MAKATO YANAVYOUWAMIZA WAKULIMA WA KOROSHO MTWARA

Wakulima wakiwa ghalani wakisubiri kuuza korosho wilayani tandahimba

Wakulima wakiwa ghalani wakisubiri kuuza korosho wilayani tandahimba

Makato ya shilingi moja kwa kila kilo ya Korosho inayouzwa chini ya mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani kugharamamia kikosi kazi yanaongeza mzigo kwa wakulima wa zao hilo.

Uchunguzi wa KUSINI katika wilaya za Nanyumbu, Masasi, Newala na Tandahimba mkoani Mtwara umebaini kuwa mkulima anatakwa shilingi moja kwa kilo kwa ajili ya kugharamia utendaji kazi wa kikosi hicho.

Kikosi kazi hicho kiliundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara wa zamani, Anatoli Tarimo, kwa ajili ya kusimamia uuzaji wa Korosho kwenye maghala kwa njia ya mnada tangu msimu 2007/8. Msimu huo ndipo ulipoanza kutumika nfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani.

Wakulima wanasema kwa kuwa Kikosi Kazi hicho, hakitambuliwi na sheria namba 10 ya mwaka 2005 ya Stakabadhi ya Mazao Ghalani, hakistahili kunyonya jasho lao.

Wanaongeza kuwa badala yake kinatakiwa kuwepo kwa kuhakikisha mkulima anafaidika na jasho lake.
Kamati hiyo inajumlisha wajumbe kutoka Idara ya Usalama wa Taifa,

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Polisi, Benki ya CRDB na NMB. Wajumbe wengine wanatoka vyama vikuu vya ushirika vya Tanecu na Mamcu, Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) na wenyeviti wa halmashauri za wilaya kwa mwaliko rasmi inaongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara akiwa Mwenyekiti.

Wajumbe kutoka NMB na CRDB wanatokana na mabenki hayo kuwa wakopeshaji wa wakulima fedha za malipo ya kwanza ya bei dira kupitia vyama vya msingi vya ushirika.

“Mimi sina tatizo na kikosi kazi, kama kitajiendesha kwa fedha zao wenyewe, huu mchango wa shilingi kwa kila kilo moja ya Korosho unawaumiza wakulima,” anasema Fikiri Makalani Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Mtwara, Masasi (MAMCU)

Anasema, “Sisemi kusiwepo kikosi kazi kwa sababu kuna mambo magumu yanayojitokeza wakati wa uendeshaji wa mfumo ambayo yanahitaji fikra za pamoja, ila ni vema hii kamati ikagharamiwa kila mmoja na ofisi yake ili hii shilingi moja irudi kwa mkulima.”

Abdul Nchinemba ni mkulima waKorosho wa wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara anasema haungi mkono makato hayo kwa sababu yanazidi kumdidimiza mkulima badala ya kumsaidia.

“Usiangalie shilingi moja kwa kilo ukadhani ni pesa ndogo, mimi msimu uliopita nimeuza tani sita, sawa na kilo 6000, kwa maana hiyo kutoka kwangu wamekata 6,000, sasa zidisha mara tani zilizouzwa kwa mwaka ndani ya mkoa, utaona hawa watu wanachukua fedha nyingi za wakulima bila makubaliano,” anabainisha Nchinemba.

Anaongeza, “Kuwa na dhamira nzuri haimaanishi kuwa umeruhusiwa kutumia jasho la wengine bila ridhaa yao, kama nia ni kumsaidia wakulima basi makato haya yasiwemo. Kamati iwepo, lakini kama lengo lao ni pesa za wakulima basi na kamati yenyewe ife.”

Anasema kwa ujumla gharama za uendeshaji wa mfumo ni kubwa zinazofikia sh. 292.50 kwa kilo ikiwemo shilingi moja ya kikosi kazi.

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Mrina wilayani Masasi, Rashid Mtingala anasema kimsingi kikosi kazi hicho kilibidi kifutwe na kazi zake kuchukuliwa na vyama vikuu vya ushirika.

“Vyama vya msingi vya ushirika vinachukua ushuru wa sh. 21 kwa kilo ambayo haifanyi kazi yeyote. Fedha hiyo ndiyo ilipaswa kuhudumia masoko na sio kukata wakulima fedha zingine,” anasema Mtingala na kuongeza

“Hiki kikosi kazi kilikuwa na umuhimu wakati mfumo mchanga, lakini kwa sasa hakuna haja ya kamati hiyo isiyo na muda wa kwisha.”

Anabanaisha kuwa chama chake kinadaiwa na wakulima tsh.8 milioni baada ya kushindwa kuwalipa wakulima kwa mujibu wa bei dira. Wakulima wengine wamelipwa1,100 badala ya 1200 ya bei dira na kwamba bila ya makato hayo angeweza kupunguza deni hilo kwa sh. 233,000.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika kijiji cha Mahuta wilayani Tandahimba Novemba 2009, aliagiza uongozi wa mkoa na bodi kuangalia namna ya kupunguza gharama za uendehsaji wa mfumo huo. Jambo ambalo linaonekana kutotekelezwa hadi sasa.

Mwenyekiti wa Kikosi Kazi hicho, Yusufu Matumbo anasema kiwango hicho kiliwekwa ili kurahisisha utendaji kazi wa wajumbe wake. Aliongeza kwamba kama wakulima wanaona mahitaji yake hayapo kwa sasa kinaweza kuondolewa.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Mfaume Mkanachapa anakiri kuwa mfumo mzima wa gharama za uendeshaji wa ununuzi na uuzaji wa Korosho umekuwa mkubwa na hivyo kumuumiza mkulima.

“Tutakutana kuangalia mfumo mzima wa gharama za uendeshaji, kuna watu wameweka gharama hapa ambazo si halisia.Wewe umeona hiyo shilingi moja ya kikosi kazi, pia hata kwenye magunia na maeneo mengine kuna kodi, gharama hizo zinamuumiza mkulima,” anasema Mkanachapa.

“Unajua huu mfumo ni mzuri, kuna kasoro ndogo ndogo za kiutendaji. Watu hapo kati walijiingiza na kuweka gharama ambazo tunatakiwa tutathimini upya ili kumpunguzia gharama kwa mkulima, yapo makato yanayowekwa kwa asilimia na mengine kwa kilo.” anasema.
Mwisho

Advertisements