UVCCM na korosho Mtwara

Chilumba

UVCCM WAICHONGEA BODI YA KOROSHO KWA JK

UMOJA wa Vijana Mkoa wa Mtwara UVCCM, umemuomba Rais Jakaya Kikwete kutumia madaraka aliyonayo kuvunja bodi ya korosho iliyopo madarakani mara moja kwa madai kuwa ndio kikwazo na chanzo migogoro na unyonyaji kwa wakulima wa zao hilo mkoani humo.

Umoja huo pia limeitaka bodi ya korosho kuondoa matangazo yake waliyoyaita ya kinyonyaji ndani ya siku saba, na kwamba hayo yasipotekelezwa wataitisha maandamano kupinga kuendelea kuwapo kwa bodi madarakani lakini pia kuwapo kwa matangazo hayo.

Akiongea mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza la vijana mkoa kilichoketi juzi katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka ya bandari mjini hapa, mwenyekiti wa uvccm mkoa, Nestory Chilumba, alisema kuwa baraza limefikia hatua hiyo baada ya kujiridha kuwa bodi ndio kikwazo cha maendeleo ya wakulima wa korosho.

Chilumba alisema kuwa wamefikia hatua ya kumuomba Raisi kuivunja bodi hiyo kwa kuwa ndio mwenye madaraka hayo, lakini wameiagiza bodi kuondo matangazo yake yaliyobandikwa katika mbao za matangazo za vyama vya ushirika na kupigwa muhiri wa bodi, matangazo ambayo yanaonesha wazi kumzurumu mkulima.

“Tangazo la bodi linapingana na makubaliano ya kikao cha wadau wakorosho kilichofanyika kule Dodoma Septemba 31 kilichopanga bei dira kuwa Sh.1,000…wao wameweka matangazo yanayoonesha mkulima atalipwa 600 katika awamu ya kwanza lakini haijulikani inayobaki analipwaje…lakini cha kushangaza zaidi nyuma ya risiti wanazotoa mkulima anapofikisha korosho zake gharani bodi imesema malipo yaliyobaki ni majaaliwa na kugonga muhuri wake sasa huu kama si wizi tuite nini”, alisema Chilumba.

Alisema kuwa huo ni unyonyaji kwani kuna ushahidikuwa kabla ya bodi iliyopo madarakani kipindi cha Waziri Stephen Wasira akiwa na dhamana ya kilimo, bei ya korosho ilifika mpaka 1,800 lakini sasa hata hiyo waliyokubaliana wadau shi 1000 inakuwa utata mtupu jambo ambalo walisema hawawezi kukubali kuliacha likiendelea.

“Minada ya korosho siyo mali ya bodi ya Korosho wala vyama vikuu bali ni mali ya wakulima hivyo iwe wazi kwa wakulima…lakini utaona sasa kila kitu ni siri mkulima ambaye ni muhusika mkuu katika mfumo huu wa stakabadhigharani hajui kitu kwanini iwe hivi jamani ifike mahali suala hili lifike mwisho tumechoka kusikia kila mwaka wakulima wakilia na kujuta kwa makosa ya wengine imetosha waondoke”, alisema Chiluma akiwa ameongozana na wajume wengune wa baraza hilo.

Alisema kwa kauli moja wajumbe wa Baraza wamekubaliana kuwa bodi ya korosho ndani ya siku saba kuanzia kesho( Jana Jumatatu) itoe tangazo lake lililobandikwa kwenye vyama vya msingi vinginevyo siku ya nane UVCCM Mkoa wa Mtwara tutaitisha maandamano kulia na wakulima juu ya suala zima la korosho na tutaomba wakulima Lindi, Ruvuma na Mkoa wa Pwani kutuunga mkono.

Alibainisha kuwa pia baraza hilo pia linawaomba wajumbe wa bodi ndani ya siku saba hizo wajipime ili kumpunguzia Rais Kazi kabla hajafanya maamuzi ambayo wamemwomba kuyafanya ambayo ni kuivunja bodi hiyo.

“ Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM kuwa hatuna imani na bodi ya korosho iliyopo kwa sasa kwa nafasi aliyo nayo na mamlaka yake tunamwomba avunje bodi ya korosho iliyopo sisi vijana tumeona hawana mwelekeo wa kusaidia wakulima,”alisema Chilumba.

Aidha baraza hilo limeshangazwa na mikutano ya wadau wa korosho kufanyika Dodoma na Morogoro na kwamba kitendo hicho kinawanyima fursa wadau wa kurosho ambao ni wakulima wenyewe kushindwa kushiriki ingawa Mtwara inazalisha karibu asilimia themanini.

“Mikutano ya wadau wa korosho ni vyema ikafanyika mikoa yenye uzalishaji mkubwa ili kuwe na uwakilishi wa kutosha na uchangiaji uwe na manufaa kwa wahusika ambao ni wakulima, mfano Mtwara inazalisha karibu asilimia themanini kwani haijapewa nafasi ya kuhodhi mkutano tena hiyo itasaidia wengine kujifunza ni kwa namna gani tumefanikiwa kuwa wakulima wakubwa hivi,” alisema Chilumba.

Mwisho.