OLYMPUS DIGITAL CAMERA
MSIKUBALI KUTUMIKA
MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali wilayani Newela Mkoa wa Mtwara yameaswa kutojihusisha na jambo lolote lenye taswira ya kuleta uvunjifu wa amani kwa kuchukua fedha za misaada kutoka mashirika ya kimataifa ambayo baadhi yao yanalengo la kuvuruga amani ya nchi iliyopo.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya ya hiyo,Christopher Magalla alipokuwa akifungua mdahalo wa mchakato wa katiba uliyondaliwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mtwara(MRENGO) kwa ufadhiri wa The foundation for sivil society ambao umefanika katika kijiji cha Mkunya.
Alisema mashirika yasio ya kiserikali ni vema wasikubali kutumiwa au kutumika vibaya na kuwa sehemu ya chanzo cha kuchochea vurugu ama ghasia katika maeneo yao kwa lengo la kupinga shughuli za serikali ambazo zinalenga kuleta maendeleo kwa makundi yote wilayani humo.
Magalla alisema wapo baadhi ya watu wasioitakia mema nchi ya Tanzania ambao wamekuwa wakiwashawishi viongozi wa mashirika hayo kupingana na mambo mbalimbali yanayofanywa na serikali kwa njia zisizo sahihi kama kuhamasisha maandamano na vurugu hivyoni vema sasa mashirika hayo yakajitambua na kujiweka mbali na wafadhili wa aina hiyo.
“Nyinyi watu wa asasi za kiraia ndio nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yetu na kuimarisha amani yetu ni vema mkajitambua na kujitenga na watu hao wasio itakia mema nchi yetu…badala yake mjikite katika shughuli za kuelimisha jamii katika masuala ya kiuchumi, masuala ya mchakato wa katiba na serikali ipo tayari kutoa kila aina ya msaada ili malengo yenu yatimie”, alisema mkuu huyo wa wilaya.
Aliongeza kuwa mchakato wa kuandika katiba mpya unakwenda vizuri na kwa kuzingatia matakwa ya sheria iliyotungwa kwa ajili ya kusimamia upatikanaji wa katiba mpya, pia ulizingatia maoni ya makundi na taasisi mbalimbali licha ya taasisi zingine kutaka maoni yao yawe bora kuliko mengine.
“Katiba hii si ya CCM,CHADEMA ,CUF wala siyo ya mtu yoyote yule ni katiba ya watanzania wote bila kuangalia rangi,kabila, dini na wala jinsia ni vema sote tukashiriki katika kila hatua inayotuhusu…sasa tupo katika hatua ya bunge la katiba lakini itafika siku tutatakiwa kupiga kura za maoni kuikataa au kuikubali sasa elimu hii leo ni muhimu sana kwa jamii,” Alisema Magalala.
Aidha mkuu huyo wa wilaya aliupongeza mtandao huo kwa kuandaa midahalo yenye tija na ambayo ikitumiwa vizuri na wananchi inaweza kuwa chachu kwa wananchi kushiriki vema katika hatua ya mwisho ya upigaji kura ambayo ndio hatua ya mwisho.
Mwisho.

Advertisements