AJALI MTWARA WATATU WAFA, TANO HOI

3MAFUNDI ujenzi watatu wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa vibaya baada ya ukuta wa ghala walilokuwa wakipandisha kenchi kuporomoka na kuwafukia.

Ajali hiyo imetokea jana saa 10 jioni katika eneo la bandari ya Mtwara ambako ghala hilo lilikuwa linajengwa ikiwa ni sehemu ya upanuzi wa Bandari hiyo.

Mashuhuda wa tukio hilo wameliambia KUSINI  hili kuwa kabla ya ukuta huo  kuporomoka mafundi zaidi ya 20 walikuwa juu ya boma hilo wakipandisha kenchi, ghafla ukuta wa marefu wa upande wa magharibi ulijipasua na kuangua.

“Wakati ukuta unaanguka mafundi walikuwa juu ya kechi, wakaanguka nazo, wengine wamekufa hapa hapa baada ya kubanwa na kenchi na ukuta” alisema mmoja wa shuhuda bila ya kujitambulisha jina.

Alifafanua kuwa “mafundi walioanguka ni wale waliokuwa upande wa ambako ukuta umeangu…kinachoonekana ni kwamba ukuta ulizidiwa uzito, ukajiacha….jengo hili linajengwa na kampuni ya shibat”

Katika tukio hilo watu wawili walifariki papo hapo na mwingine alifariki usiku huku watano wakiwa majeruhi na wanaendela na matibabu hospitali ya mkoa wa Mtwara, Ligula.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Mohamedi Kodi bila ya kuwataja majina amethibitisha kutokea kwa vifo vitatu na amepokea majeruhi watatno ambao wanaendelea na matatibabu.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara Wilman Ndile (pichani) alisema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa ajali hiyo imesababishwa na ujenzi usiozingatia viwango.

“Dalili zinaonesha lile jengo linajengwa chini ya kiwango ndiyo maana limeporomoka…hapa pamoja na wahandisi wa mradi huo pia manispaa ilipaswa kufuatilia mara kwa mara namna ambavyo ujenzi unaendelea baada ya kutoa kibali cha ujenzi” alisema Ndile

Alifafanua kuwa “Taratibu zingine za kisheria zitafuatwa…hapa kuna uzembe wa ufuatiliaji kwa mamlaka za usimamizi, haiwezekani jengo hadi linafikia karibu kupauliwa bado wataalam hawajabaini kuwa lipo chini ya kiwango”

Mwisho