ASKOFU: VURUGU MTWARA SASA INATOSHA

3

1

4

5

ASKOFU wa Kanisa la Angalikana Dayosisi ya Newala, mkoani Mtwara, Oscar Mnung’a amewaomba wakazi wa mkoa huo kuwa na subira ili kuipa Serikali nafasi ya kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kufuatia mgogoro wa kupinga usafirishaji wa gesi asilia kwa bomba kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam.

Akitoa mahubiri wakati wa Misa ya Jumapili leo mjini Mtwara, Askofu Mnung’a pia aliviasa vyombo vya habari kuacha kukuza mgogoro huo kwa kuandika habari zenye uchochezi na badala yake vihabarishe kwa kuzingatia ukweli na hali halisi iliyopo.

“Nawaagiza Wakristo wote wa Dayosisi yote sasa tutulie…habari ya gesi sasa inatosha, Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) alipata nafasi ya kuzungumza na makundi yote, tumemuelewa…nanyi mkawaambie wapangaji wenu, jirani zenu kuwa inatosha, tuipe nafasi Serikali ya kutekeleza waliyotuahidi” alisema Askofu Mnun’ga

Aliongeza kuwa “Mimi nilikuwa wa kwanza kutoa kauli ya kupinga mradi huo…wamekuja wametuelimisha tumeelewa…kuna wengine wanasema hawajamuelewa waziri mkuu, wasubiri wataelimishwa”

Alifafanua kuwa wakazi wa mkoa huo wanapaswa kutulia na kwamba vurugu zozote zisipewe nafasi ili kuidhihirisha jamii kuwa wao sio wapuuzi.

“Tukiendelea kupinga sasa sisi tutadhihirisha kuwa ni wapuuzi kweli kweli…naiomba Serikali wale wote watakao anzisha vurugu wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria” alisisitiza Askofu huyo huku akishangiliwa na waumini

Aidha akizungumzia vyombo vya habari alisema “Nawaomba sana waandishi wa habari munaweza kutumika vizuri au vibaya …msichochee jamii kuingia kwenye machafuko …tukiingia kwenye machafuko hamtapona…msiongeze chumvi katika habari zenu, tunajua mnatupasha habari lakini vema kulinda amani yetu”

Akigusia kauli za baadhi ya mawaziri alisema bila kuwataja majina alisema “Baadhi ya mawaziri wanapotoka…eti sisi tuna nguvu, tuko tayari tumejiandaa na nini…jiandae kutoa majibu…narudia tena tutulie”

Wakati Askofu Mnung’a akisema hayo, Shura ya Maimamu mkoani hapa imesema haijaridhika na majibu waliyoyaita mepesi ya Waziri Mkuu Pinda katika hoja nzito na kwamba bado serikali haijaupatia suluhu mgogoro huo.

“Baada ya kutoka pale tulifanya kikao kupitia maelezo ya waziri mkuu, kuna maeneo hatujaridhika nayo…amezungumzia ‘powerplant’ (mtambo wa kufua umeme) kama mtambo wa kusafisha gesi, ndiyo aliousema utajengwa Madimba…lakini sisi tunahitaji ‘powerplant’, mashine za kufua umeme pamoja na hiyo ya kuchakata gesi iwe Mtwara…katika eneo hilo hatujaridhika” alisema Sheikh Abubakar Mbuki msemaji wa shura hiyo.

Aliongeza kuwa “Waziri asituambie tu gharama za kutandaza nyaya kubwa kuliko bomba la gesi akaishia hapo, atuambie gharama hizo ni kiasi gani badala ya kusema ni gharama kubwa…mbona gharaza za bomba zipo wazi, kwanini hizi za nyaya hazisemwi…tunasema madai yetu ya kutaka mtambo wa kufua umeme ujengwe Mtwara yapo palepale”

Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Katani Katani alisema “Sijaelewa kabisa…nashangaa watu wanashangilia wakati madai yetu ya msingi hayajapata ufumbuzi…dai letu la kwanza lilikuwa viwanda vya kuchakata gesi vijengwe Mtwara, hilo limepatiwa ufumbuzi, la pili lilikuwa mitambo ya kufua umemem megawati 600 zijengwe Mtwara”

Aliongeza kuwa “hili hajalipatia ufumbuzi, tunachokataa sisi wana Mtwara ni kusafirisha gesi kwa njia ya bomba, tunataka mashine zinazojengwa Kinyerezi zihamishiwe Mtwara…kutuambia kupeleka umeme Dar es Salaam kwa njia ya nyaya ni gharama kubwa hilo sikubaliani”

Alisema kuwa kutokana na kutopatikana kwa ufumbuzi wa dai hilo moja, Katani anasema kuwa bado wananchi wa Mtwara wataendelea kupinga mradi huo kama madai yao ya awali yalivyokuwa.

Umoja wa vyama Tisa vya siasa vya upinzani mkoni Mtwara tayari umetoa tamko la kutokubalina na kauli ya waziri mkuu na kusisitiza kuwa mpango wa kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam upo palepale.

“Sisi tuliandaa maandamano Desemba, 27 mwaka jana tukipinga gesi kupelekwa Dar es Salaam kwa njia ya bomba, sasa waziri mkuu amekuja kutusikiliza kisha kusema msimamo wa Serikali ni ule ule…kimsingi hatujamwelewa na madai yetu yapo palepale” aliongeza

Msemaji wa Umoja huo Hamza Masoud Licheta, alisema licha ya polisi kuwazuia kufanya mikutano ya adhara bado umoja huo utaendesha harakati zake kwa njia zingine na pale itakapofika wakati Serikali haisikilizi kilio chao watakwenda kuupinga mradi huo Mahakamani.

“Hatua yetu ya mwisho ni kwenda kuupinga mradi huo Mahakamani…leo wametuzuia kuendesha mikutano wakidhani ndiyo njia ya kutunyamazisha, wakumbuke hii ni hoja ya wananchi…hata ukituziba sisi midomo wananchi wataendelea na mapambano ya kupinga dhuluma”

“Watuambie kwanza masalia ya gesi inayotumika Mtwara, Kilwa yamevutia viwanda vingapi, yapo wapi …hoja yetu ni Mtwara kuwa kitovu cha biashara ya gesi” alisema Licheta

Akizungumzia radhi ya mkuu wa Mkoa Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia alisema “Hatukubali radhi aliyoitoa mkuu wa mkoa…ni shindikizo kutoka kwa waziri mkuu na sio kutoka moyoni mwake…kama yeye ni muungwana mbona hakutuomba kabla ya hapo…hatuko tayari kufanya naye kazi”
Mwisho

Advertisements