NIMEISHI NYUMBA MOJA NA WANAUME WAWILI KWA MIEZI KUMI

This slideshow requires JavaScript.

UKISTAAJABU ya Mussa utayaona ya Filauni ndivyo wahenga hunena katika dunia hii iliyojaa kila aina ya matukio ya kustaajabisha.

Katika miaka ya hivi karibuni wanawake ulimwenguni wamekuwa mstari wa mbele kudai usawa na kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwemo kuolewa mitala wakidai kitendo hicho kinadhulum haki yao ya kupata upendo wa dhati kutoa kwa waume zao.

Licha ya baadhi ya dini kuruhusu ndoa za mitala bado wanawake wengi wamekuwa hawaungi mkono utamaduni huo ambao umeenea zaidi katika nchi za Kiafrika na Uarabuni.

Katika hali tofauti na mazoea ya wengi katika kijiji cha Mkoma wilaya ya Newala mkoani Mtwara, Fadina Abdallah (38) anawashangaza wengi baada ya kuamua kuishi na wanaume wawili nyumba moja kama mke na waume.

Ilinichukua saa mbili na nusu kwa usafiri wa Pikipiki kwa spidi ya kilomita 70 kwa saa kufika kijiji hicho kilichopo Kaskazini mwa mji mkongwe wa Newala, kilomita 150 Kusini Mashariki mwa mji wa Mtwara.

Akionekana  mwenye furaha tele mda wote Fadina anasema “Ni kweli nimeishi na wanaume wawili nyumba moja…ni huyu unayemuona na mwingine nimetenganane mwezi wa Saba mwaka huu…nimeishi nao kwa miezi kumi kabla sijaamua kutengana na mmoja”

Anaeleza kwa “Mwaka 1999 niliolewa na mume wangu wa kwanza huyu ninaishi naye sasa ambaye tuliachana mwaka 2009…mwaka 2011 niliolewa na mwanume mwengine (Bakari Sijaona) ambaye tumetengana hivi karibuni”

Akihadithia kilichotokea binti huyo anasema wakati wa uhai wa ndoa yao na mumewe wa kwanza walifaikiwa kujenga nyumba moja ya nyasi ambayo aliachiwa baada ya kutengana.

Anafafanua kuwa akiwa anaishi katika nyumba hiyo kwa mda wa miaka miwili peke yake, badae alimpata mwanaume ambaye alioana naye Septemba 2011 na hivyo kuanza maisha mapya ya ndoa.

“Kabla ya kuolewa tena huyu jamaa (mumewe wa kwanza) alikuwa anakuja nyumbani na kuniomba turudiane lakini nilikuwa namkatalia, nilitaka mda wa kupumzika maisha ya ndoa” anasema dada huyo akicheka

Anaongeza kuwa “Huyu mume wangu mpya alikuwa mgeni hapa kijijini, hakuwa na nyumba ya kuishi, alihamia kwenye nyumba yangu…nakumbuka, ulikuwa usiku nilisikia mlango unagongwa na nilipokwenda kuufungua nilimkuta mume wangu wa zamani”

Anasema baada ya kusabiana, mumewe huyo wa zamani alimwambia anahitaji kulala ndani ya nyumba hiyo kwa kuwa amefukuzwa katika nyumba aliyokuwa anaishi awali.

Anaeleza kuwa alirudi ndani kuongea na mumewe ambapo walikubaliana wampe hifadhi kwa siku hiyo ili asubuhi atafute sehemu nyingine ya kujihifadhi.

Anasema asubuhi mgeni wao huyo hakuonesha dalili zozote za kuondoka nyumbani hapo na walipojaribu kumuhoji alisema hawezi kuondoka kwa sababu hakuwa na sehemu nyingne ya kuishi na kwamba nyumba hiyo aliijenga kwa nguvu zake.

