HALI HALISI MTWARA

H10ali ya usalama ndani ya Mji wa Mtwara ni tete, watu watatu wanadaiwa kupoteza maisha na wengine kadhaa kujeruhiwa, milio ya mabomu ya machozi na bunduki kila kona.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Ligula Mohamedi kodi amethibitisha kupokea mwili wa mtu mmoja ukiwa umetobolewa kwa kitu kinachoaminika kuwa ni risasi na majeruhi wengi.

Idadi kamili ya vifo hadi sasa haijafamika, KUSINI Inaendelea kufuatilia

Habari zinadai kuwa watu wanne wameuawa akiwemo polisi aliyekuwa anakwenda kazini. Mganga Mkuu wa hospitali ya Rufaa ya Ligula amesema amepokea maiti nne na majeruhi kadhaa hadi sasa

Habari kutoka Mtaa wa Majengo zinadai kuwa vijana wamevamia ofisi ya CCM kata na ofisi ya serikali ya Kata hiyo na kuanza kuzibomoa, pia nyumba ya mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Mtwara-Mikindani Ali Chinkawene imerushwa mawe.

Ofisi ya CCM Mtwara Vijini iliyopo eneo la Sabsaba nayo imechomwa moto na watu wasiojulikana.

Katika mtaa wa Magomeni kundi la vijana linadaiwa kuwasha tairi la gari moto katikati ya barabara, Mikindani inadaiwa kuwa ofisi ndogo ya mbunge wa Mtwara Mjini, Asnein Murji na ofisi ya CCM wilaya ya Mtwara Vijijini iliyopo Mtaa wa Sabasaba zimechomwa moto.

Habari za hivi punde zinasema gari lililobeba wanajeshi kutoka wilaya ya Nachingwea mkoani lindi limepata ajali eneo la Nanganga wilaya ya Masasi mkoani Mtwara jioni hii.

Inadaiwa wanajeshi hao walikuwa wanakujakusaidia kutuliza ghasia zinazoendelea.

Shule za Msingi Shangani, Majengo wanafunzi walirejeshwa nyumbani mara baada ya mabomu ya machozi kuanza kurindima hewani.

Tangu asubuhi kama ilivyokuwa Mei, 17 mwaka huu mji wa Mtwara ulikuwa kimya, huduma nyingi za kijamii zilifungwa, ukiwemo usafiri wa Pikipiki, Daladala, usafiri wa kwenda wilayani, Maduka, Soko kuu na kituo kikuu cha Mabasi.

Hali hiyo imejitokeza kufuatia kusambazwa kwa vipeperushi na watu wasiojulikana vikiwataka wafanyabishara mjini hapa kusitisha huduma za kijamii ili wasikilize Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini juu ya hatima ya madai yao ya kupinga mradi wa usafirishaji wa gesi kutoka Msimbati hadi jijini Dar es Salaam kwa njia ya bomba.

Hata hivyo wakazi wengi wamekosa fursa hiyo baada ya matangazo yanayorushwa na televisheni ya Taifa (TBC 1) kutopatikana kwa dishi za kawaida isipokuwa DSTV tangu leo jioni, hata hivyo matangazo yalirejea leo muda mfupi baada ya Wizara ya Nishati na Madini kusoma bajeti yake.

Vipeperushi kama hivyo vilisambazwa mwanzoni mwa wiki iliyopita na kusababisha huduma za kijamii kusimama siku ya Ijumaa, Mei 17, 2013 vikidai kuwa siku hiyo bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ingesomwa Bungeni hata hivyo haikusomwa.

Baadaye taarifa zilisema kuwa bejeti ya wizara hiyo ingesomwa Mei, 22 mwaka huu leo) hali iliyotoa nafasi kwa wandaaji wa vipeprushi hiyo kusambaza ujumbe mwingine wa kutaka huduma zisimame kwa siku ya leo na kesho kwa njia ya simu za mkononi na.

Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Mtwara Mikindani, Chinkawene amethibitisha kubomolewa kwa ofisi ya chama chake, ofisi ya kata na nyumba yake kurushiwa mawe.

“Ni kweli ofisi ya CCM, Ofisi ya Serikali ya Kata zimebomolewa, nyumba yangu imerushiwa mawe” aliongea Chinkawene kwa sauti ya chini na kukata simu

Wakati Mtwara mjini hali ikiwa si shwari, Kijijicha Msimbati ambako gesi asilia inachimbwa hali ni shwari na wananchi wanaendelea na kazi zao kama kawaida

“Maduka na soko limefunguliwa, huku hali shwari kabisa, ingawa msimamo wetu upo palepale, hatutaki gesi iende Dar es Salaam kwa njia ya bomba” alisema Juma Ayoub mkazi wa Msimbati

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa alisema taarifa kamili atatoa baadaye na kwamba kwa sasa anaendelea na oparesheni.
Mwisho

Advertisements