MIAKA 7 YA UCHIMBAJI GESI HATUJAFAIDIKA NA RASILIMALI YETU

This slideshow requires JavaScript.

“Tangu kuanza kwa utafiti na baadae kuchimbwa kwa gesi, sisi wakazi wa eneo la Msimbati , eneo ambalo gesi inachimbwa hatuwezi kukuonesha matunda ya gesi bali athari zake, hizo tunaweza kukuonesha” ndivyo anavyoanza kusema Mussa Iwenini (30) mkazi wa Msimbati halmashauri ya Mtwara, mkoani hapa.

Ni umbali wa kilomita 30 kusini mashariki mwa mji wa Mtwara hadi kufika kijiji cha Msimbati kinachounganishwa na makao makuu ya mkoa kwa barabara ya vumbi inayopitika vizuri wakati wa kiangazi na kugeuka kero kwa watumiaji wakati wa masika.

Ilinichukua mda wa saa moja kwa usafiri wa Pikipiki kufika katika kijiji hicho kwa wastani wa spidi ya kilomita 30 kwa saa, nilipokewa na mandhali inayoshabihi wakazi wake kuishi kwenye lindi la umasikini licha ya kukalia utajiri mkubwa.

Nyumba nyingi zimeezekwa kwa nyasi, na zile za bati zinaonesha zilijengwa miaka mingi iliyopita na hivyo kugeuka magofu kwa sasa, niliendesha pikipiki hadi chini ya mti wa Mwarobaini uliokuwa na vijana wengi, huku fundi baiskeli mmoja karibu yao akijaribu kuziba tairi pancha.

Pembeni kuna gogo la mnazi likiwa limekaliwa na kijana mmoja wa makamo, nilijisogeza karibu yake, baada ya salamu, alijitambulisha kuwa yeye ni Iwenini mkazi wa kijiji hicho, nilipomuliza anaizungumiaje gesi.

Kijana huyo aendelea kusema “Hakuna mrabaha wala mwekezaji aliyesaidia shughuli za maendeleo ya yetu…tunaona magari yakienda kwenye visima vya gesi na kurudi, labda tuseme hiyo ndiyo faida yenyewe”

Anaeleza kuwa tangu kuanza kuchimbwa kwa gesi mwaka 2005 walipata msaada mmoja tu wa kujengewa chumba kimoja cha darasa na nyumba moja ya mwalimu katika shule ya sekondari Msimbati na kampuni ya Artumas na kwamba hakuna msaada mwingine uliotolewa kwao.

“Sisi tunashangaa tunapoambia gesi ni neema…kijiji chetu hakina umeme, nguzo na waya zimefika kijiji lakini jiulize ni wananchi wangapi wamevutia, watu hawana uwezo wa kulipia gharama…umeme kwetu sio faida, kama yupo anayesema ni faida atueleze na vile vijiji vilivyopata umeme wakati gesi haichimbwi kwao watasema nini?” anahoji Iwenini

Mkazi mwingine Mohamedi Yusufu (25) anasema kuchimbwa kwa gesi katika eneo lao hakujaleta faida yeyote mbali ya kuogelea katika vumbi kutokana na magari makubwa yanayopita kupeleka ama kuchukua vifaa katika visima vya gesi.

“Mabadiliko tunayoyaona ni kwamba, kwa sasa magari makubwa yanapita na kututimulia vumbi, kabla ya gesi kugundulika ilikuwa hatuyaoni …barabara hii ikinyesha mvua kidogo haipitiki, ukiona inachongwa basi ujue aidha kuna vifaa wanataka kupitisha au kiongozi mkubwa wa serikali anakuja” anadai Yusufu

Anasisitiza kuwa “Siku zote sisi tumekuwa wa kudanganywa, juzi Waziri wa Nishati na Madini (Prof. Sospeter Muhongo) alitangaza ofa ya wakazi wa kata ya Madimba kuunganishiwa umeme bure, tumefualia Tanesco wanasema yale ni maneno ya kisiasa, tunalipia 62,000, wanasema VAT”

