VIGOGO WANNE BODI YA KOROSHO KORTINI KWA RUSHWA

Ayoub Mbawa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Mtwara imewaburuza kortini vigogo wanne wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) wakidaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kutoa zabuni kinyume cha sheria.

Vigogo hao ambao ni wajumbe wa bodi ya zabuni ya CBT, wamefikishwa jana (leo) mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wilaya ya Mtwara, Joseph  Fovo kujibu tuhuma zinazowakabili.

Mwendehsa mashtaka wa TAKUKURU, Eveline Onditi aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa namba moja Ayoub Mohamedi Mbawa (59) ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa CBT, ndiye pia mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni.

Aliwataja watuhumiwa wengine kuwa Mariam Ally Chimbyangu (37) ofisa manunuzi ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Zabuni ya CBT, Mhandisi Shabani Yahaya Misuli (52) meneja wa mafunzo na ubanguaji na Mohamedi Hanga Mkurugenzi wa Masoko na Huduma za Mawasiliano wajumbe wa bodi.

Mwendesha mashtaka huyo, alisema kati ya kipindi cha Novemba, 2008 na Mei 2009 watuhumiwa hao wakiwa wajumbe wa bodi ya zabuni kwa pamoja wanadaiwa kutumia vibaya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kwa kushindwa kutangaza tenda.

Onditi alisema pia watuhumiwa wote wanadaiwa kutoa tenda bila ya kuwapo kwa taarifa ya kamati ya tathimini jambo ambalo ni uvunjaji wa sheria katika utendaji wao wa kazi.

Hata hivyo haikuelezwa mahakamani hapo zabuni hiyo ilihusu nini na iligharimu kiasi gani.

Watuhumwa watatu, Mbawa, Simuli na Hanga ndiye waliopandishwa kizimbani, huku mtuhumiwa Chimbyangu hakutokea mahakamani hapo, hali iliyoilazimu mahakama kutoa hati ya kukamatwa ili afikishwe kujibu tuhuma zake.

Watuhumiwa wote wapo nje kwa dhamana baada ya kukana mashtaka yanayowakabili hadi Novemba, 6 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Mwisho