NANAUKA: SERIKALI IKAJIFUNZE MSUMBIJI

Joel Nanauka

Joel Nanauka

KADA wa CCM aliyewahi kuwa Katibu Msaidizi wa Wilaya ya Moshi Vijijini Joel Nanauka m,kazi wa Mtwara ameiitaka serikali kwenda kujifunza Msumbiji namna ya kutekeleza miradio ya gesi ili kumaliza mgogoro ubaofukuta hivi sasa baina ya wakazi wa Mtwara na serikali.

Nanauka ambaye aliweka wazi msimamo wake wa kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam alisema ni kweli gesi ni rasilimali ya Taifa na kwamba Mtwara ni sehemu ya Taifa hivyo wanahaki ya kudai rasilimali hiyo kubaki katika eneo lao.

“Nakubaliana kuwa gesi ni rasilimali ya Taifa, na Mtwara ni sehemu ya Taifa hivi kuna ubaya gani mitambo ya kufua umeme ikabaki Mtwara?…waende kujifunza Msumbiji, ule umeme unaolisha Maputo na Beira kituo chake kipo Ressano Bercia ni 1/5 ya umbali wa Mtwara Dar es Salaam ni vema wakajifunza hili si lazima vinu vya umeme vikae Dare s Salaam” alisema Nanauka

Alibainisha kuwa amesikitishwa na kauli za kejeli, dharau na kukatisha tamaa zilizotolewa na viongozi waandamizi wa serikali akiwemo Waziri Sospeter Muhongo na mkuu wa mkoa wa Mtwara Joseph Simbakalia mara baada ya maandamano ya Desemba 27 mwaka jana

“Pia napenda kueleza kusikitishwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa kuhusu ujenzi wa bomba hili katika salamu zake za mwaka mpya,napenda kutumia nafasi hii kumshauri Mh.Rais,Waziri wa Nishati na Madini na Mkuu wa mkoa kupitia upya madai 9 yalisomwa siku ya maandamano ili kutoupotosha mjadala na madai ya watu wa Mtwara” alishauri kijana huyo.

Alifafanua kuwa “Nimetoa rai hii kwa sababu ukipitia hotuba za viongozi hawa wote utagundua kuwa aidha wamepewa taarifa zisizo sahihi kuhusu madai ya wanamtwara ama wamefanya haraka kujibu au hawajaelewa kabisa madai ya wanamtwara.Kwani kilichofanyika si kujibu madai yao bali kuonyesha jinsi ambavyo hawako tayari kuwasikiliza, nadhani mtazamo huu ndio unaochochea jambo hili kuwa kubwa kila siku na kuwapa mtazamo wananchi kuwa kuna ajenda ya siri katika hili”.

Nanauka alishangazwa na kukiukwa kwa Ilani ya CCM (2010) ibara ya 63(h) na (k) iliyoanisha miradi ya kinyerezi (240MW) na mradi wa Mnazi bay (300MW) kama miradi miwili tofauti inayojitegemea.

Aidha aliwataka wabunge wa Mtwara kuacha kulumbana na badala yake watoe msimamo wa kila mmoja ili wananchi wajue nani yupo pamoja na wao na nani anawasaliti badala ya hali ya sasa ambapo wabunge wengi wapo kimya.

Alisema kuwa kipaumbele cha watu wa Mtwara si kuwa na umeme majumbani ambao ni ongezeko la gharama la maisha kiuchumi bali kupunguza makali ya maisha kwa kuwa na uhakika wa kipato kwa njia ya ajira kwa shughuli za uzalishaji viwandani na shughuli zitakazoambatana na hizo, na kwamba ni vema serikali ikazingatia kauli ya Mkurugenzi Mkuu wa Wentworthy Resource Limited inayochimba gesi ya Mnazi Bay,

Bob Mcbean iliyoripotiwa December 6 London mwaka jana kuwa watapata faida kubwa kwa kuwekeza katika kiwanda cha mbolea na kemikali nyingine, kutokana na mtambo wa kufua umeme utakaojengwa Mtwara.
Mwisho