Ali Luponda (40) ni mkazi kijiji cha Madimba anasema gesi haijawanufaisha kwa lolote kutokana na sekta hiyo kutochangia maendeleo yao

“Juzi walikuja kuzindua kiwanda cha usafishaji wa gesi pale, kitongoji cha Mchepa ishara kwamba safari ya gesi kwenda Dar es Salaam imeiva, kamaimeshindwa kutunufaisha ikiwa hapa itaweza ikiwa mbali?” alihoji Luponda

Madai ya wananchi hao ya kutonufaishwa na gesi yanaungwa mkono na mwenyekiti wa kijiji cha Msimbati, Salum Athuman Tostao (50) ambaye anasema kijiji chake hakijawahi kupokea ruzuku yeyote ikiwa ni mchango wa sekta ya gesi katika maendeleo ya kijiji hicho.

“Mimi ndiye mwenyekiti wa kijiji, nakuhakikishia kuwa kijiji changu hakijawahi kupata fedha ziwe za ruzuku au mrabaha zinazotokana na gesi hii inayoondoka” anasema mwenyekiti huyo na kuongeza

“Kijiji hiki kina wakazi 5967 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002, kati ya hao 82 ndiyo waliovutia umeme, watu hawamudu gharama za kuvutia umeme licha ya kuwa zimepungua na kufikia 92,000 kwa mita ya luku…waziri alito ofa tulipofuatilia wanasema hakuna waraka unaosema hivyo” anasema Tostao

Naye diwani wa kata ya Madimba, Alawi Sadala anasema bado wananchi wa kata yake hawajaona faida ya gesi kuchimbwa katika eneo lao zaidi ya adha ya kuharibiwa barabara zao na magari makubwa yanayopitisha vifaa vya uchimbaji wa gesi.

“Tulikubali kutoa maeneo yetu kwa maslahi yetu na taifa, lakini barabara ikinyesha mvua haipitiki, faida haipo hakuna hata kijiji kimoja kati ya saba kinachoweza kuonesha faida ya gesi zaidi ya kuambulia kuumwa mafua kutokana na vumbi la magari” anasema Sadala

Anasisitiza “Ninachoweza kusema, miaka Saba ya uchimbaji wa gesi tangu mwaka 2005 hatujanufaika na rasilimali yetu, zaidi tumepoteza rasilimali zetu, ardhi, mashamba”

Vijiji ambavyo vinachimbwa gesi kutofaidika na rasilimali hiyo imebainishwa pia katika taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ya mwaka 2010/11 kwa halmshauri ya wilaya ya Mtwara.

Taarifa hiyo ambayo iliwasilishwa katika kikao cha baraza la madiwani wa hamshauri hiyo Julai,11 mwaka huu na Mkaguzi Mkazi mkoani Mtwara, Hassan Kaku inasema wanavijiji wanaozunguka maeneo ambayo gesi hiyo inachimbwa hawajanufaika na rasiliamali hiyo licha ya kuanza kuwanufaisha watu wengine kwa kuzalisha umeme.

“Bado vijiji vinavyozunguka eneo ambalo gesi asilia inachimbwa havijanufaika na rasilimali yao…vijiji hivyo havina umeme, licha ya kwamba gesi inayozalishwa hutumika kuzalisha umeme unaotumiwa na watu wengine…hili ni eneo linalohitaji kufanyiwa marekebisho” ilibainisha sehemu ya taarifa hiyo

“Ushauri wetu kwa halmashauri ya wilaya ni kupitia upya mkataba huo ili kuhakikisha vijiji hivyo vinanufaika na rasilimali yao” ilishauri taarifa hiyo.