“Sikuwa na la kufanya hivyo  tuliamua kuishi wote katika nyumba hiyo…nashukuru Mungu kwamba walikuwa wanaelewana, hawakuwahi kugobana hata siku moja…tulikuwa tunaishi vizuri mimi nikiwa mke na wao waume zangu” anasema Fadina huku akionesha kufurahishwa na maisha hayo

Anaongeza kuwa “Nilikuwa napika chakula tunakula wote, shambani tunakwenda wote, mimi nalima katikati, huku mmoja na upande mwingine …sikuwahi kumpelekea maji ya kuoga msalani mwanaume yeyote maana niliogopa kuonekana nampendelea mmoja, kila mtu alikuwa anajipelekea maji ya kuoga msalani”

Anasema hakuwa na la kufanya kwa sababu wanaume wote walikuwa wanamtamkia kuwa wanampenda na vile nyumba yao hiyo ilitawaliwa amani, furaha na upendo licha ya kuwa hakuwa na pakuishi mbali ya nyumba hiyo.

“Kila mmoja alinipenda kwa dhati…mwanzo nilipata shida sana nikiwaza jamii itanionaje, lakini badae niliona ni jambo la kawaida…nakumbuka baba mzazi aliwahi kuja na kunikemea juu ya jambo hilo lakini nilimweleza sikuwa na la kufanya kwa wakati huo” anasema dada huyo ambaye hajabahatika kupata mtoto hadi sasa.

Akizungumzia kitu ambacho jamii iliyomzunguka ilikuwa haikifahamu anasema katika kipindi chote cha maisha yake ya kukaa na wanaume wawili katika nyumba moja hakuwahi kuweka zamu ya kulala.

“Watu wanadhani nilikuwa naweka zamu ya kulala, yaani leo kwa huyu kesho kwa yule, nilikuwa nalala na mume wangu wa wakati huo, huyu aliyekuja kuomba hifadhi siku zote alikuwa analala peke yake ila huduma zingine alikuwa anapata kama mkewe” anasema huku akionesha msisitizo katika hilo

Anasisitiza “Ni vugumu jamii kuamini hilo kwa sababu walikuwa wanatuona tunalala na kuamka nyumba moja, ukizingatia kuwa wote walinioa ndoa, sio kaka zangu, lakini ukweli utabaki kuwa nilikuwa silali na wote”

Anabainisha kuwa aliishi katika maisha hayo kwa miezi kumi kabla ya Julai mwaka huu alipotengana na mumewe huyo baada ya kuhitilafina ndani ya nyumba yao kulikosababishwa na ulevi wa mwanaume huyo na kufuja fedha ya mradi wa maandazi.

“Nilikuwa naumwa nikamuomba mwenzangu apeleke maandazi kwenye mkesha wa unyago, aliondoka na maandazi 220, cha ajabu siku hiyo hakurudi hadi siku ya pili nilipomfuata …nilimkuta amelewa, maandazi yameisha na pesa hana, nilifuatana naye hadi nyumbani, nilipomuuliza fedha ipo wapi alianza kunipiga na kunisema ovyo” anahadithia Fadina na kuongeza

“Jamaa zangu walikuja juu ukizingatia nilikuwa mgonjwa…nilichoamua kuomba talaka na ndipo nilipoachana naye…kwa sasa sifikirii kuolewa, napumzika kwanza ingawa yule niliyetengana nae ananiomba turudiane na huyu nilinaye anaomba tufunge ndoa tena…mimi nimesema kwa sasa sipo tayari, niacheni kwanza”

Mwandishi wa makala haya hakuweza kuongea na Sijaona baada ya jitihada za kumpata kutozaa matunda kutokana na kuhama kijiji hicho na kwenda kuishi mkoa wa Lindi

Hata hiyo nilifanikiwa kuongea na Ali Namtokwete (47) mume wa kwanza wa Fadina ambaye anathibitisha kuwa ameishi na mtalaka wake huyo akiwa na mume mwingine katika nyumba moja chumba tofauti kwa kipindi cha miezi kumi na kwamba kwake haikua tatizo.

