CHANZO CHA VURUGU ZA WAKULIMA WA KOROSHO CHABAINIKA

t2

t3

pix t2.Watembea kwa miguu wakijaribu kupita eneo lililowekwa magogokuziba barabara kuu itokayo Tandahimba, kwenda Newala katika eneo la kijiji cha Dinduma wilayani Tandahimba wakati wa vurugu za wakulima wa korosho. Picha na Abdallah Bakari

pixt3. Polisi wakiwa katika doria za kudhibiti vurugu za wakulima wa korosho wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara mwka juzi. Picha na Abdallah Bakari

Bei dira, chanzo kuyumba kwa soko, vurugu za wakulima wa korosho
Abdallah Bakari, Mtwara.

Upangaji wa bei dira ya zao la Korosho usiozingatia utaalam ni kiini cha kuyumba kwa bei na soko la korosho mkoani Mtwara na kusababisha vurugu za wakulima wa zao hilo.

Wakulima wanawatuhumu viongozi wa vyama vya ushirka, serikali na chama tawala kuwa wanahujumu bei ya Korosho.

Uchunguzi uliofanywa na KUSINI katika wilaya za Masasi, Tandahimba, Nanyumbu na Newala mkoani Mtwara umebaini kuwa kumekuwa na ongezeko la bei dira katika misimu miwili iliyopita hali inayoyumbisha soko la zao hilo.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa msimu wa ununuzi wa zao hilo 2012/13 na 2011/12 bei dira ilikuwa 1,200, wakati msimu wa 2010/11 na 2009/10 ilishuka na kufikia 850 tu.

Msimu wa 2008/9 bei dira ilikuwa 800 na msimu 2007/8 ambao utaratibu wa Stakabadhi Ghalani ulianza bei dira ilikuwa 700 tu kwa kilo.

Uchunguzi umebaini kuwa tangu bei dira ilipopanda na kufikia 1,200, mwenendo wa soko na bei ya korosho umekuwa wa kuyumba ikilinganishwa na msimu iliyopita. Bei dira ya juu ya misimu ya awali ilifikia 850 kwa kilo ambapo ndipo vurugu za wakulima wa Korosho zilipoanza.

Wakulima wamepokea na kutafsiri kuwa bei dira ndiyo bei ya chini ambayo mazao yao yanapaswa kuyauza kwa wanunuzi.

Tafsiri hiyo imesababisha vurugu za wakulima dhidi ya viongozi wa vyama vya ushirika pindi malipo yanayotolewa yanapokuwa chini ya bei dira.

Hivi karibuni, kuliibuka vurugu za wakulima katika wilaya ya Liwale mkoani Lindi wakipinga kulipwa chini ya bei dira.

Pia vurugu za aina hiyo zimejitokeza mara kadhaa katika wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, msimu 2011/12 na kusababisha uvunjifu wa amani na ubaribifu wa mali za viongozi wanaotuhumiwa kuhusika na hujuma hizo na wakati mwingine wale wa chama tawala.

Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Mnanje wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara, Baraka Mrope anasema chama chake kimeshindwa kulipa bei dira 1,200, badala yake wameweza kulipa 1,115 kwa kilo moja ya korosho.

Anasema hali hiyo ilizua malumbano na wakulima kwa hisia kuwa uongozi wa chama hicho umeiba kiasi cha fedha kilichosalia.

“Tatizo kubwa ni kwamba bei dira inapangwa kisiasa, watu wanaangalia kujizolea sifa za kisiasa kuwa bei mwaka huu ni kubwa, hawangalii mwenendo wa soko na ndiyo maana vurugu zinatokea,” anasema Mrope.

“Mimi nilidhani ingekuwa vizuri suala la bei dira likawa mikononi mwa wataalam badala ya wadau, ili pale matarajio yanaposhindwa kufikiwa basi wawajibishwe, tusiwe kisiasa zaidi, biashara na siasa haviendi pamoja.” alifafanua.

Katibu huyo alikosoa wajumbe wa mkutano wa wadau wanaopanga bei dira kuwa unatawaliwana na wanasiasa na kwamba wanasiasa wanazima sauti za wataalam hali inayosababisha kwenda kinyume na soko.
Mwajuma Nakache ni mkulima wa Korosho wa kijiji hicho anasema “Bora stakabadhi ghalani ifutwe, bei inayopangwa haitufikii, ubabaishaji mwingi”

Diwani wa Viti Maalum wilaya ya Newala, Halima Malolo anasema matatizo ya kuyumba kwa soko kunachangiwa kwa kiwango kikubwa wakulima na wadau wa zao la Korosho kupuuza ushauri wa wataalam wakati wa upagaji bei dira.

