KUKU, NYUKI KUKABILI MABADILIKO YA TABIA NCHI CHAMWINO

1

3 Mkuu wa wilaya ya Chamwino, Fatma Ally

Abdallah Bakari, Chamwino
Njaa imekuwa kikwazo cha maendeleo kwa wakazi 330,543, kati yao wanaume ni 158882 na wanawake 171661 waliojiunga kwenye kaya 69,038 wa wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Kwa mujibu wa wananchi na viongozi wa serikali wilayani humo tatizo hilo linasababishwa na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Wakazi wa wilaya hiyo yenye eneo la kilomita za mraba 8055, zilizogawanyika katika tarafa Tano, kata 32 na vijiji 77 wanasema kilimo cha kutegemea mvua za kudra ya Mwenyezi Mungu sio shughuli ya kutumainiwa tena wilayani humo kutokana na ukame ambao huathiri hata mazao yenye sifa za kustahimili ukame.

“Kilimo kwetu si mkombozi tena, hatuwezi kuishi kwa kutegemea kilimo, kwa sasa tunahitaji kubadili mtazamo wetu ili shughuli zingine ziweze kuziba pengo la kilimo” anasema Saleh Samli mkazi wa Chamwino.

Anasema yeye kama mkulima kwa sasa anafikiria kuwekeza kwenye ufugaji wa nyuki na kuku na kwamba kwa sasa anamiliki mizinga 10 ya asili ya nyuki

“Ninaporina asali nikiuza napata fedha za kununulia chakula, hata hivyo soko la asali limekuwa si la uhakika sana, tunakata ukirina unakwenda kuuza moja kwa moja, si kukaa barabarani kusubiri wateja wa rejareja” anabainisha Smali

Mkuu wa wilaya hiyo Fatma Ally anasema ukame unaoikabili wilaya yake umesababisha wananchi kutojitosheleza kwachakula kila mwaka hali inayoathiri shughuli za kimaendeleo za wananchi.

“Unapokuwa na njaa hata uzalishaji unashuka, huwezi kuzalisha tena, maendeleo yanadidimia…hapa kwetu hata mtama unakauka kwa jua, vyakula vyote inayostahimili ukame hapa huwezi kulima” anaeleza Ally

Anasema serikali yae haijakaa kimya na kwamba ilianza kwa kuhamasisha wananchi wajishughulishe na ufugaji Nyuki ili fedha watakazopata ziweze kutumika kwa kununua chakula na mahitaji mengine ya umuhimu.

“Tumeweza kuongeza mizinga ya asili ya nyuki kufikia 16000 kutoka na 8000 na mizinga ya kisasa 400 kutoka 216 kutoka Januari mwaka huu hadi sasa…kwa kiwango kikubwa tumeweza kuwakomboa wananchi wetu kiuchumi ingawa tuna tatizo la ukosefu wa soko la uhakika” anasema mkuu huyo wa wilaya

Aongeza kuwa “kupitia ufugaji nyuki tumeweza kuanzisha vyama Tisa vya ushirika vya ufugaji nyuki, hii ni sehemu ya kukabiliana na tatizo la ukosefu wa soko la uhakika, pia kupitia ushirika huu tumetengeneza mtandao wakuongeza thamani mazao ya asali”

Akizungumzia ufugaji bora wa kuku wa kisasa kwa lengo lakibiashara ili waweze kuongeza kipato kwa wananchi na kuziba pengo la uhaba wa chakula unaosababishwa na ukame ikiwa ni athari ya mabadiliko ya tabia nchi, Fatma anasema

“Kwa sasa tumezindua mpango rasmi ufugaji kuku kibiashara katika wilaya yangu ya Chamwino… nataka kuku watumike kukabilianana athari za mabadiliko ya tabia nchi, wananchi wakipata fedha wataweza kununua chakula kwa ajili ya familia zao”

Anafafanua kuwa “Wananchi watafuga kuku kibiashara, ni ufugaji wa kisasa wa kuku wa asili, leo hii ukiwa na kuku mmoja unahakika ya kupata sh. 10,000 hivyo basi ukiwa na kuku 10 unaweza kununua chakula na mahitaji mengine”
Anasema katika kukabiliana na ukosefu wa soko wilaya yake imeandaa mtandao wa kuongeza thamani hadi kuku wanapofika sokoni kwa kuwakutanisha wafugaji na walaji.

“Tumeunda chama kimoja cha ushirika wa wafugaji kuku chenye wanachama wasiopungua 200 , hii ni baada ya kukutanisha viongozi, mabenki, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGO’S) wakulima, wafugaji, wenye maduka, mama Nitilie, wenye mabucha, wachuuzi kuku, wenye hoteli, wenye machine za kusaga na kukamua mafuta na wataalamu wa mifugo…
lengo shughuli zote ndani ya mnyororo wa thamani wa kuku zifanywe na wana-Chamwino, ili shughuli za kundi moja zitoe fursa kwa kundi lingine kufaidika nazo, kwa kufanya hivyo mzunguko wa fedha ndani ya wananchi utakuwa mkubwa”

Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Adrian Jungu anasema tayari halmshauri yake imenunua majogoo 340 wa kisasa na wamepelekwa kwa wafugaji wilayani humo ili kuhamasisha ufugaji bora wa kuku wa asili.

“Hadi sasa wilaya inakadriwa kuwa na kuku 350,000 hata hiyo kuku hao ni wachache, tunaweza kuzalisha zaidi na kuwa mkombozi wa kipato cha wananchi wetu ambao wanalazimika kutojitosheleza kwa chakula kutokana na ukame” alisema Jungu na kufafanua kuwa

“Ili kurahisisha ufugaji huo, wananchi tunawahamasisha wajiunge kwenye vikundi mbalimbali, tunataka viwepo vikundi vya utengenezaji chakula cha kuku, kutotolesha vifaranga, kutibu magonjwa na vya masoko…tunaamini kuwa tukifanya hivyo tutaweza kuwakomboa wananchi wetu, tunataka kila kaya ifuge kuku”
Doris Kavindi ni ofisa tarafa ya Chilomwa wilayani humo anasema wananchi katika tarafa yake wameanza kufaidika na mradi huo wa ufugaji kukukwa kujiunga katika vikundi na kuendesha shughuli za ufugaji

“Mwitikio wa wananchi wa tarafa yanguni mzuri, wananchi wengi mbali ya wale waliojiunga kwenye vikundi kila mmoja anafuga kuku na wanaonesha kufaidika na mpango huo kwa sababu utawawezesha kumudu mahitaji muhimu pindi wanapowauza” alisema Kavindi

Naye ofisa mifugo wa wilaya hiyo, Richmond Urasa anabainisha kuwa ufugaji kuku unakabiliwa na changamoto kubwa ya magonjwa ya Kideli na Ndui na kwamba licha ya kutumia dawa kutibu na kuchanja usafi wa banda unaweza kukinga dhidi ya magonjwa hayo.

“Kuku ni moja ya mifugo ambayo ina gharama nafuu kufuga na inaweza kukuingizia kipato kikubwa sana iwapo utafuta kanununi za ufugaji bora wake, ugonjwa wa Kideli na Ndui yanadhibitika kwa kutibu, kuchanja na usafi wa banda unaweza kukinga dhidi ya maradhi hayo” anasema Urasa

Mwisho

Advertisements