MTWARA WAONJA LAANA YA GESI

This slideshow requires JavaScript.

WAKULIMA wa Kijiji cha Mangamba Manispaa ya Mtwara-Mikindani ambao bomba la gesi linalojengwa na Serikali kutoka kijiji cha Msimbati halmashauri ya Mtwara kwenda Jijini Dar es Salaam limepita katika mashamba yao wanalalamikia mradi huo kuwa umedhulumu jasho lao wakati wa ulipaji wa fidia.

Fidia ambayo inalalamikiwa na wakulima hao ni ya mazao, hususani zao la Muhogo walilolipwa kwa thamani ya sh. 130 kwa shina kiwango ambacho wamesema ni kidogo kuliko thamani ya zao hilo.

Wakizungumza na mwandishi wa makala haya kwa nyakati tofauti wakulima hao waliwatupia lawala wathamini waliothamini mazao yao huku wakisema kuwa ndiyo matunda ya kuwa na wasomi wasiojua thamani ya mazao ya kilimo.

Abdallah Rahisi Nyodo (34) mkazi wa Mangamba  ni miongoni mwa wakulima ambao wamepoteza mashamba yao baada ya bomba la gesi kupita katika eneo hilo, anasema ulipaji wa fidia ya mazao haukutenda haki kwa zao la Muhogo kwa kulishusha thamani.

“Hadi leo hatuamini kama kweli serikali inaweza kufanya dhuluma hii kwa wakulima wake…shina la Muhogo wametulipa kwa sh. 130 hivi kuna haki hapo?…shina hili la Muhogo mkulima ametumia misimu miwili hadi mitatu kulihudumia leo analipwa bei ya kipande cha Muhogo wapi haki?” anahoji Nyodo

Anaongeza kuwa “Malipo haya yamefanywa na TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania), hebu jiulize leo hii shina la Muhogo ukiuuza kwa wachuuzi utapata sh. 5,000 hadi 7,000, hii ni bei ya shamba, ukileta mjini tenga la mashina matano ya Muhogo mbichi utauza sh. hadi 50,000 au sh. 40,000”

Anabanisha kuwa shamba lake lilikuwa na Mihogo 486 ambayo amelipwa fidia ya sh. 130 kwa shina hiyo kumwezesha kupata jumla ya sh. 63,180 badala ya sh. 2,430,000 iwapo mashina hayo angeyauza kwa wachuuzi kwa bei ya sh. 5000 kwa moja.

“Muhogo kwetu ndiyo zao kuu la chakula, ndiyo kimbilio letu…kwenye shina moja unaweza kupata Mihogo mikubwa hadi kumi ambayo ukiamua kuiuza kwa rejareja kila muhogo unaweza kutoa vipande kumi vya sh. 100 kwa kila kimoja” anafafanua mkulima huyo.

Anabainisha kuwa “Hapa gesi hatuwezi kuitazama kwa jicho la ukombozi bali ni janga linalopora kidogo tulichonacho…kama wapo wanaosema gesi ni neema basi ni kwa upade wa Serikali, sio sisi wakulima”

Naye Ali Abdallah Mabangi (38) mkazi wa Mangamba anasema shamba lake lenye mashina ya mihongo 280 lilimwezesha kupata fidia ya jumla ya sh. 36,400 ikiwa kila moja lilipwa kwa sh.130.

“Fidia ya zao la Muhogo kwa kweli imenigandamiza, ni heri wangeniambia ning’oe mihogo yangu nikatafute kwa kuuza kuliko kulipwa fidia hii…ningeuza zaidi ya sh. 5000 kwa shina…mihogo yangu nimeihudumia kwa miaka mitatu leo nalipwa sh.130 kwa shina, sio haki” anasema Mabangi

Anafafanua kuwa “Mbegu ya mihogo kutoka kituo cha utafiti Naliendele tunanunua wastani wa sh. 200 kwa mti, leo shina tunalipwa kiasi kidogo kama hiki, shina ambalo unaweza kula wewe na familia yako mkashiba, hivi kosa letu ni kuwa wakulima?…hizi ndizo athari za kuwa na wataalam wasiojua thamani ya kilimo na mazao”

Akionesha kwenye jazba Mabangi alisema “Sisi waathirika wa gesi sio wafaidika, leo hii tukitaka kula Muhogo tunanunua kwa wasioathirika, kwa fidia hii siwezi kununua shamba lingine tena…kwa sisi wakulima ukikosa shamba ndiyo masikini daima”

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mangamba Mwanusa Hassan (47) anathibitisha wakulima wake kulipwa fidia isiyoendana na thamani ya zao la Muhogo na kuongeza kuwa wakulima hao wanakosa wa kumlalamikia kutokana na kazi hiyo kufanywa na maofisa wa TPDC kutoka Dar es Salaam na kisha kuondoka.

