WAANDISHI ACHENI KUENDEKEZA NJAA

Deodatus Mfugale akisisitiza jambo

WAANDISHI wa Habari nchini wameaswa kutotumia maslahi duni yanayowakabili kuwa kigezo cha kukiuka maadili ya taaluma yao.

Rai hiyo imetolewa jana na waandishi wa habari wakongwe nchini, Chrysostom Rweymamu na Deodatus Mfugale wakati wa mjadala wa hatari za uhuru wa habari katika warsha ya maadili na Azimio la Dar es Salaam kuhusu uhuru na wajibikaji wa vyombo vya habari kwa wana habari  mkoani Mtwara.

Katika warsha hiyo iliyoandaliwana Baraza la Habari Tanzania wanahabari hao walisema licha ya ukweli kwamba maslahi duni ni moja ya changamoto inayominya uhuru wa habari, haipaswi kuchuliwa kama sababu ya msingi ya kukiuka maadili yao ikiwa pamoja na kupokea rushwa.

“Mwanzo wafanyakazi wa TRA (Mamlaka ya Mapato) walidhaniwa wanapokea rushwa kwa sababu mishahara yao duni, wakaongezewa, tujiulize je rushwa imekwisha au imeongezeka…suala hapa si maslahi, la muhimu tuzingatie maadili ya taaluma yetu” alisema Rweymamu.

Alifafanua kuwa “Suala la kufuata maadili ni la mtu binafsi, hata kama maslahi yataboreshwa aliyeooza atazidi kuoza tu…tuzingatie weledi wetu ili kulinda heshima yetu”

Akiwasilisha mada hiyo, Mfugale alibainisha hatari mbalimbali zinazoathiri uhuru wa habari kuwa ni maslahi duni, ujuzi mdogo, rushwa, vitisho vya dola na wamiliki wa vyombo vya habari binafsi.

Sospeter Magumba ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo alisema maslahi duni yanasababisha waandishi kukiuka maadili ya kazi yao kwa kupokea rushwa, ama kupidnisha ukweli kwa kujipatia maslahi yao binafsi.

“Tukumbuke, kuwa mwandishi wa habari haikupi msamaha wa majukumu ya kifamilia, unataka usomeshe watoto, uoe, ulipe pango la nyumba, matibabu…haya yote yanahitaji fedha kuyatimiza, sasa kama maslahi ni duni atawezaje kufanya hayo” alisema Magumba

Hoja hiyo iliungwa mkono na Godwin Msalichuma aliyesema kuwa licha ya ukweli kuwa wapo wenye maslahi mazuri lakini hawafuati maadili, bado kuna umuhimu wa kuboresha maslahi ya waandishi wa habari.

“Msingi wa maadili ni maslahi mazuri, waandishi walipwe vizuri, hapo utaona maadili na uhuru wa habari unakuwa…wapo wachache watakaokiuka lakini wengi watakuwa wamerudi kwenye mstari” alisema Msalichuma

Mwisho