NANYAMBA NA UTAWALABORA

NANYAMBA NA UTAWALA BORA
KUTOKUWAPO kwa uadilifu miongoni mwa watendaji wa vijji,uelewa mdogo wa wananchi juu ya masuala ya utawala na wanasiasa kutoshiriki katika kuhamasisha jamii kuhudhuria katika mikutano ya vijiji ni miongoni mwa mambo ambayo yanafanya dhana ya utawala bora kutofikiwa.
Hayo yameelezwa juzi na wakazi wa kata ya Nanyamba wilaya na mkoa wa Mtwara, awalipokuwa wakichangia mada katika mdahalo wa utawala bora na uwajibikaji uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya ya kata ambapo zaidi ya wakazi 250 walihudhuria na kutoa maoni yao.
Akichangia mada katika mdahalo huo Mohamedi Mwalimu mkazi wa kijiji cha Namkuku, alisema kuwa wananchi wengi vijijini hawana uwelewa wa kutosha juu ya umuhimu wa mikutano ya vjiji au vitongoji jambo ambalo linafanya washindwe kuhudhuria hata pale viongozi wanapoitisha mikutano hiyo.
“Ninachokiona mimi ni kwamba tuliowengi hatujui umuhimu wa mikutano hii ninaaamini kama wote tungefikiwa na elimu hii tuliyoipata leo juu ya umuhimu wa mikutano tungekuwa mstari wa mbele kuhimizana kushiriki katika mikutano”, alisema Mwalimu.
Shamte Ahamadi mkazi wa kijiji cha Dinyecha alisema kuwa kutokuwapo kwa uaminifu kwa baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji ni sababu ya wananchi kuamua kususia mikutano ya vijiji au vitongoji na kwamba elimu inapaswa kutolewa kwao na watendaji wawajibishwe pale inapobainika kutumia rasilimali za umma kinyume cha utaratibu.
“Utakuta wananchi wanakwenda katika mkutano lakini inapofika ajenda ya kusomewa mapato na matumizi mizingwe inaanza na hapo vurugu zinatokea na kwasababu hiyo wananchi wanaona haina haja ya kushiriki katika mikutano hiyo ingawa inaumuihmu mkubwa kwa maendeleo yao na utekelezwaji wa dhana ya utawala bora”, alisema Shamte.
Hadija Lyangunde makazi wa kijiji cha Nanyamba, anasema kuwa kutoshiriki kwa wanasiasa katika kuhamasisha wananchi kwenda kwenye mikutano ya vijiji na vitongoji ni moja kati ya sababu zinazochangia wananchi kutohudhuria katika mikutano hiyo.
Lyangunde alisema kuwa iwapo wanasiasa watashiriki vema na kutimiza wajibu wao wa kuahamasisha wananchi mahudhurio katika mikutano hiyo yatakuwa mazuri na kasi ya maendeleo vijijini itaongezeka na hivyo ile dhana ya utawalabora kukamilika.
Akitoa mada katika mdahalo huo ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Saidia jamii kuishi SAJAKU, Said Swallah, alisema kuwa kutekelezwa kwa dhana ya utwalabora kunakamilika kwa viongozi kuitisha mikutano na wananchi kushiriki ipasavyo.
Swallah alisema kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana mahali ambapo utawalabora hatutekelezwi, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kulingana na majuku aliyonayo ya kiutekelezaji katika kutimiza dhana ya utawalabora.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofadhiliwa naThe foundation for civicil sociaty, Diwani wa kata ya Nanyamba, Hassan Mauji aliwakumbusha wenyeviti wa vijiji juu ya umuhimu wa kuitisha vikao na mikutano mikuu ya vijiji na kuweka mikutasari ambayo itafikishwa katika vikao vya kamati ya maendeleo ya kata ili kuwezesha mipango ya vijiji kutekelezwa na halamashauri ya wilaya.
Mauji alisema kuwa kutoitisha mikutano si tu ni ukikwaji mkubwa wa utawala bora lakini pia kunachelewesha maendeleo ya wananchi katika eneo husika maana kunakuwa hakuna mipango ya maendeleo inayopangwa kwa pamoja jambo ambalo linapaswa kurekebishwa.
“Kimsingi hili jambo limekuwa ni tatizo kubwa katani kwetu, tumeshuhudia wananchi wakiwatimuwa viongozi wao kwa madai ya kutoitisha mikutano sasa hili si jambo jema…nimekuwa nikiendesha mikutano ya kamati ya maendeleo ya kata mimi kama mwenyekiti wa kamati hiyo lakini utakuta kijiji hakina muktasari hii maanayake ni kwamba hawajafanya mkutano.alisema Mauji.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo katibu mtendaji wa SAJAKU Nashiri Pontiya, alisema kuwa lengo la mdahalo huo kuibua mijadala juu ya dhana ya utawalabora baada ya kuendesha mafunzo kwa makundi yote katika jamii ikiwa ni pamoja na viongozi wa vijiji, watendaji na wananchi wa kawaida.

Advertisements