MTWARA WAMPINGA MKAPA

Katibu wa CUF, Mtwara Mjini, Saidi Kulaga

Katibu wa CUF, Mtwara Mjini, Saidi Kulaga

Askofu wa Kanisa la Angalikan Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a

Askofu wa Kanisa la Angalikan Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a

MAKUNDI mbalimbali ya jamii mkoani Mtwara wakiwemo Maaskofu, Masheikh na vyama vya siasa wamelipinga vikali tamko la Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa wakisema kuwa limeegemea upande mmoja na kwamba alipaswa kumshauri Rais Jakaya Kikwete namna ya kumaliza mgogoro uliopo badala ya wananchi.

Kwa nyakati tofauti viongozi hao leo walisema licha ya kwamba amechelewa kutoa ushauri huo, Mkapa ametoa ushauri unaobeza upande wa wananchi pekee na hajasema chochote kuhusu serikali kitendo ambacho walidai kinawafanya watilie shaka tamko hilo.

Katika tamko lake alilolitoa jana Mkapa alisema “Fujo vitisho, kupimana nguvu na malumbano sio masharti ya maendleo…nikiwa kama mwana-Mtwara na raia mwema, mpenda nchi, nimefedheheshwa sana na matukio haya ya siku za hivi karibuni Mtwara. Kwa sababu hiyo natoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara, kusitisha harakati hizi za maandamano na mihadhara”

“Badala yake wajipange kukaa katika meza moja, kupitia historia, kutathimini mipango, kuchambua kwa kina mikakati ya utekelezaji wake, hatimaye kufikia muafaka wa ujia wa maendeleo. Liwezekanalo leo lisingoje kesho” alisema Mkapa

Askofu Mteule wa Kanisa la KKKT Dayosisi Mpya ya Kusini Mshariki, Mchungaji Lucas Mbedule alisema katika mahojiano na KUSINI kuwa Mkapa, amechelewa kutoa ushauri wake na kwamba kwa hali ya sasa alipaswa kumshauri Rais Kikwete akubaliane na matakwa ya wananchi.

“Mimi kama kiongozi wa dini namuheshimu sana Mkapa, lakini amechelewa kutoa kauli yake, yeye alipaswa kumshauri rais mwenzie…kutoa tamko lake saa hizi kunatufanya tuwe na mashaka naye, nasikitika kuwa kauli aliyoitoa haitakuwa na ‘impact’ (mafanikio) kwa wakati huu” alisema Mchungaji Mbedule ambaye awali alitoa msimamo wake wa kupinga mradi huo

Aliongeza kuwa “Usiwalaumu kwa kuandamana na kuitisha mikutano, jiulize ungejuaje kama wananchi hawataki mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi, kama sio kupitia maandamano, mikutano na mihadhara, atambue kuwa suala hili lilianza kabla ya maandamano nani alijua kuwa Mtwara hawataki gesi itoke? nilidhani amshauri Kikwete asitishe mradi”

Msemaji wa Shura ya Maimam mkoani Mtwara Sheikh Abubakari Mbuki alisema “Tunamuheshimu sana Mkapa lakini nachelea kusema amekosea…siku nyingi alikuwapo Mtwara, suala la gesi alilifahamu kwanini asiliseme mapema…anaotaka kuzungumza nao wapo Mtwara kwanini akazungumzie Dar es Salaam…sawa na Kikwete kuzungumzia gesi Tabora” alisema Sheikh Mbuki

Aliongeza kuwa “Tutaendelea na makongamano, kwanini afedheheshwe na harakati zetu na asifedheheshwe na kauli za mkuu wa mkoa (Joseph Simbakalia), waziri (Profesa Sospeter Muhongo) na Rais Kikwete, anadhani wao wapo sahihi?…kubeza maandamano, mikutano ni kuwakosea wana-Mtwara”

Askofu wa Kanisa la Angalikan Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a akizungumzia tamko la Mkapa alisema “Nadhani amechelewa…awaite viongozi aliowaachia madaraka awaambie wasipuuzie jambo hili …naunga mkono hoja ya serikali kukaa pamoja na wananchi wa Mtwara…maandamano ni haki ya msingi ya Kikatiba wasipuuzwe unafikiri wangefanya nini kama hawasikilizwi”

Aliongeza kuwa “Tanzania tumekuwa mafundi wa kutatua migogoro ya wenzetu, kinawashinda nini hili…hapa ni suala la kuweka wazi mikataba, kama kweli serikali ina mipango mzuri na wananchi wa Mtwara si iweke wazi…wanashindwaje kujieleza, kuna nini hapa…wajibu hoja wasitafute mchawi, mjusi ukimfukuza sana mwisho anakuwa nyoka…wananchi hawa wamesema baasi”

Alisisitiza kuwa “Lazima sisi (viongozi wa dini) tuseme kwa sababu kwenye waumini wetu wapo maskini…sasa tunaposema mtu mwingine asianze kumtafuta aliyesema, sioni kama busara badala ya kutatua tatizo unalaumu watu kuwa ndiyo chanzo cha tatizo…kigugumizi cha nini kama mradi una maslahi na watu wa Mtwara?”

Katibu wa Chama cha Wananchi CUF, Mtwara Mjini, Saidi Kulaga alisema kwa hatua iliyofikia Mkapa alipaswa kuishauri serikali na sio wananchi kwa sababu wananchi wameweka wazi madai yao na kwamba ni wajibu wa serikali kuyaafiki.

“Hatuwezi kukaa meza moja kujadili, tunajadili nini wakati madai yetu yapo wazi…serikali itamke imesitisha mradi huu, nasi hoja yetu itakuwa imekufa…tunachotaka vinu vya kufua umeme wa megawati 300 vijengwe Mtwara na kiwanda cha kusafirsha gesi…baada ya hapo umeme na gesi hiyo iende kuuza kokote duniani” alisema Kulaga na kuongeza

“Hatutaacha mikutano, maandmano, kongamano, na majadiliano…tunaomba wananchi wapinge dhuluma hii ya serikali dhidi ya mikoa ya kusini…wasihofu katiba inatulinda, tunateteta Katiba isikiukwe…Mkata asitushauri sisi nini cha kufanya wakati anaona tunachokifanya, Mkapa anamjua mchawi wetu, aeleze wazi asifiche mgogoro uishe”

Mwenyekiti wa CCM Mtwara mjini Ali Chinkawene alikana kuzungumzia kauli ya Mkapa akisema “Umesikia mwandishi leo sitaki kuzungumzia chochote…baada ya halmshauri kuu Jumamosi ijayo siku ya Jumapili nitazungumzaq na wewe”
Mwisho