MTWARA WAMPINGA PINDA, WASEMA GESI HAITOKI

Mkutano wa adhara...Katani Katani

Mkutano wa adhara…Katani Katani

WAKAZI wa mkoa wa Mtwara wameendelea kuupinga mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi asilia kwa bomba kwenda jijini Dar es Salaam kutoka kijiji cha Msimbati mkoani humo, licha ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa ufafanuzi ulionesha kukubalika katika kikao hicho cha majumuisho jana.

Watu wengi waliohojiwa na KUSINI leo wanaonesha kutokubalina na ufafanuzi, uliotolewa na Waziri Pinda baada ya kutumia siku mbili mfululizo kusikiliza kilio cha wakazi hao.

Wakazi hao wanasema hoja moja imepatiwa ufumbuzi, nayo ni ile ya ujenzi wa kiwanda kusafisha gesi mkoani humo na kwamba hoja ya kupinga kusafirishwa kwa gesi hiyo kwa njia ya bomba bado haijapatiwa majibu na kwamba wanaendelea na msimamo wao wa kuupinga mradi huo.

Akizungumza katika mkutano wa majumuisho, Pinda alisema hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirisha kwa njia ya bomba na kwamba usindikaji utafanyika Mtwara.

“Wataalam wanasema gesi haiwezi kwa namna yeyote ile kusafirishwa kama ilivyo, lazima ibadilishwe kuwa hewa au barafu…kiwanda cha kusafisha gesi kitajengwa Madimba, gesi yote itakayotoka Mnazi Bay itasafishwa hapo na masalia yote yatabaki huku ili kuvutia viwanda vya mbolea na vingine vinavyotumia malighafi hizo” alisema Pinda na kuongeza

“Kama tungekuwa tunasafirisha gesi ghafi basi hata kiwanda cha Dangote kisingejengwa hapa…gesi itakayopelekwa Dar es Salaam ni ile iliyosafishwa kwa ajili ya matumizi ya kuzalisha umeme…tusaidieni wenzetu kuliokoa Taifa na tatizo la umeme”

“Nimemabia hapa ,gesi lazima isindikwe Mtwara, haitoki hadi viwanda vije…nadhani hili ni jambo jema lazima tuliwekee utaratibu …nikawauliza wataalam wangu kwani kiwanda cha kusafisha gesi kinajengwa wapi, wakanijibu Madimda…nikasema kumbe tatizo kubwa ni kutowaeleza wananchi suala la gesi vya kutosha…Nafikiri tatizo ni sisi Serikali hatukuwa na mpango mzuri wa kuwaelimisha wananchi” alifafanua Pinda

Shura ya Maimamu mkoani hapa imesema haijaridhika na majibu waliyoyaita mepesi ya Waziri Mkuu Pinda katika hoja nzito na kwamba bado serikali haijaupatia suluhu mgogoro huo.

“Baada ya kutoka pale tulifanya kikao kupitia maelezo ya waziri mkuu, kuna maeneo hatujaridhika nayo…amezungumzia ‘powerplant’ (mtambo wa kufua umeme) kama mtambo wa kusafisha gesi, ndiyo aliousema utajengwa Madimba…lakini sisi tunahitaji ‘powerplant’, mashine za kufua umeme pamoja na hiyo ya kuchakata gesi iwe Mtwara…katika eneo hilo hatujaridhika” alisema Sheikh Abubakar Mbuki msemaji wa shura hiyo.

Aliongeza kuwa “waziri asituambie tu gharama za kutandaza nyaya kubwa kuliko bomba la gesi akaishia hapo, atuambie gharama hizo ni kiasi gani badala ya kusema ni gharama kubwa…mbona gharaza za bomba zipo wazi, kwanini hizi za nyaya hazisemwi…tunasema madai yetu ya kutaka mtambo wa kufua umeme ujengwe Mtwara yapo palepale”

Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Katani Katani alisema “Sijaelewa kabisa…nashangaa watu wanashangilia wakati madai yetu ya msingi hayajapata ufumbuzi…dai letu la kwanza lilikuwa viwanda vya kuchakata gesi vijengwe Mtwara, hilo limepatiwa ufumbuzi, la pili lilikuwa mitambo ya kufua umemem megawati 600 zijengwe Mtwara”

Aliongeza kuwa “hili hajalipatia ufumbuzi, tunachokataa sisi wana Mtwara ni kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, tunataka mashine zinazojengwa Kinyerezi zihamishiwe Mtwara…kutuambia kupeleka umeme Dar es Salaam kwa njia ya nyaya ni gharama kubwa hilo sikubaliani”

Alisema kuwa kutokana na kutopatikana kwa ufumbuzi wa dai hilo moja, Katani anasema kuwa bado wananchi wa Mtwara wataendelea kupinga mradi huo kama madai yao ya awali yalivyokuwa.

Mmoja wa Maaskofu Maarufu Mtwara, kwa sharti la kutotajwa jina alisema “Nimemsikia waziri mkuu, amejaribu kujibu hoja lakini bado kuna masuala ya msingi hajayaguswa yanayohusu mustakabali wa maendeleo ya watu wa kusini, kama barabara…sisi tumesem gesi isiende Dar es Salaam kwa bomba”

Aliongeza kuwa “Lugha iliyotumia na Waziri wa Mambo ya Ndani Dk. Emanuel Nchimbi ni ya vitisho, sikuipenda hata kidogo, watu ambao hawajsitarabika wasije huku kwetu…unatutisha na jeshi ili iweje…kamwe vita haiwezi kumaliza mzozo wetu aelewe hilo…pia kauli za Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene eti ameandaa jeshi, kauli hizi zitatufikisha pabaya”

Hamza Halidi mkazi wa Mtwara alisema hadi sasa hajaelewa tafsiri ya kauli ya Waziri Pinda kwa kile alichokidai kuwa madai yao ya msingi ni kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

“Sijamwelewa…sisi tunapinga gesi istoke yeye anasema itatoka ikiwa imesafishwa, sasa kwa mtazamo wa kawaida unadhani hoja yetu imepatiwa ufumbuzi…sisi tunataka umeme uzalishwe Mtwara huko uende umeme sio gesi” alisema Halidi

mwisho

Advertisements