MADIWANI MTWARA WAPONDA POWERTILLER ZA PINDA

powetiller

MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani hapa wamesema matrekta madogo ya kulimia (power tiller) ambayo halmashaurihiyo iliyanunua ikiwa ni utekelezaji waagizo la Waziri Mkuu Mizengo Pinda hazijasaidia lolote katika kuinua hali ya kilimo wilayani humo.

Wakijadiliana njia bora za kuinua kilimo katika mafunzo ya kilimo bora yaliyotolewa na kituo cha utafiti wa mzao Naliendele mkoani hapa, madiwani hao walisema halmashauri zimeingia hasara kwa kununua ‘power tiller’ ambazo hazina msaada katika kilimo

“Huku kwetu power tiller hazijatusaidia kabisa…kwa sasa nyingi zimekufa na chache zilizobaki zinabeba abiria, mizigo…hakuna mabadiliko yeyote ya kilimo yalichagizwa na power tiller zile” alisema Hamisi Fundi Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

Alifafanua kuwa “Ili tuinue kilimo chetu msukumo uwekwe kwenye kununua matrekta makubwa…halmashauri zetu ziwadhamini wakulima ili wakakope matrekta sio power tiller…habari ya power tiller sitaki kuisikia tena”

Hoja hiyo iliungwa mkono na diwani wa  kata ya Kianga, Mohamedi Liumba aliyesema utekelezaji wa agizo hilo haukuzingatia mahitaji halisi yamaeneo huska na hivyo kusababisha kutofanikiwa kwa malengo kusudiwa.

“Kule kwetu power tiller zinabeba mizigo, abiria…hazilimi, sasa ili kilimo chetu kiboreke ni lazima tuangalie mfumo wa sera zetu za kilimo, kilimo kwanza imetufikisha hapa kwenye power tiller, ukweli ni kwamba kilimo chetu hakiwezi kusonga mbele kwa kutumia zana kama hizi” alisema Liumba

Aidha madiwani hao walipendekeza usimamizi wa sheria ndogo ya kilimo inayomtaka mkulima kufuata kanuni za kilimo bora inasimamiwa kikamilifu ilikuleta mageuzi ya katika  sekta hiyo mama.

Michango hiyo ilitanguliwa na maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo Kanda ya Kusini Dk. Elly Kafiriti aliyewataka madiwani kujadili njia bora za kuinua kilimo katika mikoa ya kusini ikiwa pamoja na namna ya kuisambaza teknolojia za matokeo ya utafiti yanayofanywa na kituohicho.

Alisema kwa kiasi kikubwa kudumaa kwa sekta ya kilimo katika mikoa ya kusini kunachangiwa na halmashauri kutokipa kipaumbele kilimo katika bajeti zao hali inayosababisha wakulima kutofikiwa na elimu ya kilimo bora.

“Halmashauri hazikipi kipaumbele kilimo, tunatoa teknolojia nzuri za kilimo lakini hakuna halmashauri yenye mkakati wa kuisambaza teknolojia hiyo kwa wakulima wake…hadi sasa ni asilimia 30 ya wakulima wetu ndiyo wanaofikiwa na teknolojia zetu…tujadiliane kwa nini hali ipo hivyo na nini kifanyike”  alisema Dk. Kafiriti

Mwisho

 

Advertisements