Wanawake Mtwara watakiwa kuchangamkia fursa

WANAWAKE mkoani Mtwara wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza kutokana na ujio wa makampuni mengi ya uwekezaji yanayokuja mkoani humu kuwekeza katika sekta ya gesi na mafuta.
Wito huo umetolewa jana na mwenyekiti wa muda wa taasisi ya wanawake wajasiriamali Tanzania (TAWEI), Emma Kawawa, alipokuwa anafungua mafunzo ya siku tatu ya ujasiriamali kwa wakinamama mkoani humu.
Kawawa alisema kuwa imekuwa ni desturi kwa wananwake wengi mkoani humo kuona kama shughuli za kiuchumi zinawahusu wanaume pekeyao na wao kukaa nyuma wakisubiri kuletewa na waume zao jambo ambalo alisema limepitwa na wakati na linafaa kuachwa mara moja.
“Wakinamama wenzangu naomba sana ebu tubadilike na tuende nambadiliko ya kidunia ambapo sasa wananwake ndio tunaotakiwa kushikilia uchumi na sio kuwaachia wanaume pekeyao kwani sisi tunanafasi kubwa zaidi ya kuendelea kiuchumi kuliko wao”, alisema Kawawa.
“Wanawake wenzangu ni vizuri tuchangamkie fursa zinajitokeza kwa sasa na kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali ili kujiongezea kipato kwa kuwa makampuni mengi yanakuja kuwekeza Mtwara …si kila kitu Kitoke Dar es Salaam, hata sisi tunaweza kufanya” alisema Emma ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya uwekezaji ya Entango.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo walipoanza waliwaelimisha wanawake ambao kwa kiwango kikubwa wamefuata maelekezo na hadi sasa wamepata wanachama 560 kutoka wilaya zote za mkoa wa Mtwara na sasa wanajikita katika kusaka wanachama zaidi katika mkoa wa Lindi.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa walifikia uamuzi kuanzisha taasisi hiyo baada ya kufanya utafiti na kujiridhisha kuwa wakinamama wengi wanania ya kufanya shughuli za kiujasiriamali lakini wanakosa mitaji, elimu ya biashara na kutiwa msukumo na moyo wa kujituma zaidi na ndio kazi itakayofanywa na taaisisi hiyo.
Aidha mwenyekiti huyo wa muda wa Taasisi ya wanawake wajasiriamali Tanzania(TAWEI), Emma Kawawa, alisema uzinduzi wa taasisi hiyo utafanyika Mei 31 mjini hapa ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa mke wa makamu wa raisi mama Asha Bilal.

OLYMPUS DIGITAL CAMERA