Kaku anaeleza kuwa licha ya halmashauri hiyo kupata hati inayorizisha yenye mambo ya kutilia mkazo, bado taarifa hiyo imedokeza kuwa ni muhimu kwa halmashauri hiyo kuhakikisha vijiji hivyo vinanufaika na gesi ili thamani ya rasilimali hiyo iweze kuonekana kwa jamii hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo baadhi ya madiwani walionesha kuguswa na kuchangia kwa kuitaka halmshauri kutoingia mikataba kama hivyo kabla ya kuthibitishwa na kikao cha baraza la madiwani.

“Hatuwatendei haki, wakati sisi tunafurahia umeme wa uhakika, wanakijiji ambao wameitunza rasilimali hii kwa miaka mingi wapo gizani …waliambiwa wafanye ‘wiring’ (kutandaza nyaya kwenye nyumba) wamefanya hivyo, waliambiwa walipie gharama kidogo wamefanya hivyo lakini bado hawajapata umeme” alisema Hassan Mauji diwani wa kata ya Nanyamba

Aliongeza kuwa “Nyumba za jamii, shule, misikiti waliambiwa wafanye wiring halafu wataunganishiwa umeme bure, wamefanya hivyo lakini hadi leo hawajanganishiwa umeme”

Kuu wa Wilaya ya Mtwara Wilman Ndile akizungumza katika kikao hicho , anasema ameguswa na taarifa hiyo na kuahidi kuwasiliana na shirika la umeme (Tanesco) kubaini tatizo la kutounganishiwa umeme kwa wakazi wa vijiji hivyo.

“Ni suala nyeti, nitaongea na Tanesco kuona tatizo nini…mkaguzi ametukumbusha kuwa wananchi wana haki ya kunufaika na rasilimali zao na ni jukumu letu kuhakikisha hilo” anafafanua Ndile

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Saidi Ndazigula anasema ni wakati muafaka kwa wana-Mtwara kuhakikisha wanafaidika na rasilimali zao kabla ya maeneo mengine.

“Ukimuona mtu ana wasiwasi basi ujue huyo mtu ana akili, anafahamu nini kinaweza kutokea…tupo kwenye wasiwasi…tunahisi wapo watakaochukua rasilimali yetu na sisi kutuacha patupu…ni muhimu kulijadili hili katika vikao vyetu vijavyo.

Mkurugezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Idd Mshili anasema ni kweli wanavijiji hao hawajanufaika na gesi inayochimbwa katika ardhi yao.

“Sisi halmashauri hatujawahi kupata Mrabaha kutokana na gesi inayochimbwa Msimbati…tumefuatilia wizarani mara ya mwisho hivi majuzi wametuambia labda hadi pale gesi itakapoanza kusafirisha kwenda Dare s Salaam…lakini wenzetu Kilwa wanapata Mrabaha” anabainisha Mshili

Anafafanua “Wananchi hawajakuongopea, kwa upande  wa ushuru hawajanufaika kwa lolote… ni umeme wanaolipia kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kisha wanaunganishiwa bure…gesi haijatunufaisha kwa kweli”

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani na mwandishi wa makala haya kupata ufafanuzi wa madai ya wananchi hao alionekana kulikwepa kuzungumzia jambo hilo.

Waziri Muhongo aliomba apigiwe baadae, alipopigiwa baadae hakupokea simu bali alijibu kwa ujumbe wa maneno uliosomeka “I’m in meeting” (nipo kwenye mkutano)

Mwandishi alimuomba ahadi ya muda wa kuongea nae kwa ujumbe wa maneno katika simu ya kiganjani ambapo alijibiwa kwa ujumbe uliosomeka “After 2:00 hrs” (baada ya saa mbili usiku), alipopigiwa simu mda huo, anasema “nipigie kesho kuanzia saa tano, nitakuwa ofisini sina ratiba ya vikao”

Siku iliyofuata Oktoba 11, mwaka huu alipopigiwa saa tano kama alivyoahidi, simu yake iliita bila kupokelewa na mda mfupi baadae alituma ujumbe wa maneno uliosomeka “I’m in meeting” (nipo kwenye mkutano)

Mwisho

Advertisements