VIWANDA 10 VYA KUBANGUA KOROSHO VYAGEUZWA MAGHALA

Maghala yaliyokuwa kiwanda cha korosho mjini Mtwara, kwa sasa maghala hayo yanatumika kuhidadhia mazao yakimilikiwa na kampuni ya CC 2005

Maghala yaliyokuwa kiwanda cha korosho mjini Mtwara, kwa sasa maghala hayo yanatumika kuhidadhia mazao yakimilikiwa na kampuni ya CC 2005

Viwanda 12 vya kubangua Korosho nchini vilivyobinafsishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa hivi sasa havifanyi kazi na vimegeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia mazao.

Uchunguzi uliofanywa na KUSINI umebaini kuwa kati ya viwanda hivyo viwili tu ndiyo vinavyofanya kazi na kwamba baadhi ya maghala ya viwanda hivyo kwa sasa yanatumika kuhifadhia korosho ambapo wakulima hulipia sh. 14 kwa kila kilo inayohifadhiwa na hivyo kuwaingiaiza fedha nyingi.

Kwa mujibu wa mtandao wa http://www.cashewnut-tz.org unaomilikiwa na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) msimu 2012/13 ghala la Newala I katika mnada wake wa Machi, 30, 2012 lilikuwa na kilo 8,488,000 ambazo ziliwaingizia sh. 118,832,000 milioni iwapo kila kilo ililipiwa sh. 14 gharama ya uhifadhi, takwimu hizo zinathibitisha kuwaingizia ukwasi mkubwa wamiliki wa viwanda hivyo vilivyogeuzwa kuwa maghala ndani ya mda mfupi.

Viwanda ambavyo havifanyi kazi ni Mtwara, Newala I, Masasi na Nachingwea. Vingine ni Mtama, Likombe, Lindi, Kibaha, Tanita I na Tanita II. Wakati viwanda vya Newala II na Tunduru vinafanya kazi chini ya uwezo wake kwa kubangua tani 2,000 kila kimoja badala ya tani 10,000.
Taarifa ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ya mwaka 2011/12, iliyotolewa na kaimu mkurugenzi Dome Malosha kwa Kamati ya Usimamizi wa Mashirika ya Umma (POAC) inathibitisha hali hiyo.

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe anasema ni lazima serikali itaifishe viwanda hivyo kwa kuwa hali ya wakulima wa Korosho nchini iko taabani baada ya viwanda vya kubangua zao hilo kubinafsishwa.

Mwenyekiti huyo ameshangazwa na hali ya wakulima wa Korosho jinsi ilivyo mbaya kutokana na viwanda hivyo kutofanya kazi. Pia ameshauri wanaomiliki wanyang’anywe kwa kuwa wamekiuka mikataba ya makubaliano ya mauzo.

“Kwa kuwa viwanda vyote vimeshindwa kazi wanaomiliki sasa hivi wanyang’anywe kwa sababu hali za wakulima wa Korosho ni mbaya na hazionyeshi matumaini,” anasema Zitto.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahmani Kinana akiwahutubia wanachama wa tawi la CCM Novemba, 20, 2012 katika Kijiji cha Mkunwa, wilayani ya Mtwara anasema viwanda ndiyo dawa pekee ya kuhuisha soko la korosho. Kinana alisema hayo baada ya kulalamikiwa na wananchi juu ya kuyumba kwa soko la zao hilo.

“Tumeuza Korosho, lakini ni muda mrefu hatujapata awamu ya pili ya fedha zetu, tunaomba chama kitusaidie,” anasema Hadija Hassan mkulima wa Korosho wa kijiji cha Mkunwa.

Kinana ambaye alibeba taswira ya kuguswa na tatizo hilo anasema, “wamenunua viwanda vyetu, lakini wameshindwa kuviendeleza, ajira zimepotea, wananchi wa Mtwara wanaendelea kuwa maskini.”
Alibainisha kuwa wakati viwanda hivyo vikifanya kazi, kila kimoja kiliweza kuajiri watu wengi, lakini sasa hivi vijana wanakosa kazi kwa sababu viwanda hivyo vimefungwa.

“Ama viwanda hivyo vianze kufanya kazi ama virudishwe serikalini. Nikimaliza ziara hii, nitaandika ripoti kupeleka katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kueleza msimamo wetu na nitasimamia hilo,” alisema Kinana
Anaeleza kuwa maghala ya viwanda hivyo hivi sasa yanahifadhi Korosho ambazo hazijabanguliwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Uchina na India.

Kauli zenye matumaini bila vitendo kutoka kwa viongozi wa serikali na chama kuhakikisha zao la Korosho linapata ufumbuzi wa bei nzuri katika soko ili liwe mkombozi wa wakulima ni chanzo cha kuyumba kwa zao hilo.

Uchunguzi umebaini kuwa licha ya viongozi wa serikali na chama tawala kubaini vyanzo mbalimbali vinavyosababisha kuyumba kwa soko na bei ya zao hilo. Viongozi hao bado wamekuwa wakitoa ahadi za kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo bila ya utekelezaji wowote na kusababisha kufifia kwa maendeleo ya zao hilo.

Pia uchunguzi umebaini kuwa tangu kuanza kutumika kwa mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani katika zao la Korosho mwaka 2007/8 kumekuwapo na mafanikio na changamoto za soko la zao hilo chini ya mfumo huo.

