WANAKIKUNDI WA TANGAZO KUJENGEANA NYUMBA

MWARABU2

WANACHAMA wa kikundi cha Jitegemee kilichopo katika kijiji cha Tangazo wilayani Mtwara mkoani hapa, wameazimia kujengeana nyumba bora za kisasa ili kuboresha maisha yao na kuendena na mabadiliko yanayotokea kwa sasa.

 

Akiongea na mwandishi wa habari hizi afisa mipango wa kikundi hicho Hassan Mwarabu, alisema kuwa katika mkutano mkuu wa kikundi hicho uliopita wanakikundi waliazimia jambo hilo na tayari utekelezaji wake umeanza.

 

“Wanakikundi tupo 16 na tumeweka mipango ya kujenga nyumba mbili kila mwaka hivyo katika kipindi cha miaka minane tutakuwa tumeshamaliza kujenga nyumba zote…kwa mwaka huu tumeanza na mbili ambapo tayari tumeshapata kiwanja kilichopimwa na sasa ujenzi unaendelea”, alisema Mwarabu.

 

Afisa mipango huyo alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo utatokana na kipato cha kikundi hicho kinachotokana na miradi yake ya ufugaji wa samaki, mavuni ya korosho, ufugaji wa nyuki na mapato ya pango la ofisi yake iliyopo kijijini hapo.

 

Mwarabu alisema kuwa kikundi kina jengo lake la ofisi lenye ukumbi wa mikutano na vyumba vitano ambavyo vyote vimepangishwa kwa mwekezaji ambaye analitumia jengo hilo kwa kuweka kiwanda cha kubangua korosho.

 

“Hili jengo letu tumelikodisha kwa mwekezaji ambaye anatulipa kodi ambayo sisi kwetu ni mapati…lakini licha ya sisi kupata kipato lakini tumesababisha ajira kwa wanakijiji wenzetu kwani kuna watu zaidi ya miamoja wanaofanyakazi hapa kiwandani na wengi wao wametoka hapa kijijini”, alisema Mwarabu.

 

Awali mwenyekiti wa kikundi hicho Issa Mchuzi alisema kuwa jengo hilo na mradi wa ufugaji wa samaki waliwezeshwa na shirika la maendeleo la kimataifa la UNDP kupitia kwa hifadhi ya muingiliano wa bahari na mto Ruvuma, Mnazi bay-Marine Park, ambapo walipewa jumla ya dola 50,000 zilizotumika kujenga jengo hilo la ofisi na kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki.

 

“Tulipewa fedha na wenzetu wa UNDP kupitia kwa Mnazi bay-Marine park…kwakweli jengo hili limekuwa mtaji mkubwa kwetu na hii miradi mingine yote imetokana na kodi tunayoipata kutokana na kukodisha jengo”, alisema Mchuzi.

 

Awali mwenyekiti huyo alisema kuwa kwa sasa kikundi chake kinatoa huduma ya matibabu kwa wanachama wake,kinasomesha watoto kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu kinatoa mikopo kwaajili ya kuendeshea miradi yao ya kiuchumi na kimekuwa ni kikundi cha mfano ambapo vikundi vingine kutoka maeneo mbalimbali vimekuja kujifunza.

 

Mwisho.

Advertisements