TAMASHA LA MaKuYa LAFUNIKA MTWARA

This slideshow requires JavaScript.

TAMASHA la ngoma za asili la makabila ya Wamakonde, Wamakuwa na Wayao linalojulikana kama MaKuYa ‘limefunika’ kwa kukonga nyoyo za wakazi wa Mtwara.

Tamasha hilo limefanyika mwishoni mwawiki (Novemba, 17, 18 mwaka huu) katika uwanja wa Nangwanda Sijaona na kuwaacha mamia ya watu waliohudhuria wakijawa na furaha na simulizi tele za kulisifiaika.

Likiwa limeshirikisha jumla ya vikundi 20 vya ngoma za asili kutoka wilaya zote tano za mkoa wa Mtwara zikiwa na mchanganyiko wa makabila hayo, lilisindikizwa na michezo ya asili na maonesho ya bidhaa za asili.

Mkurugenzi Mwenza wa Kituo cha Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa za Afrika (Adea) Philipo Lulale amesema katika tamasha hilo lililofunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseoh Simbakalia  kuwa tamasha hilo la nne kuandaliwa na kituo hicho tangu mwaka 2008, ambapo kwa mwaka huu litashirikisha jumla ya wasanii 400 na kwamba maandalizi yake kwa kiasi kikubwa yamekamilika.

“MaKuYa itawaweka pamoja wasanii hao wapigaji na wachezaji wangoma za asili kutoka katika wilaya za mkoa wa Mtwara kwa upande mmoja na maonesho ya bidhaa za asili na michezo ya jadi kwa upande mwingine…maandalizi yamekamilika” alisema Lulale

Alifafanua kuwa “Kwa lengo la kuhifadhi utamaduni huo kabla hatujachelewa , tamasha la MaKuYa litakutanisha tena wasanii wacheza ngoma zaidi ya 400 katika vikundi 20 kutoka makabila makubwa matatu ya mkoa wa Mtwara”

Alisema madhumuni ya tamasha hilo ni kuwa jukwaa la kila mwaka kwa ajili ya wasanii wa mkoa wa Mtwara kupiga na kucheza ngoma za asili, kudhibiti na kuhimiza utamaduni wa asili na kukuza mapenzi ya utamaduni wa mkoa wa Mtwara.

Mkurugenzi mwenza huyo alisema tamasha hilo lililofadhiliwa na ubalozi wa Finland, British Gas (T) Ltd, Wentworth Foundation na ODJILL DRILLING litatoa fursa ya wazawa na wageni zaidi ya 1300 hadi 1500 kutembelea viwanja vya Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ambako litafanyika.

Mwisho