Mafanikio hayo ni pamoja na wakulima kupata uhakika wa Soko na kupanda kwa bei kutoka 300/- ya mwaka 2006 hadi 1,200/- msimu 2012/13, hata hivyo, kumekuwapo na kuyumba kwa soko la zao hilo na kukatisha tamaa kwa wakulima na wakati mwingine kusababisha vurugu.

Mkulima wa Korosho wa kijiji cha Mikangaula wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, Jabil Suleiman anasema inashangaza kuona serikali ikichelea kuwekeza kwenye viwanda vya kubangua Korosho licha ya kujua kuwa viwanda hivyo, ndiyo mwarobaini wa matatizo ya wakulima wa zao hilo.

“Viongozi wa serikali wanatuambia matatizo ya zao la Korosho yataisha pale tutakapoanza kubangua na kuachana na mfumo wa kuuza Korosho ghafi nje, tangu wabaini mbona hakuna utekelezaji?” anahoji Suleiman.

Anaongeza kuwa, “Unajua tatizo la viongozi wetu kila kitu siasa, hawa ni sawa na daktari anayetamba kugundua dawa ya maradhi fulani lakini anapoletwa mgonjwa badala ya kumtibu yeye anapita akijigamba tu bila kutibu, tuwaeleweje?”

Rashid Nammole ni mkulima wa Korosho wa kijiji cha Mwena wilayani Masasi ni miongoni mwa wakulima waliopata kuisikia kauli ya Kinana. Anasema wakulima wa zao hilo wamechoshwa na kauli ambazo zinatia matumaini lakini hazina utekelezaji na kwamba suala la kilimo lisigeuzwe kuwa mtaji wa kisiasa.

“Alikuja Kinana Mtwara, wakulima wakamweleza kilio chao, akasema viwanda vitataifishwa ili vifanye kazi, hadi leo hakuna utekelezaji, hata kiwanda kimoja hakijajengwa hizo ni siasa katikati ya umasikini. Watueleze nini kinafanyika ili kupunguza pengo baina ya kauli na matendo,” anasema Nammole.

Profesa Do DucDinh wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi ya Vietnam alisema katika mkutano wa 17 wa mwaka 2012 kuwa ufufuaji wa viwanda vya kubangua Korosho hukutawanufaisha wakulima wa zao hilo tu. Akizungumza kwenye mkutano wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini Tanzania (Repoa), Profesa huyo aliongeza kuwa wakulima watafaidika kwa kupata bei nzuri na ya uhakika pia Taifa litaweza kusonga mbele kiuchumi.

“Vietnam hatulimi Korosho, lakini tuna viwanda vingi vya kubangua zao hilo, tunategemea malighafi kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania,” anasema Profesa DucDinh.

Profesa huyo anaishangaa Tanzania ambayo inalima Korosho, aliwataka viongozi wake kufanya uchambuzi wa kina, kuhusu kubinafsisha viwanda vya kubangua zao hilo. Jambo ambalo limesababisha hali mbaya kwa zao hilo hivi sasa.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba, Newala, Yusuf Nannila anakiri kuwa kukosekana kwa viwanda vya kubangua Korosho husababisha kuyumba kwa soko la zao hilo.

“Ni kweli Soko linayumba kwa sababu Korosho zote tunauza ghafi, sisi kama Tanecu tumeliona hilo na kwa sasa tumeanza utekelezaji wa ujenzi wa kiwanda cha kubangua korosho wilayani Tandahimba. Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kubangua tani 30,000 kwa siku,” anasema Nanila.

Anaongeza kuwa, “ Tayari ujenzi wa ghala lenye uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 12,000 linajengwa, ifikapo Novemba ujenzi wa kiwanda utaanza, tumepata mkopo kutoka Tanzania Investment Bank. Lengo ni kuwawezesha wakulima kuwa na soko la ndani la Korosho ghafi.”

Mwenyekiti huyo anafafanua kuwa licha ya kiwanda hicho kutoa ajira pia kitafungua soko kwa Korosho zilizobanguliwa kutoka kwa wakulima na hivyo kuongeza hamasa ya wakulima kuuza Korosho zilizobanguliwa.

“Vyama vya msingi vitanunua Korosho ambazo zimebanguliwa kwa kuondolewa maganda ya nje tu, wao watatuuletea sisi. Hivyo, ubanguaji wa Korosho utakuwa umeenea mkoa mzima, tutasafirisha ghafi lakini kwa kiwango kidogo,” anasema Nannila.

Mkurugenzi mpya wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Mkanachapa anasema utekelezaji wa mpango wa kubangua Korosho nchini unatekelezwa kwa kuhamasisha ubanguaji mdogo mdogo pamoja na wawekezaji wakubwa.

“Suala la viwanda vilivyobinafsishwa tuliachie serikali italiangalia, sisi tunaangalia namna ya kutekeleza maazimio mbalimbali likiwemo hilo la kubangua Korosho,” anasema Mkanachapa.

Anaongeza kuwa, “Tutakaa hivi karibuni kikao cha kutathimini zao la Korosho na njia bora ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya soko yanayojitokeza baadae utekelezaji utaanza.”
Mwisho

Advertisements