita tangu walipolipwa fidia, hivyo kusababisha wakazi wengi wa eneo la Mitengo kugeuka mashuhuda wa ardhi yao ikimilikiwa na wenye uwezo.

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 pamoja na kanuni zake za mwaka 2011 inatamka kuwa mamlaka ya serikali inapotaka kutwaa ardhi ni lazima imlipe kwanza fidia mmiliki wa asili jambo ambalo halikufanywa na manispaa hiyo.

Uchunguzi pia umebaini kuwapo kwa maeneo ya ardhi yaliyotwaliwa na manispaa hiyo kutoka kwa wamiliki wa asili bila ya kulipa fidia.

Mohamedi Ali Nyama (68) na Nurudini Tindwa (37) wote wakazi wa Mtaa wa Mnazimmoja wanadai kuwa shamba lao lenye ukubwa wa hekari 50 limetwaliwa na manispaa hiyo mwaka 2002/2003 bila ya kuwalipa fidia.

“Shamba letu limetoa viwanja 87, sisi wenyewe hatukuhusishwa kwa namna yeyote ile … tumenyang’anywa eneo lote na sisi wenyewe hatuna hata kiwanja kimoja” anasema Tindwa

Anaongeza kuwa “Wale waliogaiwa viwanja ndiyo waliotulipa fidia ya mazao, miembe na mikorosho….mwaka jana tumelipwa sh. 1 milioni na manispaa kwa eneo la barabara, hakuna fidia yoyote ya ardhi tuliyolipwa”

Mkazi mwingine Hassan Mmasamba (68) mkazi wa mtaa Mnazimmoja kata ya Mitengo, alisema licha ya kuahidiwa kulipwa fidia kabla ya ugawaji, utekelezaji wake ulikuwa kinyume kwa madai viwanja viligaiwa kabla ya fidia.

“Nilikuwa na hekari mbili, nikalipwa fidia ya jumla ya sh. 533,000 kila mita moja ya mraba walinilipa sh. 100…baada ya miezi sita walinipa eneo kwa sharti nikalipie sh. 3,116,000 yaani kila mita moja ya mraba sh. 1200…mbaya zaidi kiwanja ambacho nilichagua nimebaidilishiwa” anabainisha Ismail Mpondomoka (28) na kuongeza

“Hadi leo sijalipia, sina pesa, licha fidia kuwa ndogo pia mda wa miezi sita kabla sijapewa kiwanja hivi unadhani bado nitakuwa na pesa ya fidia…nilikwenda mjini (Mtwara) kumtafuta mfanyabishara mwenye hela nimuuzie kiwanja changu”

Mohamedi Ali Nyama (68) kulia na Nurudini Tindwa wakionesha shamba laolenye hekari 50 lililoporwa na manispaa

Anasisitiza kuwa kitendo kilichofanywa na manispaa hiyo anakitafsiri kama mkakati wa makusudi wakuwahamisha wanyonge katika maeneo yao ya asili na kuwageuza kuwa walowezi wasio na makazi.

“Siwezi kuishi tena katika eneo hili, nalazimika kwenda kijijini ambapo naweza kupata ardhi…hii ni njama ya makusudi ya kutaka kutuondoa wanyonge katika mji wetu” anafafanua

Maeneo ambayo yamekubwa na mradi huo ni Mitengo A, B na Kilimahewa, ambapo wakazi hao wanadai viwanja vingi vimegaiwa kwa viongozi wa serikali, wanasiasa na wafanyabishara.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mnazimmoja katika kata hiyo ya Mitengo, Hassan Mkumbila anasema utekelezaji wa upimaji wa viwanja 1,200 vya makazi katika maneo yake umewanyanyasa wamiliki wa asili wa maeneo hayo ambapo licha ya wengine kukosa fidia pia umedhulumu haki yao ya kumiliki ardhi.

“Malalamiko yote yapo kwa mkuu wa wilaya, tumemweleza hali halisi, amesema anayashughulikia…ukweli ni kwamba ardhi yetu tumekuwa tukiporwa na mamlaka ambayo  tulidhani ndiyo ingekuwa mtetezi wetu” anaeleza Mkumbila

Anashauri kwamba “Walau wangesema mashamba tunawanyang’anya lakini viwanja tunawapa bure, sisi wakazi wa hapa hili suala limetubana sana kwa bahati mbaya hatuna pa kusemea”

Mthamini wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Steven Mwasitu anasema mradi wa upimaji viwanja Mitengo ulilega kupima viwanja vya makazi 1200 hata hivyo ulipima viwanja 884, ambapo viligaiwa kwa sh.1200 kwa mita moja ya mraba katika maeneo ya makazi na1500maeneo ya bianshara.

