CCM KUMSHUGHULIKIA MURJI

MURJI[2]

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mtwara kimedai kauli zilizotolewa na mbunge wake jimbo la Mtwara mjini, Hasnain Murji kuungana na wananchi wanaoshinikiza gesi kutotoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam, ni sawa na kukihujumu chama.

Akizungumza na Mwananchi jana Katibu wa CCM mkoani humo, Alhaji Masoud Mbengula alisema chama kilishangazwa na kauli za mbunge huyo, kwa mba alionekana wazi kuwaunga mkono wapinzani na siyo wananchi.

“Tayari tumemwita katika vikao na kumhoji kuhusiana na kauli alizozitoa, pia taarifa rasmi zipo na tumezipeleka makao makuu ya chama ambapo ndiyo watatoa uamuzi,” alisema Mbengula na kuongeza;

“Tumesikitishwa sana na kauli ya Murji. Kauli yake ilionekana kuwaunga mkono wapinzani kwa kuwa msimamo na nia yao ni kuona Ilani ya CCM haitekelezwi. Kama alikuwa na hoja alitakiwa kutafuta njia za kusema na siyo kuzungumza jambo hilo hadharani. Kwa namna moja au nyingine yeye amechangia kukihujumu chama.”

Wakati katibu huyo akieleza hayo, Desemba 29 mwaka jana baada ya Murji kutoonekana kwenye maandamano ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara ya kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam yaliyofanyika Desemba 27, aliibuka na kusema anaunga mkono wananchi hao kutetea maslahi yao.

Alisema hoja ya msingi ni kujadili kwa namna gani bomba la gesi litanufaisha Wanamtwara, kufafanua kuwa kwa kiasi fulani hakubaliani na hoja ya gesi isiende Dar es Salaam lakini naungana na wananchi kudai jinsi watakavyonufaika na gesi hiyo.

Alisema anakubalina na gesi iende Dar es Salaam kwa sharti la kuzalisha umeme, si kwa matumizi mengine, kwamba wakianza kuitumia kwenye viwanda watakuwa wameiua Mtwara kabisa, huku akiunga mkono wana nchi kuandamana kwa maaelezo kuwa ni haki yao ya msingi na hawapaswi kubezwa na mtu yeyote kwa sababu wanateteta haki yao ya msingi ya kufaidika na rasilimali yao.

Katika maelezo yake Mbengula alisema chama hicho kilihujumiwa huku akitoa mfano wa matukio ya kuchoma moto nyumba. Nyumba hizo nyingi zilikuwa za viongozi wa CCM wakiwamo wabunge pamoja na ofisi, hasa zipo zilizochomwa wilayani Masasi mkoani humo.

“Nyumba zilizochomwa moto zote ni za viongozi na wabunge wa CCM. Mpango huu ulionekana kupangwa na kuratibiwa na watu fulani kwa lengo la kukihujumu chama” alisema Mbengula.
Murji

Mwananchi Jumapili jana lilizungumza na Murji ambapo pamoja na mambo mengine alisema kuwa kauli alizozitoa nazo ziliungwa mkono na CCM.

“Hata siku moja zikuwahi ku pinga gesi kwenda Dar es Salaam.Lengo langu ni kutaka wananchi wafaidike kwanza na gesi, watu walitaka kujua watanufaika vipi na si vinginevyo,” alisema Murji na kuongeza;

“Hata katika ufafanuzi alioutoa Waziri Mkuu alieleza jambo hilo, hata CCM waliungana na mimi kutaka gesi iwanufaishe wakazi wa Mtwara.”

Alisema kuwa kwa sasa hali imekuwa shwari mkoani humo, huku akiwataka wananchi kuwa watulivu, kwani tayari Serikali imeshaeleza msimamo wake na jinsi itakavyotekeleza mradi huo.

Akizungumzia kauli za mbunge huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema, “Taarifa rasmi za Murji bado hatujazipata, lakini inawezekana zikawa zimefika makao makuu kwa kuwa hivi sasa pale ofisini Sekretarieti yote ipo mkoani Kigoma katika sherehe za miaka 36 ya chama.”

Alifafanua kwamba taarifa za mbunge kwanza zinajadiliwa na wilaya na mkoa, baadaye kupelekwa taifa, kusisitiza kuwa huenda zikawa zimeshafika.
Source Mwananchi Tanzania
Mwisho

Advertisements