MTWARA MSIUZE ARDHI, INGIENI UBIA

Goodluck Ole-Mideye, kulia mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Ponsiano Nyami

Goodluck Ole-Mideye, kulia mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Ponsiano Nyami

WAKAZI wa mkoa wa Mtwara wametaadharishwa kuacha tabia ya kuuza ardhi kwa wawekezaji na badala yake waingie ubia ili waweze kufaidika na rasilimali hiyo.

Taadhari hiyo imetolewa jana katika kijiji cha Nahyanga ‘A’ wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Mideye alipoongea na wananchi wa kijiji hicho katika hafla ya kukabidhi hati za kimila za kumiliki ardhi.

Alisema kutokana na ugunduzi wa gesi watu wengi wameonesha nia ya kuwekeza katika mkoa wa Mtwara, hivyo ni vema uwekezaji huo usiwakimbize wenyeji bali uwanufaishe.

“Msiuze ardhi kwa wawekezaji…hii gesi sio sababu ya wewe kuikimbia Mtwara, ukiuza ardhi ina maana utalazimika kukimbia eneo hilo…ingieni ubia nao, ili muweze kufaidia na rasilimali yenu” alisema Ole-Mideye

Aliongeza kuwa “Si kwa wananchi tu, pia viongozi wa vijiji, acheni kuuza ardhi kwa wanaodai ni wawekezaji…tumebaini kuwa wengi wanakuja kwa mgongo wa uwekezaji lakini wakipata ardhi wanaikodisha kwa wananchi, wengine wanagawa viwanja”

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria namba 5 ya ardhi ya kijiji ya mwaka 1999 kijiji kina haki ya kutoa ardhi isiyozidi hekari 50 kwa mwekezaji, hata hivyo ni vema utoaji huo ukaweka mbele zaidi maslahi ya wananchi.

“Migogoro mingi ya ardhi inayotokea baina ya wanakijiji na mwekezaji inatokana na mwekezaji kuhodhi eneo kwa mda mrefu bila kulifanyia kazi…tunaangalia uwezekano wa kutoa mda wa miaka kumi kwa mwekezaji kuendeleza eneo lake…pia ataweka fedha serikalini kama dhamana ya uwekezaji wake” alisema Naibu Waziri huyo

Aidha aliwataka wananchi waliopata hati miliki hizo za kimila kuzitumia katika kuwakomboa na umasikini kwa kuzitumia kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.

“Hati hii ina maana kwako iwapo utaitumia kupata mikono, kusomesha watoto chuo kikuu na ulinzi wa rasilimali yako…ni vema wananchi mkajitokeza kwa wingi kurasimisha mashamba yenu ili yawe na ulinzi wa kisheria” alisisitiza Ole-Mideye

Awali Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Charles Genge alisema jumla ya hati 88 zimetolewa kwa wanakijiji hao kati ya hizo hati 9 ni za wanawake pekee.

“Kukamilika kwa mchakato huu ni mwanzo wa mchakato mwingine wa urasimishaji wa rasilimali za wananchi hususani ardhi…wananchi wamepokea vizuri kwa kuchangia kaisi cha sh. 4000 kwa kila mmoja” alisema Genge

Alifafanua kuwa”Katika kurahisisha mchakato huu halmashauri imenunua vifaa viwili vya utambuzi wa mipaka (GPRS), na tayari masjala ya ardhi ya wilaya na ya kijiji cha Nahyanga A zimekamilika…lengo hapa ni kuwawezeaha wananchi wetu watumie ardhi katika kujikomboa na umasikini”

Mwisho

Advertisements