“Ni kweli sheria ya ardhi ya mwaka 1999 inata watu walipwe fidia kabla ya eneo lao kutwaliwa, lakini ‘practice’ (utendaji) za Tanzania zimekuwa aidha vikienda vyote kwa pamoja au fidia inafuata” anasema Mwasitu

Hata hivyo hakuweza kuzungumzia kwa kina mradi wa Mitengo baada ya Ofisa Habari wa Manispaa hiyo Jamadi Omar kumtaka ofisa huyo kutoendelea kujibu maswali yanayohusu mradi huo kwa madai tume imeundwa na mkuu wa wilaya hiyo kufuatilia suala hilo.

“Hili suala lipo kwa DC (Mkuu wa Wilaya) tunasubiri taarifa ya maandishi ili tuweze kujibu, sasa tukiruhus hapa kujibu kabla ya hiyo tume tutakuwa hatuko sahihi” alisema Omary

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile anakiri kuwa utekelezaji wa mradi huo umekiuka sheria ya ardhi na haujawatendea haki wamiliki wa asili wa maeneo hayo.

“Nilipopata malalamiko niliunda tume huru kuchunguza… Pasipo na mashaka yeyote tume imebaini kuwa utwaaji wa eneo hilo ulikiuka sheria ya ardhi ….pia tume imebaini kuwa viwanja vingi vimechukuliwa na viongozi wa serikali, wanasiasa, wafanyabishara” anasema Ndile

Anaongeza kuwa “Mfano ofisi ya DC wamepewa viwanja 12 wakati walioomba wanne… yupo kiongozi mmoja wa kuchaguliwa amepewa kiwanja, badae akahitaji kingine, alipokwenda manispaa anaambiwa kina mtu, yeye analazimisha anyang’anywe ili apewe yeye”

 

Anafafanua kuwa tume yake pia imebaini kuwa viwanja vimegaiwa lakini wamiliki hawajulikani huku maeneo mengine yakigaiwa viwanja kabla ya kufanyiwa tathimini na kulipa fidia.

“Nilitaka kujua nani anamiliki kiwanja namba ngapi nyaraka hizo hazipo…Yupo mama Fatuma Bishanga, yeye wamegawa viwanja katika shmba lake la hekari 11 hakuna uthamini wala fidia aliyolipwa … tunasema hii serikali gani isiyotenda haki kwawananchi wake” anabainisha mkuu huyo wa wilaya

Anafafanua kuwa pia vipo viwanja 41 vinavyogusa eneo la bomba la gesi ambapo alisema kwenye ramani havionekani, hali aliyotilia shka utendaji kazi wa maofisa ardhi katika manispaa yake.

“Kuna viwanja 90 vina ‘double allocations’ (vimegaiwa kwa watu zaidi ya mmoja) sasa kama wewe ni ofisa ardhi uliokwenda shule unawezaje kufanya mambo haya…nimesema hili nitaliongea na wala sitalifumbia macho” anasisistiza DC

Anaeleza kuwa tume yake imebaini kuwa wapo watendaji waliopoteza sifa ya kuendelea kuwa watumishi wa umma na hivyo suala hilo limepelekwa ngazi ya juu ili waweze kuchukuliwa hatua wakati viongozi wengine watashughulikiwa na mamlakahuska ikiwa pamoja na kufikishwa mahakamani.

“Tume imependekeza kuwa kuwapo na ukaguzi wa kiwanja kimoja hadi kingine ili kujua wamiliki wake, tena hiyo tume iwe imetoka nje ya Mtwara…watu hawamuogopi Mungu, wanawadhulumu wanyonge, nipo hapa kusimamia haki” anasisitiza Ndile

Anaongeza kuwa “Hili suala ndio kwanza limeanza kushughulikiwa, wananchi waendelee kuwa na subira, linapelekwa ngazi za juu kwa maamuzi zaidi…pia naomba niseme wazi kuwa tumeimebaini kuwa wakazi waeneo la Machame ni wavamizi”

Mwisho

Advertisements