JWTZ: ‘TUTAKAOWAHOJI’ MTWARA NI WENGI

Brigedia Jenerali John Chacha

Brigedia Jenerali John Chacha

Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limesema lililazimika kuwakamata baadhi ya wafanyabiashara, waendesha pikipiki na watu wengine kutokana na jeshi hilo kupokea taarifa za siri kuwa watu hao wanahusika kuchochea vurugu za gesi zilizotokea Mtwara Mei, 22/23 mwaka huu.

Mkuu wa Brigedia ya ulinzi ya kusini, Brigedia Jenerali, John Chacha amebainisha hayo, leo alipokuwa alijibu hoja mbalimbali zilizoelekezwa kwake wakati wa semina ya ufahamu wa gesi kwa askari polisi, waendesha pikipiki, wazee na wanahabari iliyofanyika katika ukumbi wa Boma mjini Mtwara.

Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, kiongozi huyo wa jeshi allisema si nia ya jeshi lake kupambana na wananchi ila lina wajibu wa Kikatiba wa kulinda amani ndani na nje ya mipaka.

“Ni kweli kumekuwapo na wakati mwingine vitendo vinavyofanywa na baadhi ya askari pengine ni kinyume na utaratibu, kama nilivyosema si jukumu la jeshi kupambana na wananchi wake, lakini baada ya wananchi wa Mtwara kupambana na polisi, kuchoma moto nyumba na ofisi za serikali, kusimamisha huduma za jamii, tukasema haiwezekani tulinde mipaka wakati watu wanauwana huku” alisema Chacha bila kufafanua vitendo hivyo na kuongeza

“Kuna wafanyabiashara wakubwa hapa Mtwara hapa, ndiyo wachangiaji wakubwa wa kuendesha vurugu, majina ninayo hapa zaidi ya 50, haya wenzangu nyie viongozi wa bodaboda wanasema ninyi ndie wasambaza hizo fedha katika vikundi mbalimbali…

sasa ikaonekana kwamba tuwatafute hao wanaotajwa kwamba ni watueleze ni kwanini wanafanya hivyo, kwanini wanataka kuharibu amani ya Mtwara na nchi nzima?…ni wale wachache ambao tuliambiwa tufanye uchunguzi tutawaita, wengine bado wapo wahindi hatujawaita, wapo viongozi wa dini hatujawaita tukaona hawa wachache…lakini sio nia ya jeshi kupambana na wananchi wake kwa hiyo naomba mulielewe

Kiongozi huyo wa jeshi alishauri “Tumieni taratibu za kuwakilisha matatizo yenu, lakini njia zinazotumika si sahihi zinaleta vurugu…kule Mkanaledi wakachoma nyumba nne, sisi tupo…kuna baadhi ya watu hapa, Newala na Dare s Salaam na pengine hapa wapo mnafanya uchochezi zaidi….itafika mahali itatushinda, mutapata madhara makubwa , mtakuja kujilaum badae”

Bregedia Jenerali huyo alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya mwenyekiti wa waendesha bodaboda wa eneo la kituo kikuu cha mabasi, Rajabu Majidi kumtaka kiongozi huyo kutoa kauli hatima ya vitendo vinavyodaiwa kufanywa na wanajeshi kwa kuwateka na kuwapiga bakora baadhi ya wananchi.

“wapo ndugu zangu kama watatu hizi walikamatwa na kupigwa bakora na wanajeshi wako, naomba utoe tamko dhidi ya vitendo hivyo” alisema Majidi

Awali Kamanda Sinzumwa aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa wazi kueleza hisisa zao na kwamba hatua atakayechukuliwa hatua kwa kufanya hivyo.

“Mjisikie huru kabisa kuchangia, elezeni hisia zenu…hatua hii inalenga kukuza ufahamu wa sula la gesi wa askari polisi na wadau wetu” alisema Sinzumwa.
Mwisho