WAKULIMA WAAMBIWA,TAFUTENI MASOKO KWA MTANDAO

 

WAKULIMA wilayani Masasi moa wa Mtwara, wamehimizwa kumuia simu za mkononi na mitandao ya kompyuta kwa kutafuta ushauri wa kitaalamu wa kilimo na masoko ili kujikwamua na tatizo la ubora na soko la mazao wanayolima.

Wito huo ulitolewa jana na Katibu Tawala wa wilaya ya Masasi, Danford Peter, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mnara wa mawasiliano wa kampuni ya simu Tanzania (TTCL), katika kata ya Lupaso wilayani Masasi, ambapo alimwakilisha mkuu wa wilaya hiyo.

Alisema baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya mitandao ya mawasiliano ya kompyuta na simu za mkononi kwa kueneza ujumbe wa uchochezi na lugha chafu jambo ambalo halileti tija kwao, lakini alisema kama mitandao hiyo itatumika vizuri inaweza kuwa nyenzo muhimu kwa maendeleo hasa wakulima.

Aidha, Peter aliwataka wakulima kutumia simu na mitandao mingine kwa kutafuta masoko ya mazao wanayoyapata kutokana na kilimo ndani na nje ya maeneo yao wanayoishi kwa ajili ya kupanua wigo wa soko na kukuza kipato.

Alisema mitandao ni njia mojawapo ya kutangaza kiasi cha mazao yaliyopatikana hasa mazao ya ufuta, alizeti, choroko na korosho ambalo ndio zao kuu la biashara kwa mkoa wa Mtwara, na kwa kufanya hivyo wanunuzi watapa kufahamu wastani wa uzalishaji wa mazao katika maeneo husika.

“Tunafahamu kwamba korosho ndio zao pekee linalowapatia wananchi wetu kipato..sasa mitandao hii ni njia mojawapo ya kutangaza kwamba tunakorosho kiasi gani sisi tuliopo hapa Lupaso, tuna ufuta kiasi gani tuliozalisha, tuna alizeti kiasi gani tuchozalisha tunahitaji soko..sasa njia pekee ya kuwasiliana na kutangaza hivyo vitu ni kupitia mitandao.” Alisema.

Kwa upande wake, Meneja wa TTCL mkoa wa Lindi ambae alimwakilisha mkurugenzi wa kanda ya Zanzibar na kusini, Nicodemus Mngulu, alisema kupitia mfuko wa kusimamia utoaji wa huduma ya mawasiliano kwa wote nchini (UCSAF), kampuni hiyo ilipewa jukumu la kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 20 katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa mawasiliano vijijini.

“Katika kata hizo za mwanzo, Lupaso na Lipumbulu ni mojawapo ya kata zilizonufaika na mradi huo. Hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano kwa urahisi zaidi na pia kuchangia ukuaji wa maendeleo katika maeneo ya vijijini.” Alisema Mngulu.

Mnara huo uliozinduliwa unakuwa ni mnara wa tano wa kampuni hiyo kwa mkoa wa Mtwara, na kwamba unatoa huduma katika vijiji vitatu vya Lupaso, Mchoti na Lipumbulu vyenye wakazi zaidi ya 2,000, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

Mwisho.

kusini

Advertisements