NANYAMBA WAELIMISHWA UTAWALA BORA

DIWANI wa kata ya Nanyamba Hassan Mauji akisisitiza jambo wakati akimkaribisha makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Hamisi Fundi kufungua mafunzo ya utawala bora kwa wenyeviti wa vijiji, madiwani na maafisa watendaji wa kata katika tarafa ya Nanyamba halmashauri ya wilaya ya Mtwara

DIWANI wa kata ya Nanyamba Hassan Mauji akisisitiza jambo wakati akimkaribisha makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Hamisi Fundi kufungua mafunzo ya utawala bora kwa wenyeviti wa vijiji, madiwani na maafisa watendaji wa kata katika tarafa ya Nanyamba halmashauri ya wilaya ya Mtwara

Na Ripota wa Kusini, Nanyamba
WENYEVITI wa vijiji, maafisa watendaji wa vijiji na kata, na madiwani wa tarafa ya Nanyamba wilaya ya Mtwara mkoani hapa, wamepatiwa mafunzo ya stadi za utawalabora ili waweze kutekeleza majukumu yao vema.
Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yameanza juzi yanakamilika leo JUMATANO katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya tarafa ya Nanyamba, ambapo mwenzeshaji mkuu ni afisa tarafa ya Ziwani, Francis Mkuti, na yanaendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Saidia jamii kuishi SAJAKU.

Akifungua mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na The Foundation for civil society, makamu wa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Hamisi Fundi aliwakumbusha wenyeviti wa vijiji juu ya umuhimu wa kuitisha vikao na mikutano mikuu ya vijiji ili kutekeleza dhana ya utawala bora.

Fundi alisema kuwa kutoitisha mikutano ni ukikwaji mkubwa wa utawala bora hivyo ni vema kila kiongozi akatimiza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuitisha mikutano na vikao muhimu vya kisheria.

“Kimsingi hili jambo limekuwa ni tatizo kubwa wilayani kwetu, tumeshuhudia wananchi wakiwatimuwa viongozi wao kwa madai ya kutoitisha mikutano sasa hili si jambo jema…utakuta kuna kijiji hakijafanya mkutano kwa miaka miwili huu ni ukiukwaji mkubwa wa utawalabora”, alisema Fundi.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo katibu mtendaji wa SAJAKU Nashiri Pontiya, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo viongozi na wananchi katika kutekeleza dhana ya utawala bora na kujenga mahusiano bora ya kiutendaji kati ya watendaji na viongozi wa kuchaguliwa.

“Mwisho wa mradi huu tunataka tuone wananchi wakihudhuria katika mikutano huku viongozi nao wakitimiza wajibu wao kwa kuitisha mikutano kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo”, alisema Pontiya ambaye pia ni mratibu wa mradi huo.

Advertisements