BWENI LATEKETEA KWA MOTO CHUO CHA KILIMO MTWARA

This slideshow requires JavaScript.

BWENI namba mbili la Wanawake katika Chuo cha Kilimo Naliendele, Manispaa ya Mtwara-Mikindani limetekelea kwa moto na kusababisha hasara kubwa.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo moto huo ulizuka leo saa 8:30 asubuhi na kuteketeza bweni lote na vitu vilivyokuwamo ndani yake.

Habari zinasema kuwa hakuna mwana chuo yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo, mbali ya kupoteza vitanda, magodoro, nguo na vyeti na vyombo huku chanzo kikidaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.

“Tulikuwa darasani, mara tukaona moshi ukizuka kutoka kwenye hili bweni…tulipofika tulijitihadi kuuzima kwa kutumia mitungi ya gesi ya kuzima moto lakini haikusaidia kitu kwa sababu moto ulikuwa tayari umekolea” alisema Peterson Robert Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanachuo hicho.

Aliongeza kuwa “Haikuwa rahisi kuokoa vitu vilivyomo ndani, moto  ulianza mlango wa kuingilia na kama unavyoona madirisha yamefumwa kwa nondo…tunashukuru kwamba wakati moto unaanza wanachuo wote walikuwa darasani, bweni lilikuwa limefungwa”

Alieleza kuwa bweni hilo lilikuwa linalaza wanachuo 160 na kwamba  kutokana na moto huo vitu vingi ambavyo thamani  yake bado haijajulikana vimeteketea, huku akilalama kuwa tatizo la hitilafu ya umeme katika mabweni hayo limekuwa la mda mrefu .

“Kubwa ambalo wanachuo wanalia ni vyeti vyao vimeteketea kwa moto, wanajua namna ambavyo upatikanaji wa vyeti mara vinapopotea ulivyo mgumu…tunaomba serikali iliangalie hili kwa mtazamo wa kipekee…hii ni mara ya tatu hitilafu ya umeme inajitokeza kwa bahati nzuri hizo za awali tunakuwa karibu hivyo tunawahi kuzima umeme” alisisitiza Robert

Alifafanua kuwa gari la zima moto liliwasili saa moja tangu kuzuka kwa moto huo, huku tayari bweni hilo likiwa limeteketea kwa moto.

Mkuu wa Chuo hicho, Waziri Ali Mwinyi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa tukio kama hilo kutokea chuoni hapo tangu kujengwakwa chuo hicho mwaka 1975.

“Bado tunaendelea na uorodheshaji  wa mali zilizoteketea za wanachuo na thamani ya jingo ili tujue thamani ya vitu vyote vilivyotekea…chanzo kinadaiwa nihitilafu ya umeme” alisema Mwinyi

Mwisho