RAIS AONGEZEWE MADARAKA

This slideshow requires JavaScript.

WAKAZI wa kijiji cha Msijute, Halmashauri ya wilaya Mtwara, mkoani hapa wametaka katika Katiba ijayo Rais aongezewe madaraka ili kumpa nguvu ya kufanya maamuzi.

Wakitoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya Katiba jana wakazi hao bila kufafanua aina ya madaraka anayopaswa kuongezewa Rais  walisema hawaoni umuhimu wa kupunguza madaraka ya kiongozi huyo wa juu wa nchi.

Saidi Nawanda (62) na Selemani Likoko (68) kwa nyakati tofauti walisema mamlaka aliyonao Rais kwa sasa hayatoshi hivyo ni muhimu aongezewe.

“Rais aongezewe madaraka, ili akisema jambo basi litekelezwe” alisema Nawanda bila ya kufafanua madaraka anayopaswa kuongezewa.

Maoni kama hayo pia yaliyolewa na Likoko, ambaye alihoji iweje Rais apunguziwe madaraka badala ya kuongezewa.

“Rais aongezewe madaraka, iweje apunguziwe” alisema Likoko

Katika mkutano huo ulioendehswa na mwenyekiti Sengondo Mvungi, ulitanguliwa na maelezo ya umuhimu wa kutoa maoni ya Katiba yaliyotolewa na mjumbe wa Tume hiyo, Kibibi Hassan ambaye aliwaambia ni wakati muafaka kwao kutengeneza katiba waitakayo.

“Tumieni fursa hii kutoa maoni yetu…jisikieni huru, utakachosema ndicho kitakachonukuliwa, baada ya hapa tutarudi kwenu tukiwa na rasim ya Katiba, safari hiyo tutaiwasilisha kwenu kupitia mabaraza ya wilaya” alisema Hassan

Aliongeza kuwa “Tutaipeleka kwenye Bunge maalum la Katiba na baada ya hapo italewata kwenu kwa ajili ya kupigia kura ya ndiyo na hapana…msiwe na wasiwasi, hii ni Katiba yenu”

Mwisho

Advertisements