WANASIASA WAONGO WAFUKUZWE, WASHITAKIWE

This slideshow requires JavaScript.

MKAZI wa kijiji cha Libobe kata ya Kitere halmashauri ya wilaya ya Mtwara, mkoani hapa, Saidi Hassan Changu (44) ametaka Katiba mpya iruhusu kushitakiwa kwa kosa la jinai wanasiasa watakaoshindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi, pamoja na kuondolewa madarakani kabla ya miaka Mitano kwisha.

Akizungumza mbele ya Tume ya Katiba ilipotembelea katani humo na kufanya mkutano wa kukusanya maoni katika kijiji cha Kitere juzi, mwananchi huyo alisema kuwa Madiwani, Wabunge na Rais wapimwe utekelezaji wa ahadi zao, mara wanapotimiza nusu muhula wa uongozi wao.

Alisema inapobainika kuwa kiongozi huyo ameshindwa kutimiza ahadi zake kwa asilimia 50 katika kipindi hicho cha nusu muhula, Katiba iruhusu kuondolewa madarakani kwa kiongozi huyo na kushitakiwa kwa kosa la kudanganya wananchi.

Changu alifafanua kuwa hatua hiyo itaondoa viongozi waongo wanaopata uongozi kwa kutoa ahadi hewa kwa wananchi na hivyo kudidimiza maendeleo.

“Nataka Madiwani,Wabunge na Rais wakishindwa kutekeleza nusu ya ahadi zao kwa wananchi inapofikia nusu muhula, basi Katiba iruhusu watu hao kuondolewa madarakani na kushitakiwa kwa kosa la jinai la kujipatia uongozi kwa njia ya udanganyifu” alisema Changu

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mohamed Yusuf Mashamba alipojaribu kumuhoji utata utakaojitokeza kwa kuwa viongozi hao wanatoa ahadi kwa mujibu wa Ilani za vyama vyao, hivyo kuwa vigumu kwao kushitakiwa, Changu alisema

“Zipo ahadi za vyama na zipo ahadi za mgombea binafsi, hapa nazungumzia ahadi za mgombea binafsi…haya ndiyo maoni yangu mimi, naomba iandikwe hivyo”

Mashamba alimuondoa hofu mtoa maoni huyo kwa kumueleza kuwa “Maoni yako tumeandika kama ulivyosema, nilichokuwa najaribu kukueleza ni utata unaoweza kujitokeza”

Pia mkazi huyo alipendekeza wenyeviti wa halmashauri, Meya, na Spika wa Bunge wasitokane na madiwani na wabunge ili kuepuka ushabiki wa kisiasa katika kufikia maamuzi na iwe rahisi kwao kuwawajibisha.

Mwisho

Advertisements