ASASI ZIFANYE KAZI VIJIJINI

wanasikiliza

ASASI zisizo za kiserikali wilayani Tandahimba mkoa wa Mtwara, zimetakiwa kutekeleza miradi yao maeneo ya vijijini kuliko na watu wengi ambao wanahitaji kusaidiwa kwa kujengewa uwezo katika maeneo muhimu ya afya, elimu na kilimo badala ya kung’ang’ania mijini pekee.

Rai hiyo imetolewa juzi na afisa maendeleo ya jamii wa wilaya ya Tandahimba , Peter Nambunga. wakati akifungua mafunzo ya siku tatu juu ya usimamizi wa rasilimali za umma sekta ya afya na uwajibikaji wa jamii katika kilimo yaliyohusisha washiriki 90 kutoka kata za Mkundi, Chikongola na Mnyawa.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Mikundi farmers empowerment initiative MIFEIN chini ya mradi wake wa uwajibikaji wa jamii katika usimamizi wa rasilimali za umma (SAM/PETS) katika sekta ya afya na kufadhiliwa na Shirika la The Foundation for Civil Society (FCS) ambapo washiriki wote wanatoka katika vijiji vya kata hizo.

Nambunga, alisema kuwa asasi hizo zikifanya kazi vijijini zinaweza kuwahamasisha jamii kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na hivyo kuwapunguzia majukumu wahudumu namatokeo yake watapata muda wa kutosha kushughulikia masuala ya afya kwa jamii.

“Leo tunaona MIFEIN wakitimiza wajibu wao kwa mujibu wa mkataba wao na waliowafadhili…huu ni mfano mzuri wa kuigwa na asasi zingine hapa wilayani kwetu na sisi upande wa serikali tutahaikisha tunatoa kila aina ya msaada kwao ili lengo lao lifanikiwe…jambo holo ilibidi lifanywe na serikali lakini kutokana na ufinyu wa bajeti na kuwapo kwa mifumo mizuri ndio maana leo tunawaona wenzetu hawa wanatusaidia”, alisema Nambunga.

Aidha Nambunga aliwahimiza wananchi kutoa ushirikiano kwa asasi hizo ili ziweze kutimiza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuisaidia serikali kutatua matatizo yanayoikabili jamii katika nyanja za uchumi, afya, elimu na maeneo mengine kwani serikali imeona umuhimu wa asasi hizo na ndio maana imekuwa ikizisajili na kuziruhusu zifanyekazi.

Aidha nambunga, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kwamba pale asasi za kiraia zinapokwenda kwao kuwaelimisha ni budi wazingatie ili kuhalakisha maendeleo.

Alisema kuwa licha ya kazi nzuri zinazofanywa na asasi zisizo za kiserikali lakini serikali haitasita kuzichukulia hatua kali za kisheria zile zitakazokwenda kinyume na utaratibu uliowekwa ikiwa ni pamoja na kutumia fedha za wafadhili kinyume na malengo yake.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Mkundi, mwenyekiti wa MIFEIN, Salehe Rashidi, alisema kuwa, mafunzo hayo yanashirikisha washiriki kutoka katika makundi ya walemavu, wajumbe wa bodi za zahanati na wawakilishi wa wananchi kutoka katika vijiji vya kata za Chikongola, Mkundi na Mnyawa.

“Mheshimiwa mgeni rasmi mradi huu utatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo awamu ya iliyofuata ni kuunda Kamati ya PETs ambayo ilifanya ufuatiliaji ndani ya eneo la mradi, kisha kuandaa taarifa ya mradi na kutoa mrejesho kwa wadau mbalimbali katika mikutano na midahalo itayoandaliwa”, alisema mwenyekiti huyo.

 

Mwenyekiti huyo alisema kuwa mada zilitolewa na mtaalamu kutoka halmashauri yA wilaya ya Newala, Wilfred Mpanda na Abasi Imekuaji kutoka asasi za kiraia, ambapo alisema mada hizo zinatarajiwa kuibua mijadala miongoni mwa wananchi na ambayo ikifanyiwakazi itasaidia kuboresha huduma za afya kwa kiwango kikubwa.

 

MIFEIN ni Asasi ya Kiraia iliyoanzishwa Januari 2012 na kusajiliwa rasmi na serikali kupitia kwa Msajili wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. ikiwa na lengo kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa Sera mbalimbali za Taifa ikiwamo kilimo na Afya na makazi yake makuu ni katika kijiji cha Mikundi wilayani Tandahimba.

Mwisho.

 

 

 

Advertisements