MIKUTANO YA GESI KWANZA, KUFUNIKA MTWARA

Mwenykiti wa UDP Mtwara mjini Seleman Chimpele akihutubia mkutano

Mwenykiti wa UDP Mtwara mjini Seleman Chimpele akihutubia mkutano

VUGUVUGU la kupinga gesi inayovunwa kijiji cha Msimbati, wilaya ya Mtwara mkoani hapa kwenda Dar es Salaam kwa njia ya bomba linazidi kushika kasi ambapo umoja wa vyama vya siasa vya wilayani hapa leo vinatarajia kuanza mikutano ya adhara kuelimisha wananchi juu ya athari za mradi huo.

Makamu Mwenyekiti wa umoja huo unaojumuisha vyama 10 vya siasa, Uledi Abdallah ameuambia mtandao wa KUSINI uwa kwa siku tatu mfululizo wanatarajia kuendesha mikutano mikubwa ya adhara katika viwanja vya Soko kuu, Bima na Mkanaledi.

“Katika mikutano hiyo wananchi tutawaelimisha juu ya athari za mradi huo kwa watu wa mkoa wa Mtwara leo jioni tutakuwa Soko kuu, siku inayofuata tutakuwa Bima na siku ya tatu tutakuwa Mkanaledi…tunataka wananchi waelewe” alisema Uledi ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wilaya ya Mtwara mjini.

Aliongeza kuwa “Januari 13 tutawapokea viongozi wa NCCR Mageuzi Taifa, James Mbatia na wabunge wote wanne wa chama watafanya mkutano mkubwa wa adhara mjini Mtwara”

Akizungumzia kauli ya Waziri wa Nishati na Madini Professa Sospeter Muhongo kuwa wakazi wa Mtwara hawapaswi kuizuia gesi hiyo kwa sababu zaidi ya asilimia 75 ipo baharini, Uledi alisema “Amekurupuka, hakuna sehemu ya bahari isiyo na miliki, ndiyo maana watu walikamatwa kwa kuvua eneo la Tanzania…ni kauli inayolenga kupotosha umma ionekane madai ya Mtwara hayana msingi..ni siasa zilizopitwa na wakati”

Alifafanuwa kuwa wakazi wa Mtwara hawapingi gesi kulinufaisha Taifa ila wanataka mitambo ya kuzalishwa umeme ijengwe Mtwara na kisha umeme usafirishwe kwenda kokote ndani na nje ya nchi.

“Tunataka ‘power plant’ (mashine za kufua umeme) zijengwe Mtwara halafu umeme usafirishwe hata Marekani…tunapinga na tutaendelea kupinga, iwapo serikali haitatusikiliza basi tutakwenda Mahakamani kusimamisha mradi huo” alisema Makamu mwenyekiti wa umoja huo

Aidha alibainisha kuwa hivi karibuni umoja huo ulipokea mwaliko kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini ikiwataka waende kuteta nae wizarani jambo ambalo amesema hadi sasa wanalitafakari.

“Barua inasema hadi kufikia januari 20 mwaka huu tuwe tumekwenda wizarani kuongea na waziri…sisi tunaendelea kulitafakari hilo, kisha tutatoa majibu kwao na wananchi pia”

Tofauti na ilivyokuwa awali sasa vyama hivyo vimefikia kumi baada ya kuongezeka kwa Chama cha Wananchi (CUF) na CCM, huku vyama vya awali vikiwa ni Chadema, NCCR-Mageuzi, SAU, TLP, APPT Maendeleo, ADC, VDP na DP, vikiwa na kaulimbiu ya gesi kwanza vyama baadeye, hapa hakitoki kitu, umoja huo ndiyo ulioratibu maandamano ya Desemba, 27 mwaka jana.

Wakati Uledi akibaisha hayo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara Mohamedi Sinani amesema chama hicho Januari 7, siku ya Jumatatu kitafanya kikao cha kamati ya siasa mkoa kulijadili suala la gesi.

Sinani ameidokeza KUSINI hana majibu ya suala hilo kwa sasa na kwamba alimumuomba mwandishi kuvuta subira ili kukipa uwezo kikao hicho kulijadili sula hilo bila ya kuathiriwa na fikra za mwenyekiti.

“Tutakutana Jumatatu kwenye kikao cha kamati ya siasa mkoa baada ya hapo nitawaambia nini msimamo wa chama mkoa” alisema Sinani

Mwisho