PELEKENI WATOTO SHULE

KATIBU wa itikadi siasa na uenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Tandahimba akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na wananchi katika mkutano wa hadhara kijiji cha Lubangala.

KATIBU wa itikadi siasa na uenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Tandahimba akisisitiza jambo alipokuwa anaongea na wananchi katika mkutano wa hadhara kijiji cha Lubangala.


WAKAZI wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, wamehimizwa kuzingatia elimu ya watoto wao kwa kuwapeleka shule vijana wote waliochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari mwaka huu.
wito huo umetolewa kwa nyakati tofauti na katibu siasa itikadi na uenezi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Tandahimba, Ibrahimu Ndolya, alipokuwa anawahutubia wakazi wa vijiji vya Nakayaka, Bilikani, Mahuta,Chikongola na Lubangala, alipokua katika ziara ya mbunge wa Tandahimba Juma Njwayo.
Ndolya alisema kuwa kwakuwa vijana wengi mwaka huu wamefaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari ni vema wazazi wakawapeleka watoto wao kwa wakati ili waweze kupata elimu hiyo muhimu itakayojenga maisha yao ya baadae.
“Nataka nichukue fursa hii kukupongezeni kwa wilaya yeu kuongoza kimkoa kwa kufaulisha watoto wengi mwaka jana…lakini hiyo haitakuwa na maana kama hatutawapeleka sekondari kwa visingizio vya kukosa fedha kwaajili ya kuwanunulia mahitaji muhimu”, alisema Ndolya.
Kiongozi alisema kuwa inashangaza kuona wazazi wanatumia fedha nyingi kwaajili ya mambo ya jando na unyago huku wakishindwa kuwapatia mahitaji muhimu kwaajili ya elimu ya watoto wao wakidai eti hawana fedha.
“Sisemi tuachane na mambo ya jando na unyago hapana hii ni mila yetu na inapaswa kuendelezwa lakini ebu tuangalie fedha na rasilimali nyingine zinavyotumika kwaajili hii…kama tunavyoweka bajeti ya unyago basi na elimu iwe hivyo pia maana elimu ndio urithi bora kwa watoto wetu”, alisema Ndolya.
Aidha Ndolya alisema kuwa kuwapeleka tu shule watoto haitoshi badala yake wazazi wawe wanafuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao na kuwa karibu na walimu na kuwapa ushirikiano kwani wazazi ndio wenye jukumu kubwa la kuhakikisha mtoto anapata elimu bora.
Aliwataka kuwapuuza wanaobeza shule za kata kwa madai eti hazina walimu wala miundombinu na ndio maana mawaziri watoto wao hawasomi huku, na kuwahimiza kuwapeleka na kufuatilia maendeleo yao kwani kuna ushahidi wa kutosha waliofanya hivyo watoto wao wamefanya vizuri licha ya kusoma katika shule hizo.
“Kuna mambo mengine jamani tujipe nafasi ya kujiuliza si kila jambo unaloambiwa unalikubali tu, hivi mtu anpokwambia hizi shule sio nzuri ndio maana watoto wa mawaziri hawasomi huko jiulize hapa Lubangala kuna waziri gani hata mwanawe asome pale…lengo la serikali ni zuri ni kuhakikisha kila mtu anapata elimu”, alisema Ndolya.
Wilaya ya Tandahimba imeongoza kimkoa kwa kushika nafasi ya kwanza kwa ufulu wa wastani wa alama 111.08, ikifuatiwa na Mtwara vijijini(105.12), huku nafasi ya tatu ikishikwa na Manspaa ya Mtwara Mikindani (103.17), ya nne Halmashauri ya mji wa Masasi (96.87), ya tano,Halmashauri ya wilaya ya Masasi (95.27),Newala imekuwa ya sita (94.98) huku Nanyumbu ikishika mkia kwa kupata wastani wa 92.22 kati ya wastani wa alama 250.
Mwisho.

Advertisements