CHANGAMKIENI FURSA

OLYMPUS DIGITAL CAMERA

VIJANA Mkoani hapa wametakiwa luchangamkia fursa ya ujasiriamali inayoletwa na Shirika la utafutaji wa gesi la Statoil kwa kuandika wazo la biashara na kushindanishwa ili kupata moja litakaloweza kupatiwa mtaji. Wito huo umetolewa na katibu tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda katika siku ya uzinduzi wa shindano hilo pamoja na ufunguzi rasmi wa chumba cha kompyuta cha mashujaa wa kesho kitakachotumika kuwafundishia vijana elimu ya kuandika mpango wa biashara na ujasiriamali,uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Stella Maris Mtwara. Alisema kuwa mpango huo ni mzuri ambapo unatoa fursa kuwaandaa vijana katika kujielekea katika uchumi mkubwa wa gesi na mafuta katika Mkoa huo ifikapo mwaka 2022 wakati mashirika na kampuni za gesi zitakapokuwa zinahitaji huduma mbalimbali za kijamii. “Ninawashukuru hawa watu wa Statoil kwa kutoa fursa hii nzuri kwa vijana kwani itawafanya kujijenga kifikra ili kuweza kuukabili uchumi wa gesi unaokuja haswa pale mwaka 2022 ambapo faida ya ugunduzi wa gesi na mafuta zitaanza kuonekana” alisema Luanda. Alisema kuwa anawaomba wananchi wa Mtwara na vijana wote kujiingiza katika ujasiriamali kama vile ufugaji wa kuku na kulima bustani za mboga maana vitu hivyo vinahitajika na wageni wanaoingia katika shughuli za uchumi wa gesi Mkoani hapo. Naye meneja wa Shirika hilo hapa nchini Ostein Michelsen, alisema shindano hilo linawalenga vijana wa Mkoa wa Mtwara wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25 ambapo fursa imekuja katika eneo lao kutokana na Mkoa kukua kwa kasi katika Tanzania baada ya ugunduzi wa gesi na kuwepo kwa sekta hiyo hapa nchini. “Tungependa kuwapa hamasa vijana kushiriki kwa wingi katika fursa zinazojitokeza katika sekta ya gesi ili waweze kuona matokeo chanya kupitia biashara mpya katika Mkoa wao hivyo itakapofikia mwaka 2022 waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi huo” alisema Michelsen. Akifafanua zaidi alisema ndani ya chumba cha kompyuta kutakuwa na kompyuta 15 ambazo zitaunganishwa na mtandao wa intaneti ambapo wanafunzi na washiriki wa shindano hilo watazitumia katika kufanyia kazi ya kuendeleza mawazo ya biashara na kuchanganua zaidi mipango ya biashara zao. Alisema kuwa mwisho wa mashindano hayo kutakuwa na wajasiriamali watano watakaochujwa kutoka 40 wa mwanzo na kati ya hao mmoja atajishindia kitita cha dola za kimarekani 5,000 ili kuendeleza wazo lake, ambapo wale wengine wanne watapata dola 1,000 kila mmoja.

OLYMPUS DIGITAL CAMERA

Advertisements