“Ni kweli nimeishi na mwanaume mwenzangu katika nyumba moja nikiwa na huyu mwanamke na mumewe mpya, tulikuwa tunaishi kama ndugu, hatukuwahi kugombana na wala mimi sikuwahi kulala kitanda kimoja na huyu mwanamke…alikuwa ananihudumia kwa mahitaji mengine na si tendo la ndoa” anasema Namtokwete

Anaongeza kuwa “Unajua wakati mimi sijaachana na huyu mwanamke tulikubalina kuhudumiana hadi kifo kitakapotutenganisha hivyo ili niweze kutimiza ahadi yangu hiyo iliniladhimu kusogea karibu na yeye”

Anabainisha kuwa jamii inayowazunguka ililipokea kwa mitazamo tofauti tukio hilo hasa likizingatiwa si la kawaida, hata hivyo mapokeo hayo hayakuweza kurudisha nyuma ahadi yake ya kumuhudumia mtalaka wake.

“Wakati tupo kwenye ndoa yetu, nilipatwa na maradhi ya mda mrefu, huyu mwanamke aliniuguza kwa moyo wa upendo, pia alihakikisha napona maradhi hayo, sikuwa na cha kumlipa bali kumuahidi nitamhudumia maishani mwake , naye aliniahidi hivyo” anasema Namtokwete

Anabainisha kuwa ameishi na mume mwenzie kwa amani na upendo hadi tofauti zao zilipowatenganisha na kwamba kwa sasa anatarajia kufunga nae ndoa nyingine mwanamke huyo.

“Hakuna mkono wangu katika kuvunjika kwa ndoa yao…kwa kuwa wao wameachana mimi nandaa utaratibu ili nifunga naye ndoa nyingine…bado nampenda mke wangu na kama unavyoona tupo hapa na tunaendelea na maisha yetu kama kawaida” anaeleza mwanaume huyo huku akionekana mwenye furaha na kuongeza

“Kuna wakati mwenzangu alikuwa aniamini alidhani namzunguka hivyo alikuwa anaaga anasafiri alafu utashangaa anarudi ghafla usiku akidhani atanifumania…nadhani badae aligundua hicho kitu hakipo akaacha kufaya hivyo”

Daima Mohamed mkazi wa kijiji hicho anasema yeye pamoja na wanakijiji wenzake walikuwa wanahisi mwanamke huyo alikuwa anashirikiana naye tendo la ndoa wanaume wote kwa zamu hali iliyowafanya wamuone mwanamke asiye na maadili.

Anabainisha kuwa kimsingi kilichokuwa kinaendelea ndani ni siri ya watatu hao na kwamba jamii imehukumu suala hilo kama kinyume na maadili kutokana na mtazamo wa nje kwa kuzingatia wote hao walimuoa ndoa ya kiislamu.

“Unajua hili si tukio la kawaida, huwenda halijawahi kutokea, tunafahamu usaliti kwenye ndoa upo lakini si kama huu wa mwanamke kukaa na wanaume wawili kwenye nyumba moja…kwetu sisi tulikuwa tunawashangaa namna wanavyoishi…kikubwa kilichotushangaza ni kuona wanaume hao wanavyoweza kusihi bila ugomvi” anasema Mohamed

Anaongeza kuwa “Maisha yao yalikuwa daima ya furaha, walikuwa wanashirikiana shambani na hata shughuli za kijamii…hakuna aliyeonekana kujali maneno ya watu, utadhani waligeuza mbolea yakustawisha upendo wao”

Mwenyekiti wa Baraza la WaislamTanzania mkoa wa Mtwara, Sheikh Marijan Dadi anasema kwa mujibu wa uislam hakuna tatizo lolote watu hao kuishi pamoja iwapo mwanamke alikuwa hatembei na wanaume wote.

“Uislamu inaruhusu wanaume kuoa wanawake wengi lakini si mwanamke kuolewa na wanaume wengi kwa wakati mmoja, msingi hapa ni kwamba iwapo mwanamke atafanya hivyo itakua vigumu kutambua watoto ni wa baba yupi…kama alikuwa analala na mumewe wa ndoa tu hapo hakuna tatizo” anasema Sheikh Dadi

Mwisho

Advertisements