LIPUMBA AWASHA TENA MOTO WA GESI

Lipumba

Lipumba

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Serikali inayo wajibu wa kuzuia neema ya gesi iliyopatikana mikoa ya kusini kugeuka kuwa laana kwa kurejea tamko la Ikulu la Oktoba, 12, 2011 linaloweka wazi nia ya serikali ya kujenga mitambo ya kufua umeme wa megawati 300 mkoani Mtwara.

Akitoa mada ya matumizi ya rasilimali gesi kwa maendeleo ya uchumi wa mikoa ya kusini hususani Lindi na Mtwara na Taifa kwa ujumla katika ukumbi wa Veta mjini Mtwara jana Lipumba alisema Serikali inapaswa kutoa ufafanuazi kwa wananchi sababu za msingi za kukiuka tamko lake hilo ambalo lina gharama nafuu na kung’ang’ania mradi wenye gharama kubwa

Akinukuu sehemu ya tamko hilo la Ikulu la Oktoba, 12, 2011 Lipumba alisema “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo.”

Aliongeza kuwa “ Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.

Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania”

Lipumba alibainisha kuwa serikali inakusudia kujenga bomba lenye ukubwa wa kusafirisha futi za ujazo bilioni 200 kwa wakati mmoja ili hali uwezo wa kampuni ya Wentworth Resources kuzalisha gesi kwa sasa ni futi za ujazo bilioni 80 hali itakayoilazimu kampuni hiyo kufanya jitihada za kuzalisha gesi ya ziada kukidhi mahitaji ya bomba hilo.

Alisema haoni mantiki kwa serikali kung’ang’a kutekeleza mradi wenye gharama
kubwa zaidi ili hali kusafirisha umeme kutoka Mtwara kwenda mikoa Sita ambayo haijaunganishwa kwenye gridi ya Taifa ni nafuu na wenye maslahi zaidi kwa Taifa.

“kufua umeme wa Megawati 300 Mtwara na kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa kutagharimu dola milioni 684 wakati ujenzi wa bomba la gesi Mtwara hadi Dar es Salaam kutagharimu dola milioni 1220 za Kimarekani …ni mara mbili ya gharama za kuzalisha umeme Mtwara na kusambaza mikoa sita” alifafanua Lipumba na kuongeza

“Serikali itoe ufafanuzi wa mradi huo, mantiki ya kufanya hivyo ni ipi, hakuna uwazi badala yake kuna ubabe, kutisha watu”
Aidha Lipumba alizungumzia kuyumba kwa soko la Korosho ambapo alitaka kuimarishwa kwa vyama vya ushirika ili viweze kuhudumia wakulima vizuri sanjari na wananchi wa mikoa hiyo kuwekeza kwenye elimu.

Wakati Lipumba akitoa kauli hiyo, Shura ya Maimamu Mkoani Mtwara imetoa tamko likiwataka wananchi wa mkoa wa Mtwara kuepuka vurugu wakati wakiendelea na msimamo wao wa kupinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisi za Mwananchi mkoani Mtwara, Katibu wa shura hiyo, Sheikh Idrisa Lingondo alisema kimsingi Shura ya Maimamu inaendelea na msimamo wake wa kupiga mradi huko kwa maelezo kuwa hauna maslahi kwa wakazi wa kusini.

“Shura ya maimamu inawaomba wananchi wa mikoa ya kusini kuwa watulivu na kulipinga suala la kujegwa kwa bomba la gesi kwa njia ya amani bila kumdhuru yeyote tunayetofautiana naye kimawazo na wala kuharibu mali zake ikiwa pamoja na mali za Serikali” alisema Sheikh Lingondo

Washiriki wa Kongamano hilo lililowashirikisha viongozi wa CUF wa mikoa ya Lindi na Mtwara, viongozi wa serikali, dini na wakazi wa mikoa hiyo na kuandaliwa na CUF walisisitiza kuwa hawako tayari kuona rasilimali hiyo ikipelekwa jijini Dar es Salaam na kwamba matumizi ya nguvu na vitisho hayaweza kusaidia kulegeza msimamo wao.

“Suala la gesi lazima lichukuliwe kwa uzito wake, vinginevyo laana inaweza kuingia…watu hawako tayari kwa namna yeyote ile kuonagesi ikiondoka kwa njia ya bomba” alisema Saidi Abdallah
Mwisho

Advertisements