“Wakulima walijaribu kupinga fidia hiyo, lakini wakaambiwa haiwezi kubadilishwa kwa sababu ndiyo iliyotolewa na Serikali, wamebaki wanauguza maumivu ya kuporwa nguvu zao na serikali” anasema Hassan ambaye wakati wa ulipaji wa fidia alikuwa kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Mangamba

Yusuf Namkwinda (30) mkazi wa Majengo Manispaa ya Mtwara Mikindani ni mchuuzi wa biashara ya mihogo mibichi ambayo huikaanga  na kuiuza (chips dume), anasema kwa sasa Mihogo mibichi baridi ananunua kati ya bei ya sh. 4000 hadi 5000 kwa shina la muhogo.

“Ninapokwenda shambani kununua mihogo huwa nanunua shina kwa bei kati ya sh. 4000 hadi 5000 kutegemea ukubwa wa shina, katika shinamoja hadi mihogo 10 mikubwa…wanapoleta hapa mjini nanunua tenga moja la mihogo kati ya sh. 40,000 hadi 45,000” anasema Namkwinda

Anafafanua kuwa “Tenga huwa na mihogo kati ya 70 hadi 80, nikiuza shina moja naweza kupata kati ya sh. 10,000 hadi 12,000, nauza kipande cha muhogo mbichi sh. 200, muhogo mmoja unaweza kutoa vipande kati ya saba hadi 10…nakaanga chips dume kipande sh. 100 muhogo mmoja unaweza kutoa vipande hadi 20…tenga moja naweza kupata kati ya 55,000 hadi 70,000”

Mmoja wa wataalam wa kilimo Manispaa ya Mtwara-Mikindani Salum Mnyitu asema thamani ya uzalishaji wa zao la muhogo kwa shina moja inakadiriwa kufikia kati ya sh.2500 hadi 3500.

“Kutokana na ardhi yetu kuchoka (kukosa rutuba) huwezi kuzalisha muhogo kwa msimu mmoja ukawa umekomaa …kuanzia misimu miwili hadi mitatu ndipo muhogo unakuwa tayari  umekomaa na unaweza kutoa mazao mazuri, zaidi ya palilizi sita unafanya kwa wastani wa palilizi mbili kwa msimu” anasema Mnyitu

Anafafanua kuwa “Si haki kulipa sh. 130 kwa shina la muhongo hata kama lina msimu mmoja tangu lilipopandwa bado gharama za kulitunza ni zaidi ya sh. 130, ukizingatia mbegu nayo wanainunua…wameshindwa kuthaminisha zao hili, thamani yake ingeangaliwa kwa kuangalia umuhimu wa zao hilo kwa wakulima wenyewe”

Mbunge wa Mtwara mjini, Asnain Murji anasema hajapata malalamiko rasmi kutoka kwa wakulima hao licha ya kukiri kuwa kiwango walicholipwa ni kidogo ukilingalisha na thamani ya zao hilo na gharama za uzalishaji.

“Nitafuatilia hilo, nipe mda …ninachofahamu ni kwamba serikali ndiyo iliyopanga viwango hivyo…kama wamelipwa hivyo si haki, thamani ya muhogo kwa walaji ni kubwa” anasema Murji

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani na mwandishi wa makala haya kupata ufafanuzi wa madai ya wakulima hao alionekana kulikwepa kuzungumzia jambo hilo.

Baada ya mwandishi kuomba ufafanuzi wa suala hilo Waziri Muhongo aliomba ampigiwe baadae, alipopigiwa badae hakupokea simu bali alijibu kwa ujumbe wa maneno uliosomeka “I’m in meeting” (nipo kwenye mkutano)

Mwandishi alimuomba ahadi ya muda wa kuongea nae kwa ujumbe wa maneno katika simu ya kiganjani ambapo alijibiwa kwa ujumbe uliosomeka “After 2:00 hrs” (baada ya saa mbili usiku), alipopigiwa simu mda huo anasema “nipigie kesho kuanzia saa tano, nitakuwa ofisini sina ratiba ya vikao”

Siku iliyofuata Oktoba 11, mwaka huu alipopigiwa saa tano kama alivyohaahidi, simu yake iliita bila kupokelewa na mda mfupi baadae alituma ujumbe wa maneno uliosomeka “I’m in meeting” (nipo kwenye mkutano)

Mwisho

Advertisements