‘KWANINI HAWATAKI GESI ITOKE MTWARA’

1DESEMBA 13, 2012 Mtandao wenu wa KUSINI ulichapisha bahari zinazohusu vyama vya siasa vya upinzani vya wilaya ya Mtwara kuungana kupinga gesi wenda Dar es Salaam kwa kaulimbiu “Gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu”.

Kutokana na maoni na michango ya wasomaji wangu, KUSINI imeona  bora ichapishe hoja zinazojengwa na Wana Kusini katika kutia nguvu hoja yao ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam kwa njia ya bomba.

Kimsingi wakazi wa kusini hawapingi gesi kwenda nje ya Mtwara na Lindi, wanasema gesi inaweza kupelekwa kokote Duniani ili mradi iwe iliyosafishwa tayari kutoka Mtwara na sio mbichi (raw).

Wanasema ni vema kiwanda cha kusafisha gesi kikajengwa Mtwara ili wakazi wa Mtwara wapate ajira na hivyo kupunguza hali duni ya maisha inayowakabili kwa sasa, wanahoji ni mwekezaji gani aliye tayari kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 500 kwenda Mtwara kuwekeza wakati gesi ambayo ingekuwa kigezo cha yeye kwenda huko inapatikana Dar es Salaam?

Wakazi wa mikoa ya kusini wameona kwa macho yao kule Songosongo Kilwa mkoani Lindi, ambako gesi imesafirishwa kwenda Dar es Salaam, hakuna kiwada wala mwekezaji aliyewekeza eneo lile, zaidi ya ufukara kuzidi kuwaandama wakazi wale.

Waungwana husema, kosa si kutenda kosa bali kurudia kosa.

Hoja nyingine ni ile ya mitambo ya kufua umeme  kujengwa Kinyerezi, wanahoji kwanini Dar es Salaam na sio Mtwara, ipi ni gharama kubwa kujenga bomba au kutandaza nyaya za umeme? Jibu hapo ni kutandaza nyaya za umeme ni nafuu, kwanini basi mtambo huo usijengwe Mtwara halafu umeme ukapelekwa hata Rwanda?

Hoja ya KUSINI ni kwamba kwanini tutumie akili nyingi kuongeza uhamiaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini badala ya kutatua tatizo?

Leo hivi mitambo, viwanda vingejengwa Mtwara  watu wangetoka Dar es Salaam na kwingineko kuja kufanya kazi Mtwara, watu wangehama mjini na kukimbilia kijijini, lakini hebu jiulize leo jiji la Dar es Salaam ndilo tegemeo la pato la Taifa kwa asilimia zaidi ya 80, iwapo jiji hili litapatwa na janga lolote (siombei) hivi Tanzania itakuwa katika hali gani?

Hapa nadhani ni ufinyu wa kufikiri, ndio maana hata kuhamia Dodoma hawataki wamekaririshwa kuwa ‘Dar ndiyo mpango mzima’ na kwamba kitu kingine kizuri hakipaswi kuonekana zaidi ya Dar na maeneo mengine na sio kusini.

Wananchi wa mikoa hiyo pia wanaumizwa na historia ambayo mikoa ya kusini mara baada ya uhuru ilitangazwa kuwa ni maeneo ya kupigania vita ya ukombozi kusini mwa Afrika, kwa msingi huo hakuna maendeleo yeyeto kwa miaka 10, ndiyo maana barabara za kuingia Lindi na Mtwara hazikutengenezwa.

Ndiyo maana Reli ya Kutoka Nachingwea kwenda bandari ya Mtwara iling’olewa, ndiyo maana mikoa ya Lindi na Mtwara haikuunganishwa na umeme wa grid ya Taifa.

Watu wa kusini wanahisi kuonewa kwani hata walipotaka kulima zao la pamba ambalo wataalam wa kilimo wanathibitisha kuwa linastawi vizuri katika mikoa hiyo serikali ilipiga marufuku kwa madai wapo wadudu nchi ya Msumbiji ambao wanaweza kuingia Tanzania nakuathiri pamba ya kule mikoa za kanda ya ziwa.

Wazee wa mikoa hii wanasema kulikuwapo na makubaliano yasiyo rasmi kuwa baada ya vita vya ukombozi kwisha mikoa ya kusini ingefidia kwa kuharakishiwa maendeleo jambo ambalo halijafanyika hadi leo.

Mungu kawaona kawapa gesi, nayo inaondolewa kupelekwa Dar ndipo wanapohoji Kusini imeikosea nini Tanzania? Kwani kuna ubaya gani mitambo na gesi ikibaki Mtwara, sio Tanzania au wakazi wake hawasitahili?

KUSINI inashauri Serikali kutafakari upya jambo hili vinginevyo linaweza kutupeleka pabaya, hebu tujifunze kwa wenzetu Sudani Kusini.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

Advertisements