LINDI WAMSHANGAA KIKWETE, WASUSA MKUTANO

This slideshow requires JavaScript.

MKUTANO wa kukusanya maoni ya sera ya gesi asilia mkoani Lindi umeingia dosari baada wananchi kuamua kuondoka mkutanoni hapo kwa madai hawakubaliani na uwamuzi wa serikali kupeleka gesi Bagamoyo.

Tukio hilo la aina yake limetokea jana katika ukumbi wa Lindi Beach Resort ambapo wananchi hao waliamua kuvunja mkutano huo na kisha kuondoka na kuwaacha wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini wakishikwa na butwaa.

Mkutano huo ulifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila ambaye aliwataka wananchi kuwa huru kutoa maoni yao kwa kuzingatia maslahi yao na Taifa kwa ujumla.

Ilikuwa mithili ya mchezo wa kuigiza pale Mzee Omar Chitanda aliposimama na kutoa maoni yake yaliyopinga gesi kwenda Dare s Salaam na kisha kumalizia kwa kufunga mkutano.

“Tunawataka hao waliowatuma waje hapa, mimi naomba niwe mtu wa mwisho kuzungumza, mkutano huu uishie hapa…tumejifunza kwa vitendo yaliyotokea Songosongo kule Kilwa, gesi imepelekwa Dar es Salaam, wananchi masikini…mkutano umefungwa” alisema Chitanda na wanachi waliinuka na kuondoka mkutanoni

Dalili za kuvunjika kwa mkutano huo zilijionesha tangu wachangiaji wa mwanzo, walioshawishi wengine wakubaliane na hoja ya kuughairisha mkutano huo hadi siku nyingine ili waweze pia kuyapitia kwa utuvu makabrasha ya rasmu ya sera hiyo ya gesi asilia ambayo waligaiwa mkutanoni hapo.

Wachangiaji hao waliweka wazi msimamo wao wa kupinga gesi kusafirishwa kwenda Bagamoyo, huku wakimshangaa  Rais Jakaya Kikwete kuzindua ujenzi huo jijini Dar  es Salaam wakidai kuwa kitendo hicho kinaonesha kutothaminiwa kwa watu wa kusini.

“Hivi inawezekana Ikulu ijengwe Dar es Salaam halafu jiwe la msingi liwekwe Lindi? Tunamshangaa rais katika hili,  hii ni dharau kwetu” alisema Hassan Tendo huku akipigiwa makofi na wananchi.

Aliongeza kuwa “Hivi Lindi tumeikosea nini Tanzania, sisi tunasema gesi haindoki hapa labda mukiweza mutuibe kwa ‘usanii’ wenu…tuleteeni rasmu hii baada ya kujua maslahi yetu yapoje”

Mkazi mwingine Mohamed Kimwaga aliitaka serikali kusitisha mpango wake wa kupeleka gesi Bagamoyo kabla ya wananchi wa maeneo inakotoka kunufaika nayo kwa maelezo kuwa utasababisha mgogoro.

“Baada ya uhuru kwa miaka kumi Mikoa ya Lindi na Mtwara ilizuiliwa kuendelezwa kwa kugeuzwa eneo la mapambano ya kukomboa nchi jirani…tumejaribu kuomba fidia hakuna aliyetusikiliza, leo Mungu ameamua kutufidia gesi, munataka kutunyang’anya, haiwezekani”

Aliongeza kuwa “Tunaomba haya yafike kwa aliyewatuma…kama viwanda vijengwe hapa kwetu, huko Dar es Salaam ziende nyaya za umeme tu …naomba rasmu hii ighairishwe ije mara ya pili baada ya kuisoma na kuielewa ndipo muje kutuomba maoni yetu”

Naye Chacha Salum aliunga mkono hoja za wenzake za kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam akisema kitendo hicho kunahatarisha uchumi wa nchi na kusababisha watu kukimbilia mijini.

“Leo hii asilimia 85 ya pato la taifa linatoka Dar es Salaam, bado unataka viwanda vikajengwe huko, hivi hatujiulizi iwapo yatatokea maafa Dar es Salaam uchumi wetu utasimamia wapi? Kwa kuhamishia kila kitu Dar es Salaam unasababisha watu nao wakimbilie huko kwa kufuata fursa za kiuchumi” alisema Salum

Alifafanua “Siungi mkono gesi kwenda Dar es Salaam, viwanda vijengwe huku, ili watu watoke Dar es Salaam kuja kuishi huku Lindi ili uchumi wa huku nao ukuwe….watu waLindi maskini”

Awali akiwasilisha mada Kaimu Kamishina wa Gesi Nchini, Mhandisi Robert Kayoza aliwaambia wananchi hao waliojitokeza kwa wingi kuwa hatua hiyo inalenga kupata maoni ya wananchi juu ya namna sera ya gesi asili iwe kwa kulinda maslahi ya Taifa.

Mhandisi Kayoza aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendelo ya Petroli nchini (TPDC) Yona Kilane ambaye alionesha kukerwa na kitendo cha wananchi kususia mkutano huo.

“Sisi tumekuja na mapendekezo ya sera ya gesi asilia na tunachukua maoni yetu, hapa hatuna sera sasa inashangaza kuona wananchi wameshindwa kutuelewa” alisema Kilane.

Akizungumzia wananchi kuondoka mkutanoni hapo, Mhandisi Kayoza alisema yawezekana wananchi hao walishindwa kumuelewa wakati alipokuwa akiwasilisha mada yake hapa pale aliposema eneola viwanda linalohitajika ukubwa wake ni zaidi ya mji wa Lindi.

“Sijasema Lindi hakuna eneo la kuweka viwanda, hapa wamenielewa vibaya, nimesema eneo la viwanda linalohitajika ni kubwa kuliko mji wa Lindi…nawapongeza kwa kujitokeza kwa wingi na wale waliochangia walitupanua mawazo” alisema Kayoza.

Mwisho

 

Advertisements