WAZIRI AZUIWA KWA MAGOGO MTWARA

Simbachawene

Simbachawene

HOJA ya wananchi wa mkoa wa Mtwara kupinga gesi asilia kupelekwa Dar es Salaam inazidi kuchukua sura mpya siku hadi siku baada ya juzi Mbatia kufanyiwa vurugu, sasa msafara wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene unadaiwa kuzuiwa kwa magogo na mawe alipojaribu kutembelea kijiji cha Msimbati ambako gesi asilia inavunwa.

Habari za kuaminika zilizolifikia gazeti hili mjini Mtwara jana zinadai kuwa tukio hilo lilitokea saa 8 mchana mbapo waziri huyo alilazimika kugeuza msafara wake katika kijiji cha Ziwani na kurejea mjini Mtwara baada ya kutaarifiwa kuwa hali si shwari.

Habari zinadai kuwa waziri huyo aliwasili mjini Mtwara kwa ndege ya asubuhi na kupokelewa na viongozi wa mkoa ambapo inadaiwa kimyakimya alianza safari ya kwenda Msimbati kabla ya kupewa taarifa ya hali tete ya usalama.

Mashuhuda wa tukio la kufungwa kwa barabara wamesema kuwa baada ya wananchi kupata habari za ujio wa waziri huyo, walionekana wazi kutokubalina, hivyo walijikusanya na kuamua kuifunga barabara kwa kukata magogo na kuyalaza barabarani kwa lengo la kumzuia asiingie katika kijiji hicho.

Gari lililokuwa limebeba waandishi wa habari ndiyo la kwanza kuwasili kwenye kizuizi hicho hata hivyo hawakudhuriwa zaidi ya kuamriwa kugeuza gari na kuondoka.

Kubwa linalodaiwa kuwakasirisha wananchi hao ni kauli za kejeli za viongozi wa serikali kuwa wananchi wa kijiji hicho wananufaika na gesi asilia kwa kutumia umeme bure ili hali wanalipa ankara za umeme kila mwezi.

“Waziri wa Nishati na Madini Sospeter Muhongo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora George Mkuchika kupitia vyombo vya habari wamesema sisi tunatumia umeme bure…hizi ni kejeli…ninazo bili za umeme tangu nilipounganishiwa” alisema mkazi wakijiji hicho kwa sharti la kutotajwa jina

Aliongeza kuwa “Kana kwamba haitoshi leo wanataka waje kututukana waziwazi ili wadhihirishe kuwa sisi ni wapuuzi, hatujasoma …tumesema baasi, hatutaki kuonana na kiongozi yeyote yule”

Mwenyekiti wa kijiji cha Msimbati Salum Athumani Tostao anathibitisha kuwapo kwa hali hiyo na kuongeza kuwa polisi walikwenda kijijini hapo na kufyatua mabomu ya machozi kuwatisha wananchi hao hata hivyo msimao wao uliendelea kuwa hawataki kuongea na waziri huyo.

“Walikuja polisi, kama kawaida yao wakafyatua mabomu ya machozi hewani…hakuna mwananchi aliyekimbia, ilikuwa kama mchezo wa mpira wa miguu wao wanafyatua mabomu hewani wananchi wanashangilia na kuzidi kuongezeka eneo la tukio” alisema Tostao akiongea kwa simu.

Alifafanua kuwa “ Waziri hakuwahi kufika huku, ilikuja gari moja iliyobeba waandishi, walipoona hali ni tete wakampigia simu asije na ndipo polisi walipokuja badala yake…polisi waliacha kupiga mabomu na kuamua kuongea na wananchi ambao hawakuonesha woga wowote, waliwaambia polisi hawataki waziri akanyaje ardhi ya kijiji chao”.

Alibainisha kuwa yeye kama kiongozi wa kijiji hakupewa taarifa juu ya ujio huo na kwamba hilo halikumshangaza kwa madai ni kawaida ya viongozi hao kuipuuza serikali yake kwa kuingia kijijini hapo na kutoka bila ya kutoa taarifa kwake.

“Wananchi walipata taarifa kuwa waziri au naibu wake anakuja na ndipo walipofunga barabara wakisema hawataki kumuona akikanyaga ardhi yao…kwa bahati nzuri gari ya kwanz akufika ilikuwa ya waandishi wa habari, kwa huruma wananchi wakawaambia warudi” alisema mwenyekiti huyo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki akiliri wananchi kufunga barabara ingawa alikanusha madai ya Naibu Waziri Simbachawene kuwapo ziarani mkoani hapa.

“Waandishi wa habari waliokwenda katika ziara za kazi zao za kawaida ndiyo waliozuiliwa na wananchi hao…Naibu waziri hajawahi kufika Mtwara kwa siku ya jana…wananchi walidhani hilo gari ni la waziri lakini ukweli si yeye” alisema Kamanda Nzuki

Akizungumzia hilo Simbachawene alisema “Hapana sio kweli, ningekuja hapo mjini singeweza kujificha…tatizo la wananchi wetu hawajapata elimu sasa nitaendaje huko kimyakimya ili iweje….jana nilikuwa ofisini na vikao kutwa nzima…nenda ‘airport’ (uwanja wa ndege) kaulize…hata mimi nimeona kwenye jamii forum, ile ni ‘open paper’ (kurasa wazi) mtu yeyote anaweza kuweka chochote”

Aliongeza kuwa “Inasikitisha, aheri wewe uliyenipigia simu kuliko magazeti yanayochukua habari kwenye jamii forum…inaonekana kuna watu wamedhamiria hili jambo hili”

Tukio hilo limetokea siku moja tangu mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia afanyiwe vurugu na baadhi ya watu katika mkutano wake wa adhara uliofanyika Uwanja wa Mashujaa mjini hapa na badaye kutaka kumdhuru kwa madai ya kutoridhishwa na hotuba yake hali iliyosababisha akatishe ziara yake.
Mwisho