MANISPAA MTWARA YABOMOA NYUMBA YA ASIYEONA

This slideshow requires JavaScript.

FAMILIA Nane katika Mtaa wa Sino kata ya Ufukoni Manispaa ya Mtwa Mikindani zimepoteza makazi baada ya nyumba zao, ikiwemo ya mtu asiyeona kubomolewa na manispaa hiyo.

Wakizungumza katika eneo la tukio jana (leo) wakazi hao walisema licha ya kutopewa taarifa ya kusudio la ubomoaji huo, waliwashtumu mgambo na polisi kuwapiga raia hao.

Mzee Mohamed Hassan Mnokote (80) mkazi wa eneo hilo ambaye ana ulemavu wa macho (kipofu) alisema Novemba, 10 mwaka huu saa 2 asubuhi siku ya Jumamosi walifika watu waliojitambulisha askari mgambo na polisi na kuanza kubomoa nyumba yake.

Alisema licha ya mgambo hao kuelezwa kuwa mmiliki wa nyumba hiyo haoni mgambo hao walipuuza maelezo hayo na kuendelea kuibomoa na kusababisha hasara ambayo thamani yake haijajulikana.

“Tangu mwaka 2005 nilijenga hapa, hakuna aliyekuja kuniambia siruhusiwi kujenga, leo wanakuja kunibomolea , wanasema hili eneo la soko” alisema Mnokote

Aliongeza kuwa “wamevunja kitanda, baiskeli, vikombe…wanasema nihame niende wapi ili hali yangu ni kama hii”

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wengine wa eneo hilo, Salum Mussa (27) alisema jumla ya nyumba Nane zilizokuwa zinaishi watu zimebomolewa  na kusababisha uharibifu mkubwa wa vyombo vya ndani.

“Walivunja mlango, kabati, meza, vikombe …mimi nilifika hapa 2005, tulikuta pori… walikuwa wanatuona wakati tunajenga lakini hawakutuambia tusijenge, leo wanakuja kutubomolea…kwanini basi wasitupe taarifa ili tuhamishe vitu vyetu?” alihoji Mussa

Amina Yusufu (22) mke wa Mussa anasema alipigwa ana askari bila sababu yeyote, kitendo ambacho alikilalamikia kuwa ni ukatili usio na msingi.

“Nilikuwa nimekaa upenuni, walipofika wakanishika na kunipiga huku wengine wakivunja nyumba…nikiwauliza nimekosa nini wanazidi kunipiga…nchi hii sio yetu, ina wenyewe” alisema Amina

Diwani wa Kata ya Ufukweni, Mohamedi Nchanyambi alikataa kuzungumzia suala hilo kwa maelezo lipo ngazi ya manispaa na kwamba wasemaji wake ni Meya au Mkurugenzi.

“Nenda kwa mkurugenzi, au muone Meya kwa hapa lilipofikia siwezi kulisemea…tusije kupishana taarifa” alisema Mchanyambi

Jamad Omar ni Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, alikiri manispaa yake kuendesha bomoa bomoa katika eneo hilo na kufafanua kuwa eneo hilo ni la wazi kwa ajili ya matumizi ya soko.

“Hata mimi nilihizunika niliposikia yule kipofu amebomolewa nyumba yake…tulikwenda pale mwaka jana tukawaambia wahame kwa sababu lile eneo la soko…hadi leo hawajahama ndiyo maana wamebomolewa” alisema Omar

Mwisho

Advertisements