OLYMPUS DIGITAL CAMERA

WATOTO WANAOTUMIKISHWA

 

JAMII ya wakazi wa mkoa wa Mtwara wenye uwezo kiuchumi wameaswa kujenga tabia ya kujitolea kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ili kuwawezesha kuishi maisha mazuri hapo baadae badala ya kuwatumikisha katika shughuli zao wakiwa na umri mdogo.

 

Wito huo umetolewa jana na katibu mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Faidika Wote Pamoja (Fawopa-Tanzania), Baltazar komba, alipokuwa anaongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufunga mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

 

“Watu wenye uwezo kiuchumi au hata wale wenye nafuu kidogo ni vema wakawasaidia hawa watoto na sio kuwatumisha kwa kigezo cha kuwa wao ni masikini…hii inaweza kuwa mbaya zaidi baadae maana watoto hawa watakuwa wakijua kuwa walinyanyaswa na hao wenye uwezo na pia wanaweza kuwa na tabia mbaya za wizi na ukabaji hata wakiwa wakubwa”, alionya Komba.

 

Mafunzo hayo yaliyoendeshwa na Fawopa kwa ufadhili wa Serikali ya Uholanzi chini ya usimamizi wa Shirika la Maendeleo la nchi hiyo la Terre Des Hommes, yamehusisha watoto 200 wanaotumikishwa majumbani, katika biashara na maeneo mengine mkoani Mtwara na yamefanyika katika ukumbi wa ofisi ya kata ya Vigaeni manspaa ya Mtwara Mikindani.

 

Komba, ambaye pia ni mratibu wa mradi huo, huo unaojulikana kama ‘Tuwalee watoto Mtwara (Tuwam)’, unashirikisha watoto kutoka kata za Vigaeni na Reli na vijiji vya Msijute, Mayanga na Likonde pia maeneo ya Soko kuu la Mtwara na Maghalani.

 

“Hawa watoto wanaolengwa katika huu mradi ni kuanzia miaka 12 hadi 17 na lengo kuu la mradi huu ni kuwaokoa watoto 200 kutoka maeneo ya soko kuu, baa, mamalishe na stendi kuu na kuwarudisha watoto 80 katika shule za msingi na sekondari kwa kuwapatia mahitaji yote,”alisema.

 

Mratibu huyo aliongeza kuwa; watawaandikisha watoto 120 katika vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi na kuwapatia vitendeakazi mara baada ya kuhitimu mafunzo yao ili waweze kujitegemea.

 

“Mradi huu una lengo la kuwafikia watoto wanotumikishwa kwa kufanyishwa kazi mbalimbali za kuajiriwa ama kujiajiri …unajua Mtwara sasa uchumi wake unakuwa kwa kasi na watu wengi wanatumia fursa hiyo kufanya shughuli za kuzalisha kipato na wanatumia watoto ili kupata nafuu ya malipo sasa hii sio sawa.

 

Aidha Komba alisema kuwa baada ya mradi huyo shirika lake litatoa kiasi cha shilingi milioni 20 kwa wazazi wanakotoka watoto hao baada ya kuwapatia mafunzo na kuwaunganisha katika vikundi ili waweze kuwa na shughuli za kuzalisha kipato na kuweza luwalea watoto wao vema.

 

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi kwa niaba ya watoto wenzao,Juma Namwamba kutoka Railway na Kudra Saidi wa mtaa wa soko kuu, walisema kuwa mafunzo hayo ni ukombozi kwao na wanategemea kuishi maisha tofauti hapo baadae kwani mambo waliojifunza ni muhimu kwa makuzi yao.

 

Nae mwalimu wa mafunzo hayo Clemence Mwombeki, alisema kuwa miongoni mwa mambo waliofundishwa watoto hao ni pamoja na stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi na kuwajenga kisaikolojia ili waweze kukabiliana hali taofauti ya maisha watakayoishi baadae.

 

Mwisho.

Advertisements