TUNATAKA SERIKALI YA UMOJA WA KITAIFA

This slideshow requires JavaScript.

MKAZI wa kijiji cha Chekeleni, halmshauri ya wilaya ya Mtwara, mkoani hapa, Hamis Hassan Mnova (26) amependekeza Katiba ijayo itambue uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Akitoa maoni yake mbele ya Tume ya Katiba katika kijiji cha Kitere juzi, Mnova alisema angependa kuona Katiba ijayo inaruhusu uwapo wa Serikali ya Kitaifa ili mawaziri watoke kwenye kila chama cha siasa.

Akifafanua hoja yake hiyo alisema kwa sasa licha ya kuwapo kwa watu wenye uweo wa kuongoza wanakosa nafasi kutokana na kuwa wabunge kupitia vyama pinzani jambo ambalo linadhorotesha maendeleo ya nchi.

“Mawaziri naomba watoke vyama vyote vya siasa, yaani Katiba iruhusu serikali ya Umoja wa Kitaifa” alisema Mnova

Pamoja na hilo, mkazi huo alipendekeza Katiba kupunguza idadi ya vyama vya siasa na kubaki vinne ili viweze kutoa ushindani wenye tija.

“Vyama vya siasa vibaki vinne” alipohojiwa na mwenyekiti wa mkutano huo, Mohamed Yusuf Mashamba ambaye ni mjumbe wa Tume hiyo kuwa vyama vingine viende wapi, Mnova alijibu “Vijiunge na vyama hivyo  vinne, venyewe vitakubalina vipi vife na vipi viimarishwe”

Aidha mkazi mwingine Issa Seleman Namdimba (43) wa kijiji cha Lilido alipendekeza Katiba igawe Taifa katika majimbo  kwa kuzingatia kanda zilizopo.

Alisema hatua hiyo itawezesha rasilimali za sehemu husika kunufaisha watu wa eneo hilo na hivyo kuharakisha maendeleo.

Pia alipendakeza kuwa viongozi wanapoapa washike Katiba badala ya vitabu vya dini kwa sababu serikali imetamka haina dini.

“Kiongozi anapoapa anaapa kuitumikia serikali na sio dini, na kwa kuwa serikali haina dini basi kiongozi yeyote anapoapa atumie Katiba” alisema Namdimba.

Awali Mshamba aliwataka wananchi kuwa huru kutoa maoni yao na kwamba kila maoni yatachukuliwa na kuheshimiwa, huku akiwataadharisha wananchi hao kushangilia pale mtu anapotoa maini yanayomgusa au kuguna pale anapotoa maoni kinyume na mtazamo wake.

mwisho