KKKT KUSINI MASHARIKI LAPATA ASKOFU

Askofu Mteule, Mchungaji Lucas Mbedule

Askofu Mteule, Mchungaji Lucas Mbedule

KANISA la KKKT Dayosisi mpya ya Kusini Mshariki imepata Askofu mteule, Mchungaji Lucas Mbedule katika uchaguzi wake uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Masasi.

Katika uchaguzi huo uliovuta hisia za wengi, Askofu wa Dayosisi mama ya Kusini, Isaya Mengere alimtangaza Mchungaji Mbedule kuwa askofu mteule baada ya kuwabwaga wenzake wawili kwa kupata kura 34.

Katika uchanguzi huo Mchungaji Mbedule alishindana na Mchungaji Zakaria Lyakungi aliyepata kura 13 na  Mchungaji Wiseman Simwinga aliambulia kura 4 huku moja ikiripotiwa kuharibika.

Uchaguzi huo ilifikia hatua ngumu kumpata msaidizi wa askofu huyo, ambapo wajumbe walilazimika kupiga kura mara tatu ili kumpata mshindi baada ya awamu ya kwanza na pili wagombea kushindwa kufikia theluthi mbili ya kura zilizopigwa .

Hata hiyo Askofu Mengere alimtangaza Mchungaji Yeriko Ngwema wa kanisa la Masasi kuwa mshindi baada ya kupata kura 35 dhidi ya Mchungaji Zakaria Lyakungi aliyepata kura 18, ambapo Mchungaji Wiseman Simwinga alitolewa katika hatua ya mwanzo ya upigaji kura.

Askofu mteule Mbedule na msaidizi wake Ngwema wanatarajia kusimikwa rasmi Juni, 16 mwakani siku ambayo Dayosisi hiyo mpya ya kusini mashariki itazinduliwa.

Awali askofu wa kanisa la Angalikana Dayosisi ya Newala  Oscar Mnung’a aliwataka wajumbe kumchagua kiongozi anayesukumwa na dhamira ya kweli ya kulitumikia kanisa na kuwaongoza waumini wake katika mafanikio kwa mujibu wa imani.

Askofu Mnung’a ambaye alionesha kuteka hisia za wajumbe alisema kiongozi bora ni yule anayeweza kuchambua baya na nzuri na kusimamia haki mbele ya waumini wake kwa mujibu wa maamrisho ya Mungu.

“Chagueni kiongozi mwenye maono, mwenye kusimamia haki, mwenye uwezo wa kuchambua mambo na kuwaongoza kwa mujibu wa imani yetu” alisema Askofu Mnung’a

Dayosisi ya kusini mashariki ni mongoni mwa dayosisi mbili andaliwa zitakazozinduliwa Juni mwakani nyingine ni dayosisi ya Ziwa Victoria Shinyanga ambazo zitafanya kanisa hilo kuwa na dayosisi 22 nchini.

Mwisho

 

Advertisements