WAKONGWE WABWAGWA UCHAGUZI CCM MTWARA

Sura mpya zatesa, Mkuchika, Makame wapeta, Kamba chali

Alhaji Masoud Mbengule Katibu wa CCM mkoa wa Mtwara

UCHAGUZI wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) umefanika jana jumamosi katika wilaya zote Sita za mkoa wa Mtwara huku safu ya wenyeviti ikitawaliwa na sura mpya.

Ni mwenyekiti wa wilaya ya Masasi pekee, Kazumali Malilo aliyeweza kutetea kiti chake kwa kishindo kwa kumbwaga mpinzani wake Andrew Kasawala aliyeambulia kura 224, huku yeye akijizolea kura 1380 kati ya 1604 zilizopingwa.

Nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu (Nec) katika wilaya hiyo imetwaliwa na Pole Ramadhani Pole kwa kura 978 baada ya kumbwaga mpinzani wake Ketty Kamba aliyepata kura 489.

Katibu wa CCM wa mkoa wa Mtwara Alhaji Masoud Mbengule ameiambia Kusini ofisini kwake leo Jumapili  kuwa uchaguzi huo umepita salama huku nafasi nyingi za uongozi zikichukuliwa na sura mpya.

Alisema katika wilaya ya Newala, Ali Athumani Sadi ametangazwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya kupata kura 803 dhidi ya mtetezi wa kiti hicho aliyeangukiwa pua kwa kupata kura 721, huku nafasi ya Nec ikihodhiwa na George Huruma Mkuchika aliyepata kura 1001 na kuwabwaga  Abdallah Napinda (267) na Shaibu Namkuna (261).

“Tandahimba nafasi ya uwenyekiti ulirudiwa mara mbili baada ya aliyeongoza kutofikia nusu ya wapiga kura, ziliporudiwa Sophia Makonyola aliyekuwa anatetea kiti hicho alipata kura 619 na Abdul Haji Namtula alipata kura 980, hivyo Namtula ndiye mwenyekiti mpya wa CCM Tandahimba” alisema Alhaji Mbengule

Aliongeza kuwa “Nafsi ya Nec  jumla ya kura 1623, kura 38 ziliharibika…Balozi Rashid Makame kura 995, Namyundu Ali Salum kura 419 na Lihundu Abdallah Samli  alipata kura 171, hivyo M-Nec wa Tandahimba ni  Balozi Makame”

Alisema Mtwara mjini nafasi ya uwenyekiti imechukuliwa na Ali Mussa Chikanwene kwa kura 449 na kumbwaga mtetezi wa kiti hicho Yusuf Mineng’ene alipata kura 174, huku Hawa Mangasala akiambulia kura 35 na Bakari Mbwana kura 6kati ya kura 672 zilizopigwa huku 8 zikiharibika.

Katika nafsi ya Nec, Alhaji Mbengule alisema Godbless Kweka ameshinda nafasi hiyo kwa kura 373, na kuwabwaga Saidi Mussa Swalehe aliyepata kura 247, Phiri Makaburi (29) na Ernest Haule (16) kati ya kura 668 zilizopigwa huku 3 zikiharibika.

Kwa upande wa Mtwara vijijini, Ali Komba alimbwaga mtetezi wa kiti cha uwenyekiti  Ahmadi Likomba baada ya kupata kura 867 kwa 570 kati ya kura 1454 zilizopigwa huku kura 77 zikiharibika.

Aidha kwa upande wa Nec katibu huyo wa mkoa alisema Salehe Livanga aliwabwaga  Alhaji Mpeme (390) na Salehe Nandieti (156) baada ya kupata kura 816 kati ya 1416 zilizopigwa huku kura 54 zikiharibika.

“Wilaya ya Nanyumbu kura nafasi ya uwenyekiti ilirudiwa mara mbili, baada ya marudio matokeo yalikuwa, Muhata Masusa kura 407 na Ali Mohamedi Dua kura 395…mwenyekiti mtetezi Chibwana Mtimbe yeye alishindwa mapema” alisema alhaji Mbengule

Aliongeza kuwa “Nec, Hassan kambutu alipata kura 426 na kuwashindwa Rajabu Mrope aliyepata kura 361, Linga Idd Mpwanya kura 106 na Mwema Hassan Issa kura 67…M-Nec hapa ni Kambutu…uchaguzi umepita salama na sura mpya kama nilivyokueleza”

Mwisho

Advertisements