MKUU WA MKOA HAJAKOSEA, NI KWELI MTWARA WAPUUZI

Anaba, Mhariri Mtendaji KUSINI

Anaba, Mhariri Mtendaji KUSINI

KWA mara ya kwanza KUSINI inaungana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kuwaita wakazi wa mkoa huo ambao wanapinga gesi asilia kwenda Dar es Salaam kuwa ‘Wapuuzi’

Kimsingi ni kweli wananchi hawa ni wapuuzi kama tafsiri yetu ya Kiswahili ya neno ‘Wapuzi’ itakuwa sahihi, kwa tunavyoelewa,  wapuuzi wametokana na hali yao ya kupuuzia mambo, yaani wanambiwa jambo la msingi halafu wahalitilii maanani.

Si tusi kabisa kama wana Mtwara wanavyodai wametukanwa, hajatukanwa mtu ila wameambiwa ukweli kuwa wao ni wapuuzi, na ni kweli nasadiki kuwa wapuuzi, tena naongeza kuwa ni wapuuzi wakubwa na kutokana na upuuzi wao ndiyo maan mkoa umeendelea kuwa masikini na hali ya maisha yao ni duni.

Ni upuuzi wa wakazi hao ndiyo uliosababisha kung’olewa kwa reli iliyokuwa inatoka Nachingwea mkoani Lindi kwenye mashamba ya karanga hadi bandari ya Mtwara, wananchi hao waliona reli wakati inang’olewa lakini wakapuuzia.

Ni wapuuzi kweli ndiyo maana wakati wenzao wanaunganishwa kwenye gridi ya taifa ya umeme wao walikosa na wakakaa kimya, yanii walipuuzia.

Hakuna jina nzuri kwa wana-Mtwara zaidi ya wapuuzi, walikatazwa kulima pamba ili hali inastawi vizuri wakakaa kimya licha ya kwamba uwamzi huo ulikuwa unawadidimiza kimaendeleo lakini walipuuzia, walikubali eneo lao kugeuzwa kisiwa kwa kukosa barabara ya lami ya kuwaunganisha Jiji la Dar es Salaam tangu uhuru licha kwamba ikikuwa kero kwao lakini wakapuuzia.

Ni wapuuzi haswa pale bandari yao ‘ilipouawa’ wakabaki kimya na maisha yakaendelea kama kawaida, hawa na tabia yao ya upuuzi ndiyo maana walikubali eneo lao kugeuzwa kuwa uwanja wa vita za ukombozi kusini mwa Afrika na hakuna fidia yoyote waliyolipwa kutokana na kucheleweshewa maendeleo kwa miaka kumi, na wapo kimya, hivi kweli hawa sio wapuuzi?

Hatuandiki uchambuzi huu kwa lengo la kuchochea jambo fulani kama wavivu wa kufikiri wanavyoweza kutafsiri, hapa tunajaribu kuwatanua mawazo wana Mtwara wanaodai wametukanwa kwa kuambiwa wapuuzi, kwanza nimebaini hawajui kiswahili na sasa nawatolea mifano hii inayoendana na neno upuuzi labda watanielewa.

Leo gesi inapelekwa Da es Salaam wanataka kujiondoa kwenye upuuzi kwa kuandamana ndiyo maana Simbakalia aliwakumbusha kuwa nyie ni wapuuzi kama yeye alivyopuuza kupokea maandamano ya wapuuzi, hivi tatizo lipo wapi wana Mtwara?

KUSINI inaona Simbakalia hajakosea na hata yeye mwenyewe anajua hivyo ndiyo maana hajaomba radhi, alichofanya ni kuwakumbusha kuwa ninyi ni wapuuzi mliozoea kupuuzia kila jambo kama yeye alivyopuuza maandamano yenu.

Ni rai yetu kuwa hii tabia ya kupuuza mambo ifike mwisho kwani sasa tumeona imemwambukiza hadi mkuu wa mkoa wa Mtwara Simbakalia naye amepuuza maandamano ya wapuuzi hapo nani mpuuzi?

Mwisho

Advertisements