“Tatizo sisi wakulima hatukubaliani na ushauri wa wataalam, kwenye mkutano wa wadau wa Korosho wa kupanga bei dira, msimu uliopita wataalam walishauri bei dira iwe 950 lakini tukapinga, tukapanga 1,200,” anabainisha Malolo.

Mkulima wa Korosho wa kijiji cha Mbuyuni, wilayani Masasi, Jafari Mkata anasema kimsingi matatizo ya kuyumba kwa soko katika misimu miwili iliyopita inachangiwa na kupanda kwa bei dira kunakopingana na hali halisi.

“Bei dira inapokuwa kubwa kuliko hali halisi ya soko, wanunuzi hawaingii sokoni, Korosho zinachelwa kuuzwa na kupungua bei, kwa mtindo huu wakulima hawawezi kuwaelewa hivyo kunatokea vurugu,” anasema Mkata.

“Kutokana na bei dira kuwa kubwa hata ushuru wa asilimia tano kwa halmashauri za wilaya unakuwa mkubwa, mfano miaka hii miwili ushuru umekuwa 60 kwa kilo, hayo yote yanamuumiza mkulima anayelipa,” anaongeza.

Mtafiti wa zao la Korosho Kituo cha Utafiti Naliendele, mkoani Mtwara, Dk. Louis Kasuga anaeleza kuwa wataalam hawajapewa fursa ya kusikilizwa wakati wa upangaji wa bei dira ya zao hilo.

“Sisi wataalam tulipendekeza bei dira kwa msimu 2012/13 iwe kati ya 900 au 1,000 lakini wadau walipinga hilo. Sisi tunafikiria mbele lakini si kwa haraka kama wakulima wanavyotaka…kwa bahati mbaya utaalam umeingiliwa na wanasiasa ambao wana nguvu kubwa ya ushawishi,” anafafanua Dk. Kasuga.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mtwara, Masasi (MAMCU), Fikili Makarani anasema ni muhimu kuwa na bei dira ili kutoa taswira halisi ya mwenendo wa soko. Anaongeza ingawa kunahitajika umakini katika uwekaji wa bei hiyo.

“Tulianza vizuri na mfumo huu wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani, mwaka wa kwanza na bei ya 700 msimu 2007/8. Bei ikapanda hadi 800 na 850 kwa msimu uliyofuata na hakukuwa na tatizo. Sasa miaka miwili iliyopita tumepandisha kuliko uhalisia” anasema Makalani.

“Hapa kuna siasa zinazolenga kuwaonesha kuwa wakulima hao watafaidika na zao hilo wakati uhalisia wa bei haupo…kuna umuhimu wa ushauri wa taalam kuzingatiwa, tujenge tabia ya kuaminiana,” anashauri.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Mfaume Mkanachapa anasema wataalam wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukubalika kwa mapendekezo ya bei dira zao, baada ya kufanya utafiti wa bei na kuwasilisha kwenye mkutano wa wadau wa zao hilo.

“Mkutano wa Wadau upo kisheria na ndiyo wenye mamlaka ya kupitisha bei dira, kimsingi kunatakiwa kufanyika kwa tathimini kuona pale bei dira inapokuwa juu zaidi tunapata na kukosa nini? Tunapoweka bei dira kubwa wanunuzi wanapungua sokoni,” anasema Mkanachapa

“Ukiweka beid dira ya chini mfano tulipoweka sh. 800 wanunuzi wengi walijitokeza hatimaye kuliibuka na ushindani na bei ikapanda…leo tumeweka 1200 wanunuzi waliofika wachache ambao wameweza kukaa pamoja na kuyumbisha soko.” anaongeza.

Anafafanua kuwa suala la bei dira ni vema likaangaliwa kiutalaam zaidi sanjari na kuelimishwa kwa wakulima kuwa bei dira sio mkataba bali ni mwelekeo wa bei, hivyo inaweza kupanda au kushuka.

“Kule Pwani hawakuuza kwa Stakabadhi ya Mazao Ghalani, wameuza Korosho zao kwa bei ya 400 hadi 500 wakati bei dira ni 1,200 hapo unaweza kuona mambo yanayovyokwenda,” anabainisha Mkurugenzi huyo.
Mwisho

Advertisements