DC. WALIOANDAMANA WASILAUMIWE

DSC08014[1]MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile amesema sio sahihi kuwalaumu wananchi kwa kuandamana kupinga gesi asilia inayovunwa mkoani humo kupelekwa Dar es Salaam wakati hawajaelimishwa namna ambavyo watanufaika na bomba hilo.

Akifungua baraza la majadiliano baina ya uongozi na vyama vya wafanyakazi wa Bandari ya Mtwara mwishoni mwa wiki Ndile alisema licha ya kwamba maandamano hayo yamepokelewa kwa hisia tofauti na Watanzania bado si sahihi kuwabeza.

“Ni kweli hatuwezi kueleweka kama gesi inakwenda Daes Salaam wakati hawajui watanufaikaje, hayo sio maswali madogo, lazima yajibiwe” alisema Ndile

Aliongeza kuwa “Gesi ni fursa nyingine ya uchumi, tayari mwekezaji Dangote ameanza kazi ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha saruji, na hivi karibuni lile eneo la Msijute ambalo serikali imelitwaa kutoka kwa mwekezaji, tutagawa viwanja kwa ajili ya viwanda, tumesema itakuwa ‘industrial area’ (eneo la viwanja)…mimi nadhani si sahihi kuwalaumu wananchi”

Kauli hiyo ya mkuu wa wilaya inapingana na zile zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa juu wa serikali za kuwatupia lawama wananchi wa Mtwara kwa kuandamana, akiwemo Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo aliyelaani maandamano hayo kwa maelezo kuwa ni hatari kwa usalama wan chi.

Kiongozi mwingine ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia aliyewaita wapuuzi waandamanaji hao na badae wahaini.

Kwa upande mwingine kauli ya mkuu huyo wa wilaya inaungana na ile iliyotolewa na Mbunge wa Mtwara Mjini Asnain Murji ambapo alisema wananchi ni haki yao ya msingi kujua namna ambavyo bomba la gesi linalopelekwa Dar es Salaam litawanufaisha.

Aidha Ndile aliutaka uongozi wa bandari hiyo kushirikiana na wafanyakazi ili kutatua changamoto zinazoikabili bandari hiyo ili iweze kuchochjea kwa kasi ukuaji wa uchumi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Bandari hiyo, Modest Kakusa alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa baraza hilo la majadiliano la 28 linalenga kuzungumzia maslahi ya wafanyakzi, mazingira ya kazi na kudumisha amani kazini.

“Tunatarajia baada ya miaka 20 ijayo bandari iweze kupokea shehena ya mzigo tani 25 milioni badala ya sasa ambapo tani 240000 tu ndizo zinazoingia na kutoka Bandarini kwa mwaka” alisema Kakusa
Mwisho