MRENGO YAIKUNA SERIKALI

OLYMPUS DIGITAL CAMERAMRENGO NA WADAU

ASASI zisizo za kiserikali mkoani Mtwara zimetakiwa kuiga mfano wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani humu MRENGO kuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira, na kujiandaa na uchumi mkubwa unaotazamiwa kutokana na kuwapo kwa rasilimali ya gesi asilia.

Wito huo umetolewa na afisa maendeleo ya jamii wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Mwajuma Nyoni, alipokuwa anafungua warsha ya siku tatu ya kwa viongozi wa ngazi mbalimbali juu ya ushiriki wa jamii katika tasnia ya uziduaji wa gesi asilia na mafuta iliyoandaliwa na mrengo.
Nyoni alisema kuwa kitendo cha Mrengo kuwajengea uwezi ama ufahamu viongozi hao kuhusu masuala ya gesi asilia ni kitendo kinachotakiwa kuigwa na wadau wengine ambapo alisema ni wajibu wa kila mdau kutimiza wajibu wake ipasavyo na sio kuisubiri serikali pekee.

Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa Chama cha walimu(CWT), iliyoandaliwa na Mtandao wa mashirika yasiyo ya Kiserikali mkoa wa Mtwara(MRENGO) na kufadhiriwa na Mfuko wa hifadhi wa mazingira duniani (WWF), na iliwakutanisha Viongozi wa vyama vya siasa na serikali, viongozi wa dini, Asasi za Kiraia, waandishi habari, Wenyeviti wa Mitaa,Watendaji wa vijiji, madiwani na Maofisa Tarafa.

“Kuwepo kwa makundi haya ya washiriki katika warsha hii kumenipa faraja kubwa sana maana nina uhakika kuwa elimu hii itakayotolewa hapa itawafikia walengwa kwa haraka na bila upotoshaji wa maudhui halisi ya mafunzo haya, ni lazima taarifa sahihi ziwafikie wananchi tena kwa wakati”, alisema Nyoni.

Mama Nyoni alisema kuwa ni nia ya serikali kuona kila mwananchi popote alipo anapata taarifa zote muhimu juu ya maendeleo ya mradi wa gesi asilia na namna atakavyonufaika baada ya mradi kukamilika lakini pia wanapaswa kujua wajibu wao juu ya nini wanatakiwa kufanya katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

“Pamoja na haya yote lakini yatupasa kujua historia ya utafutaji wa gesi asilia, ugunduzi, uchimbaji, usambazaji, uuzaji na hatimaye namna ya kusimamia maduhuri yatokanayo na mauzo hayo pamoja na masuala ya sera ya taifa yahusuyo gesi asilia na sheria zake ni muhimu watu wakayajua ili wakaweza kufahamu na kuyajadili…sasa haya yote sio jukumu la serikali pekee kuelimisha umma na wengine muige”, alisema Nyoni.

Akiwasilisha mada mhadhiri wa chuo kikuu cha STELAMARIS. Prof. Aidam Msafiri, alisema kuwa ni muhimu kwa kila mmoja kutambua na kuzingatia kuwa gesi hiyo ni tunu iliyoletwa na mungu na hivyo kushiriki katika kuitumia kwa kuzingatia matakwa ya jamii yote na sio kubaguana huku wale walio na mamlaka la kiutendaji serikalini wakizingatia maadili ya utendaji ili kuwezesha watu wote kunufaika.

Naye mweka hazina wa MRENGO. Mustafa Kuyunga alisema kuwa lengo la kuandaa warsha hizo ni kuwajengea uelewa watu wote katika jamii ili kuwaweka tayari kukabiliana na changamoto zinazotokana na uziduaji wa gesi ikiwa ni pamoja na uhalibifu wa mazingira na kwamba baada ya warsha hiyo wataendesha midahalo vijijini kwa lengo hilo hilo.
Mwisho.

Advertisements