MADIWANI MTWARA WAJIFUNZA KILIMO CHA KOROSHO

This slideshow requires JavaScript.

USAMBAZAJI hafifu wa matokeo ya teknolojia za utafiti wa kilimo na mifugo unaofanywa na taasisi ya utafiti kanda ya kusini Naliendele, mkoani Mtwara kwa wakulima umebainishwa kuwa miongoni mwa sababu za kilimo kuendelea kuwa duni katika mikoa ya kusini

Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa taasisi hiyo kanda ya kusini, Dk. Elly Kafiriti alibainisha hayo juzi alipokuwa akiitambulisha taaisi yake kwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara waliotembelea taaisi hiyo kujifunza kilimo bora cha korosho

Alisema hadi sasa matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa na wataalam katika taasisi hiyo ni kati ya asilimia 30 hadi 50 tu ndiyo yanayowafikia walengwa hali inayosababisha kudhorota kwa kilimo katika mikoa ya kusini inayojumuisha Lindi, Mtwara na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

“Mchango wa teknologia hizi ukiniuliza ni upi katika kuinua kilimona maisha ya wakulima, mimi siezi kujibu…ukienda kwa mkulima kule chini hali ni duni…kama wamepiga hatua ni kidogo sana, yaani huwezi kupima matokeo ya teknologia zetu, kama yapo ni machache….tufikirie kwanini” alisema Dk. Kafiriti

Aliongeza kuwa “Ulipomwacha mwaka 1976 hadi leo yupo vilevile kama amebadilika ni kidogo sana…sasa madiwani tushauriane nini tufanye ili teknolojia yetu iwafikie walengwa kwa urahisi na uhakika zaidi”

Alitaja sababu zingine kuwa ni pamoja uchache wa maofisa ugani, ukosefu wa fedha na mwamko mdogo wa wakulima kutumia teknolojia mpya za utafiti wa kilimo na mifugo.

Akichangia mada hiyo diwani wa kata ya Kianga, Mohamedi Liumba alisema wakulima wengi bado hawajanufaika na teknolojia za mazao zinazotolewa n taasisi hiyo kutokana na kuwapo kwa pengo la kuwafikishia

“Nina hakika kabisa matokeo ya tafiti zinazofanywa haziwafikii wakulima…tupo ngazi ya juu katika utafiti lakini mkulima wa kawaida hajui “ alisema Mohamedi

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Hamis Fundi alisema mafunzo hayo ya siku mbili kwa madiwani yamelenga kuongeza ufahamu wa madiwani hao juu ya kilimo bora cha zao kuu la biashara kwa wakazi wa mikoa ya kusini la Korosho.

“Diwani ndiye mwenye watu hivyo kwa kumwelimisha hapa ataweza kuwaelimisha wakulima wengi kupitia vikao na mikutano yake…sasa tunataka elimu hii iwafikie  wakulima wengi ili mabadiliko yaonekane” alisema Fundi

Mkurugezi Msaidizi wa Uendelezaji wa zao la korosho katika taasisi hiyo, Dr. Louis Kasuga Msipande alisema kitengo chake kwa sasa kinafanya utafiti shirikishi wa kuangalia upya umbali wa miche ya mikorosho kutoka shina moja hadi linguine.

“Umbali wa sasa wa mita 12 kwa 12 hadi 16 kwa 16, umelalamikiwa na baadhi ya wakulima kuwa mikorosho huwa karibu karibu, utafiti unaendelea kuangalia nafasi hizo kulingana na maeneo katika wilaya ya Newala, Nachingwea mkoani Lindi na Tunduru mkoani Ruvuma.

Aidha alipinga dhana kuwa wakulima wa korosho mikoa ya kusini wanapalilia mikorosho kwa kutumia moto, akisema suala hilo linakuzwa kisiasa japo halina ukweli.

“Kwa ukaaji wangu huku kwa maiaka mingi nimebaini kuwa hakuna mkulima anayedhamiria kuchoma moto shamba lake kupalilia shamba lake….tatizo ni kwamba wanachelewa kupalilia kwa hiyo watu wakichoma moto mapori huungua na korosho zake” alisema Dk. Kasuga

Mwisho

Advertisements