DAWA YA MURJI YAPIKWA

CCM Logo[1]KESHO kutwa (Januari 7,2013) Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Mtwara inatarajia kukutana mjini hapa kujadili masuala mbalimbali ya chama pamoja na hoja ya wakazi wa mkoa huo kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam na kupendekeza hatua stahiki dhidi ya Mbunge wa Mtwara mjini Hasnain Murji.

Murji atakuwa kikaangoni katika kikao hicho kufuatia kauli ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula kuwa wanachama wa CCM wanaompinga Rais Jakaya Kikwete kuwa ni waasi.

Kamati hiyo itakutana huku tayari kukiwa na mgongano mkubwa baina yao, kufuatia chama hicho wilaya ya Mtwara mjini, Mbunge Murji kuunga mkono wananchi wa mkoa huo kupinga kuondolewa kwa gesi inavyovunwa kijiji cha Msimbati mkoani humo.

Mwenyekiti wa CCM wa Mtwara mjini, Ali Chinkawene hivi karibuni alisema kuwa msimamo wa chama chake ni kuungana na wananchi kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam na kwamba Serikali inapaswa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam.

“Niliitisha kikao cha kamati ya siasa kujadili nini msimamo wa chama katika hili, kamati ya siasa wakasema hawawezi kukisemea chama kwa sababu chama ni wanachama hivyo nikaitisha kikao cha halmsahauri kuu ambapo pia tuliwaalika mabalozi wa matawi” alisema Chinkawene

Alifafanua kuwa “Katika kikao hicho wajumbe walipinga kwa nguvu zote suala la gesi kupelekwa Dare s Salaam, wakaniambia niseme msimamo wao kuwa hawataki gesi iende Dar es Salaam hadi pale maslai ya Wana Mtwara yatakapowekwa wazi na serikali”

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa msimamo huo sio wake binafsi bali ni maazimio ya vikao halali vya chama hicho vinavyowakilisha wanachama na kwamba historia ya mikoa ya kusini jinsi ilivyonyimwa maendeleo ilitumika na wajumbe kujenga hoja yao hiyo.

Kwa uwamzi huo, CCM Mtwara mjini inaungana na vyama Tisa vya awali vilivyokuwa vinapinga suala hilo, vyama vingine ni Chama cha Wananchi (CUF), Chadema, NCCR-Mageuzi, SAU, TLP, APPT Maendeleo, ADC, VDP na DP, vikiwa na kaulimbiu ya gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.

Mbunge wa Mtwara mjini, Hasnain Murji ameweka wazi msimamo wake wa kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam na kuongeza kuwa yupo tayari kuvuliwa Ubunge kama ikibidi kufanya hivyo kutetea maslahi ya wananchi.

Tofauti na Murji, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia ambaye ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Mbunge wa Newala George Mkuchika Waziri wa Ofisi ya Rais Utawala Bora wao wanaonesha wazi kuunga mkono mradi huo.

Kwa nyakati tofauti mawaziri hao wamekaririwa wakiwatia moyo wananchi kuwa mradi huo unalenga kuwanufaisha wao na Taifa kwa ujumla, licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wananchi.

Novemba, 20 mwaka jana wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulhaman Kinana, Ghasia alizomewa na wananchi pale alipojaribu kutetea mradi huo.
Licha ya kwamba wanasiasa hao sio wajumbe wa Kamati ya Siasa ya mkoa, bado uwezekano wa kikao hicho kuwa kigumu ni mkubwa kutokana na baadhi kuonesha wazi kutounga mkono hoja ya gesi kupelekwa Dar es Salaam.

“Kesho kutwa (kesho) kutakuwa na kazi ngumu, wapo wajumbe waliopania kutetea maslahi ya wananchi…wanaona chama kitakufa iwapo wataunga mkono gesi kuondoka, watu wanajipanga kwa hoja sio ushabiki” kilisema chanzo chetu ambacho ni kada wa CCM.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Mohamedi Sinani amethibitisha kufanyika kwa kikao hicho Januari 7, siku ya Jumatatu kulijadili suala la gesi nap engine kauli ya mkuu wa mkoa huo kuwaita waandamanaji wapuuzi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Sinani “Tutakutana Jumatatu kwenye kikao cha kamati ya siasa mkoa baada ya hapo nitawaambia nini msimamo wa chama mkoa kuhusu gesi” alisema Sinani

Wadadisi wa mambo wanasema kikao hicho pia kitajadili msimao wa Mbunge Murji na ule wa chama wilaya na kutolea tamko
Mwisho

Advertisements