MAWAZIRI WAZOMEWA MBELE YA KINANA MTWARA

This slideshow requires JavaScript.

MAMBO yalikuwa magumu kwa mawaziri watatu wa Rais Jakaya Kikwete baada ya kukumbana na zomeazomea walipopanda jukwani kujibu kero mbalimbali za wananchi katika mkutano wa kwanza wa viongozi wapya wa CCM taifa ulioongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdullhaman Kinana ulioanyika uwanja wa soko kuu mjini Mtwara Novemba 21 mwaka huu.

Mawaziri waliozomewa jukwaani mbele ya Kinana ni Hawa Ghasia wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Naibu Waziri wake Agrey Mwanri na Christopher Chiza wa Kilimo, Chakula na Ushirika

Chiza ndiye aliyekuwa wa kwanza kukumbana na hali hiyo ngumu ya mkutano lakini mambo yalikuwa magumu zaidi kwa Ghasia ambaye tangu alipopanda jukwaani hadi anateremka sauti za kumzomea zilikuwa zinapamba moto .

Ghasia alikuwa anajibia hoja iliyouliza na Rukia Ismail Athumani aliyewashutumu yeye mbunge wa Mtwara vijijini na Asnein Murji mbunge wa Mtwara Mjini kuwasaliti wananchi wa Mtwara kwa kuruhusu gesi kupelekwa Dar es Salaam wakati wananchi wenyewe hawajafaidika nayo.

“Ghasia na Murji mumeutekeleza umma huu kwa kukubali kuipeleka gesi Dar es Saalam…sisi hatukichukii chama lakini hatutaki gesi kwenda Dar es Salaam” alisema Athumani huku akishangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo.

Kabla ya dada huyo kuteka hisia za wananchi kwa kuwasilisha kero yao hiyo, Kinana alimruhusu mwananchi mwingine, Issa Kambona ambaye alimweleza wazi kuwa hakubaliani na sula la gesi asili ya Mtwara kupelekwa Dar es Salaam.

Kinana alisema amesikia hoja hizo za wananchi na kwamba atamtuma waziri wa Nishati na Madini (prof. Sospeter Muhongo)  kuzungumza na wananchi wa Mtwara kuhusu gesi, hata hivyo Waziri Ghasia alipanda jukwani kujibia shtuma zilizoelekezwa kwake.

“Si kweli kwamba hatutetei maslahi yenu…gesi iliyopo ni nyingi hatuwezi kutumia sisi na kuimaliza, kuna futi za ujazo trilioni 20 elfu, tunaweza kuitumia kwa zaidi ya miaka 90….pia wizara ya nishati imetoa ofa ya kuwalipia chuo vijana 150 kila mwaka” alisema Ghasia huku akizomewa hali iliyompa wakati mgumu.

“Uongo, uongo…..hatutaki, hatutaki, huyoo, huyooo” sauti za wananchi zilisikika zikimpinga na kumzomea waziri huyo, hali iliyomlazimu Nape Nnauye katibu wa Siasa, Itikadi na Uwenezi wa chama hicho taifa kuingilia kati kujaribu kuweka mambo sawa.

“Kelele unazozisikia hiyo dada, zinaashiria kuna jambo, nafasi hizo 150 hawazipati, kama zinatolewa basi kwa upendeleo” alisema Nape huku akishangiliwa na wananchi kwa kusema “ndiyooo”

Baada ya hali kutulia Ghasia alijaribu kuendelea kutoa ufafanuzi lakini sauti za kumzomea zilimzidi na ndipo alipofikia hatua ya kusema “kila mtu hapa amelelewa katika mazingira tofauti, hilo halinihusu…watu wangu wa Mtwara vijijini wamenielewa” alisema Ghasia na kuteremka jukwanii hali iliyozidisha kelele za kumzomea.

Nape alisawazisha mambo kwa kusema, hoja ya wananchi hao imechukuliwa na itawasilishwa kwa serikali ili kuona namna ambavyo inaweza kukaa na wananchi hao na kuweka maslahi yao mbele.

Panzia la zomea zomea lilifunguliwa na Chiza alipopanda jukwaani kujibia hoja ya kuyumba kwa soko la zao la korosho, ambapo wananchi walimpinga baadhi ya kauli alizozitoa.

“Tatizo la korosho ni baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika na wengine ni watendaji wa serikali …nipo hapa na wala siondoki, nitalishughulikia hili ili korosho zinunuliwe” alisema Chiza huku sauti za wananchi zikimpinga kwa kusema “uongooo”

Hata hivyo Chiza aliweza kukabiliana na hali ya zomeazomea jukwaani baada ya watuliza wananchi kwa kusisitiza kuwa ataendelea kuwapo Mtwara, kushughulikia tatizo hilo ili ununuzi uendelee.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwanri alipata wakati mgumu mara alipopanda jukwaani na kuanza kuzungumzia namna ya kumaliza kero ndogondogo zinazoletwa na mamlaka zake, wananchi walikuwa wanazoea “huyoo…hatutaki” lakini baada ya kuanza kuongea alionekanakuiteka hadhira na mambo yakawa shwari. “

“Tumesema wauza vitumbua, wasibughuziwe … mkurugenzi njoo jukwani, nakuagiza kuanzia leo marufuku wanafunzi kurudishwa shuleni kwa sababu ya michango” alisema Mwanri huku akishangiliwa

Awali Kinana alisema mkutano huo unalenga kuzipatia ufumbi kero za wananchi ambazo zinawezakuwa kikwazo kwa chama hicho kuingia madarakani mwaka 2015.

Katibu mkuu huyo wa chama tawala alisema umefika wakati wa chama kusimamia utendaji wa serikali kutatua kero za wananchi  wa mkoa wa Mtwara zikiwapamoja na kuyumba kwa soko la korosho na gesi.

“Najua hapa kuna kero kubwa mbili, korosho na gesi, nimekuja na Mawaziri hapa watatoa majibu leo” alisema Kinana huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu ulioudhuria mkutano huo.

Mwisho